Sunday, 22 May 2016

Tagged Under:

Madawati yawatoa jasho Ma- RC, DC

By: Unknown On: 21:46
  • Share The Gag

  • Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa.

    VIONGOZI wa serikali hususan wakuu wa mikoa na wilaya, wako katika heka heka za kutekeleza kutengeneza madawati. Lengo ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi atakayekaa sakafuni, kabla ya muda wa ukomo, waliopewa Rais John Magufuli .

    Wakati zikiwa zimebaki siku 39 kabla ya muda huo wa ukomo ambao ni Juni 30 mwaka huu, miongoni mwa maeneo ambayo gazeti hili limefanya ufuatiliaji, imeshuhudiwa mikakati mbalimbali ikitumika kwa ajili ya kupata fedha za utekelezaji wa agizo ikiwamo kuangukia wahisani.
    Baadhi ya wakuu wa mikoa wameelekeza halmashauri zao, kuhakikisha mapato ya vyanzo vya ndani yanaelekezwa kwenye utengenezaji wa madawati huku wengine wakishawishi wananchi kuchangia kwa hiari kutekeleza agizo.

    Hata hivyo, katika mchakato huo wa kutekeleza matakwa ya agizo, baadhi ya maeneo yamebainika kufanya uchakachuaji kwa kutengeneza madawati kwa kutumia mabanzi badala ya mbao ambao hata hivyo, umeshtukiwa na viongozi wa serikali wa maeneo husika.
    Uchakachuaji Vitendo vya matumizi ya mabanzi badala ya mbao kutengeneza madawati, vimebainika mkoani Tabora, ambako Mkuu wa Mkoa, Aggrey Mwanri amebaini hilo na kuagiza halmashauri zote zenye kufanya hivyo kuacha mara moja.
    Mwanri alibaini hayo hivi karibuni, alipofanya ziara katika wilaya za Igunga na Nzega, ambako aliagiza viongozi kufuatilia na kuhakikisha fundi yeyote atakayebainika kutengeneza madawati kwa kutumia mabanzi, asilipwe fedha.
    Mwanri alisema ni jambo la aibu, kuona madawati yakitengenezwa kwa mabanzi wakati mbao zipo. Aliahidi kurudi wilayani Igunga na Nzega, kupiga kambi kuhakikisha utengenezaji madawati unakamilika muda uliopangwa.

    Aidha aliagiza Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga, Alois Kaziyaleli kuhakikisha fedha zote zitokanazo na makusanyo ya vyanzo vya halmashauri, zinapelekwa katika utengenezaji wa madawati. Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Zipporah Pangani, Mwenyekiti wa Halmashauri, Peter Onesmo na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Jackilin Liana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Igunga, Jeremia Jomanga kwa nyakati tofauti, walimhakikishia Mwanri kuwa ifikapo Mei 30, watakuwa wamekamilisha utengenezaji madawati katika shule zote za wilaya ya Igunga.

    Kulingana na taarifa ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega iliyotolewa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani, Halmashauri imeidhinisha Sh milioni 100 kwa ajili ya kutengeneza madawati kabla ya muda wa ukomo. Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo ya Nzega, Emanueli Kitundu, alisema Januari mwaku huu kulikuwa na upungufu wa madawati 40,000, lakini mwezi huu upungufu ni madawati 10,000.

    Wahisani waokoa jahazi Miongoni mwa maeneo ambayo wahisani mbalimbali wamejitolea kuokoa jahazi la upatikanaji madawati ni mkoani Manyara, ambao ni moja ya mikoa 19 inayopakana na hifadhi 16 za taifa, iliyopokea fedha kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa). Tanapa ilitoa madawati 16,500 yenye thamani ya Sh bilioni moja kuunga mkono mkakati wa serikali. Hundi za fedha hizo zilitolewa kwa wakuu wa mikoa 19 mkoani Arusha mbele ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

    Madawati hayo yatasambazwa katika shule za msingi za wilaya 55 zinazopakana na hifadhi hizo. Vile vile hivi karibuni, kampuni za Tanzania Bundu Safaris na Rungwa Game Safaris, zilikabidhi madawati 90 kwa shule ya msingi Loiborsiret wilayani Simanjiro. Akipokea madawati hayo juzi, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mahmoud Kambona, alishukuru kampuni hizo na kusema huu ni wakati wa jamii ya wafugaji kupata elimu.
    Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro pia imepata wahisani wakiwemo Ubalozi wa Japan, ambao wamewatengenezea madawati 212 . Akitoa taarifa hivi karibuni kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Steven, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Theresia Mahongo alisema wamejipanga kukamilisha utengenezaji wa madawati 6,672 kabla ya Juni 30, mwaka huu.

    Alisema mahitaji ya madawati katika shule za msingi ni 16,244, yaliyopo ni 12, 572 na upungufu ni madawati 6,672 sawa na asilimia 34. “ Tumepata wahisani wa kututengenezea madawati 212 kutoka Ubalozi wa Japan na wengine ili kukamilisha madawati,” alisema Mahongo. Vile vile manispaa imepata kibali cha kuvuna miti sita, itakayowezesha kupasua mbao 9,000 zitakazotengeneza madawati 300.

    Aidha alisema pia imetengwa bajeti ya fedha kwa ajili ya madawati. Manispaa ya Moshi Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro, Jeshi Lupembe alisema halmashauri imetenga Sh milioni 20 zitakazotengeneza madawati 500 na kufanya madawati yaliyotengenezwa na halmashauri kuwa 750 na yaliyobaki 600 yatatolewa na wadau mbalimbali.

    Alisema wadau mbalimbali waliojitokeza kusaidia kuchangia madawati na idadi kwenye mabano ni Kampuni ya vinywaji baridi ya Bonite, walioahidi kutoa madawati 100, Benki ya Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro-KCBL (100), Chama cha Walimu na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa madawati 20 na wadau wengine.
    Alisema halmashauri imeshatoa Sh milioni 10 na kuomba kibali cha kukata miti mitano kwa ajili ya utengenezaji wa madawati 250 na vitanda 150 katika shule ya Moshi ufundi ambayo ndiyo ilikuwa na upungufu mkubwa.

    Dar yaandaa uchangishaji
    Kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ofisa Elimu wa Mkoa , Raymond Mapunda alisema mkoa huo umejitahidi kupunguza uhaba wa madawati kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ingawa bado upo upungufu.
    Alisema ili kumaliza tatizo hilo, wako kwenye maandalizi ya mwisho ya kualika wadau kwenye chakula cha jioni, hafla iliyopangwa kuzinduliwa kati ya Juni 2 na 3 mwaka huu ili kuwashirikisha wadau na wahisani mbalimbali.
    “Kama mkoa tuna mambo makubwa matatu tunayafanya ili kuhakikisha tunamaliza tatizo la miundombinu ya elimu hasa kwa upande wa madawati na vyumba vya madarasa, na jambo mojawapo ni hilo la kuzindua uchangiaji wa vitu hivyo kupitia chakula cha jioni tunachoandaa”, alisema Mapunda.

    Alisema mkoa una upungufu wa madawati 94,030 kwa shule za msingi na sekondari. Kwa upande wa vyumba vya madarasa, kuna upungufu wa vyumba 8,317. Akichanganua, Mapunda alisema katika shule za msingi, madawati yaliyopo ni 102,175 na upungufu ni 66,301 huku upande wa sekondari kuna viti na meza 99,189 na upungufu ni viti na meza 27,729.
    Hata hivyo alisema mwitikio wa wadau kuchangia miundombinu hiyo ni mkubwa. Hivi karibuni Umoja wa watoa huduma ya usafiri wa daladala jijini hapo, wameahidi kuchangia madawati 100. Mgawanyo huo ni kama ifuatavyo, wilaya ya Ilala wamepata Sh milioni 323, Temeke, 391 na Kinondoni 391. Halmashauri zenyewe zimetakiwa kujitengea fedha kutoka vyanzo vyao kwa ajili ya kununua madawati.

    Wananchi wachangishana Mkoani Simiyu, wakazi wa kijiji cha Luguru wilayani Itilima, katika kuunga mkono mkakati huo, wameamua kuchangishana Sh 10,000 kila kaya kwa ajili ya kutengeneza madawati 380 ya shule ya msingi kijijini hapo.
    Mwenyekiti wa kijiji, Dolnad Aloyce alisema waliwahamasisha wananchi kupitia mkutano wa hadhara kwa ajili ya kufanikisha lengo hilo. Kwa upande wa Wilaya ya Bariadi, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bariadi, Albert Rutahiwa, alisema “Tumebakiza siku 42 (sasa 39) kukabidhi madawati , hivyo wote kwa ujumla wetu jukumu letu ni moja tuhakikishe upatikanaji wa mawadati ifikapo Juni 30’’.

    Taarifa kutoka mkoa wa Pwani, zinasema wilaya ya Mkuranga hadi sasa, imefanikiwa kutengeneza madawati 5,043 kwa ajili ya shule za msingi na sekondari. Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Abdalla Kihato alitoa taarifa hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo aliyekuwa ziarani humo.
    Kihato alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kwamba hadi Juni 30, hawana wasiwasi tatizo la wanafunzi kukaa chini litakuwa limekwisha kwani wanashirikiana na wadau mbalimbali kutengeneza madawati. Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huo wa Pwani, Ndikilo mkoa huo ulikuwa una upungufu wa madawati 43,047 kwa shule za msingi lakini kwa jitihada zilizopo, tatizo limepungua kwa kiwango kikubwa.

    Vile vile, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa ameuhakikishia umma kuwa tatizo la uhaba wa dawati kwenye halmashauri zilizopo mkoani kwake litamalizika kabla ya Juni 30. Alisema kwa mkoa mzima wa Songwe mahitaji ya madawati ni 63,537 ambapo yaliyopo ni 49,692 hivyo pungufu ni madawati 11,804.
    Imeandikwa na Lucas Raphael, Igunga, John Gagarini, Kibaha, Joachim Nyambo, Mbozi, Kareny Masasy, Itilima, John Nditi, Morogoro, Ikunda Erick, Dar es Salaam na Arnold Swai, Moshi

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment