Saturday, 29 August 2015

Tagged Under:

Baba wa familia iliyoteketea: Ningeona miili nami ningekufa

By: Unknown On: 01:43
  • Share The Gag
  • Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad (kulia) akimfariji,  Masoud Mattar Masoud alipomtembelea nyumbani kwake kumpa pole jana. Mattar amepoteza familia yake ya watu tisa waliofariki katika ajali ya moto usiku wa kuamkia juzi. Picha na ofisi ya makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar 

    By James Magai, Mwananchi
    Dar es Salaam. Baba wa familia iliyoteketea kwa moto ndani ya nyumba walimokuwa wamelala, jijini Dar es Salaam, Masoud Mattar Masoud (59) amesema kama angeona miili ya familia yake, naye angekufa.
    Masoud alipoteza ndugu tisa baada ya nyumba yake kuteketea kwa moto, unaosadikiwa ulitokana na jiko la gesi.
    Katika tukio hilo lililotokea eneo la Buguruni Malapa, usiku wa kuamkia juzi, jumla ya watu tisa walifariki dunia kwa kuungua moto ndani ya nyumba hiyo namba 40, baada ya juhudi za wananchi kuwaokoa kushindikana.
    Walioteketea katika tukio hilo ni mama wa familia hiyo, Samira Juma Ibrahim (42) maarufu kwa jina la mama Aisha na watoto wake wanne; wavulana watatu na msichana mmoja. Watoto hao ni Ahmed Masoud (15), aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Msimbazi na Aisha Masoud (13), aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Alfurqan.
    Watoto wengine wa familia hiyo ni Abdillah Masoud (10), ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Alfurqan, pamoja na Ashraf Masoud (5).
    Mbali na watoto wa familia hiyo, wengine waliofariki katika tuki hilo ni mama yake Samira, yaani bibi wa familia hiyo, Bimdogo Masoud (72); mtoto wa dada yake Samira, Wadhati Saleh (27) na mtoto wake Fahir Fesal (mwaka mmoja na nusu) pamoja Samira Haroun (17).
    Wadhati ambaye alikuwa akiishi Magomeni, alikuwa mgeni katika nyumba hiyo na alifika nyumbani hapo asubuhi ya siku ya tukio hilo yeye na mtoto wake pamoja na Samira ambaye ni binti aliyekuwa akiishi naye.
    Mashuhuda wa tukio hilo walisema baada ya kusikia kelele za vilio, waliizunguka nyumba hiyo kwa lengo la kutaka kuwaokoa, lakini ilishindikana baada ya milango kutofunguka na moto kuwa mkali kiasi cha kushindwa kuingia.
     “Katika namna ya kujaribu kujiokoa, Ahmed alijaribu hata kurusha nje funguo ili waweze kufunguliwa mlango, lakini ilishindikana. Hivyo alirudi chumbani wakashikana pamoja kusubiri kifo,” alisema Suleiman Bashraf (45), ambaye ni kaka wa Samira.
    Bashraf, anayeishi Mikocheni na ambaye anasema alifika eneo la tukio wakati dada yake na watoto wake wakiwa wameshafariki, alibainisha kuwa baba wa familia hiyo, alikuwa kazini wakati wa tukio hilo
    Jana katika mahojiano na Mwananchi akiwa Kigogo CCM yaliko matanga kwa ndugu wa mkewe Masoud, ambaye ni baba wa familia hiyo iliyoteketea alisema, “Ninaushukru uongozi wa msikiti wa Gulam kunizuia kufika eneo la tukio na pengine hata mimi ningekufa palepale.”
    “Siku ya tukio mimi sikuwapo nyumbani, nilikuwa kazini na kwamba nilipata taarifa za tukio hilo kutoka Pemba kwa mjomba,” anaeleza.
    Masoud ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Kontena (TICTS) inayofanya kazi kwenye Bandari ya Dar es Salaam, anasema anapokuwa zamu ya usiku huwa anaondoka nyumbani saa 10 jioni na kupitia msikitini kufanya ibada na baada ya hapo anakwenda kazini.
    Masimulizi
    Masoud, huku akibubujikwa machozi kwa huzuni na kujifuta mara kwa mara anasimulia: “Siku ya tukio hilo kulikuwa na ugeni nyumbani kwangu kwani kulikuwa na mtoto wa dada wa mke wangu aitwaye Wadhati Saleh, huwa ana kawaida ya kuja karibu kila wiki kumsalimia bibi yake. Wadhati alifika asubuhi ya siku hiyo akiwa na mtoto wake pamoja na binti mmoja aliyekuwa akiishi naye aitwaye Samira.
    “Mtu pekee ambaye hakuwapo nyumbani wakati naondoka kwenda kazini alikuwa Ahmed ambaye alikuwa shuleni.
    “Kwa kawaida wakati ninapoondoka nyumbani mara nyingi huwa nataniana na mke wangu. Yeye huwa ananitania kuwa mbona unaondoka mapema hivyo nami huwa namjibu kuwa napitia msikitini kwanza. Hata siku hiyo wakati naondoka mke wangu ambaye alikuwa amekaa nje na mtoto wa dada yake (Samira) alinitania kama kawaida yake ‘mbona mapema hivi’, nami kama kawaida nilimjibu kuwa ‘napitia msikitini’.
    Basi mtoto wa Wadhati alinifuata, nikamchukua na nikamrudisha kwa mama yake halafu nikamuaga kuwa ningerudi kumchukua. Niliagana na familia yangu na nikaiacha ikiwa yenye furaha. Niliondoka hadi msikitini ambako nilifanya ibada kama kawaida na baada ya ibada nilikwenda kituoni ambako nilipanda daladala na kwenda kazini. Kule kazini nilizima simu na kuiweka kwenye chaji. Majira ya saa 10 alfajiri nilikwenda msikitini kwa ajili ya ibada ya alfajiri na kwamba baada ya kutoka msikitini, nilirudi kuchukua simu.
    Nilipoiwasha tu nilisikia milio kuashiria kuwa kuna simu nilikuwa nimepigiwa lakini sikupatikana. Punde kidogo nilipigiwa simu na mjomba wangu Suleiman Salim, kutoka Pemba. Aliniuliza kuwa niko wapi maana napigiwa simu sipatikani, nami nikamjibu kuwa niko kazini na simu yangu niliizima nikaiweka kwenye chaji. Kisha aliniambia niende haraka nyumbani kuna moto.
    Aliponiambia hivyo niliomba gari kazini likanipeleka nyumbani. Wakati tukiwa njiani nilipigiwa tena simu nyingine na mkwe wangu, Ali Saidi, mume wa mtoto wa dada. Alinitaka pia niende haraka nyumbani. Nilimuuliza kama kuna usalama lakini yeye akasisitiza tu kuwa niende haraka.
    Nilihisi kuna tatizo kubwa na pale pale akili yangu ikaanza kuchanganyikiwa. Nilipofika katika msikiti wa Masjid Gulam, nikasimamishwa na maimamu na waumini wengine waliokuwapo pale msikitini, wakaniambia nisiende huko nyumbani.
    Walifungua mlango wa gari wakanishusha na wakanichukua na kunipeleka hadi msikitini. Huko wakaniambia nipumzike humo kwanza huku wakinitaka niwe mstahimilivu. Imam Said na waumini wengine walinizunguka. Nikawaambia wanieleze nini kinaendelea kwa kuwa mimi ni mtu mzima, lakini waliendelea kunipa maneno ya kunifariji.
    Ndipo wakaniambia kuwa hawakutoa hata mtu mmoja katika ajali hiyo. Nadhani wakati ule waliponizuia kwenda kule nyumbani kwangu ndio wakati Polisi walikuwa wakizipakia maiti kwenye gari kuzipeleka hospitalini. Hali yangu ilibadilika sana na pengine kama ningeziona maiti nami ningekufa palepale.
    Nilikaa msikitini humo hadi asubuhi kwenye saa nne kasoro hivi nilipochukuliwa kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako miili ya marehemu ilikuwa imehifadhiwa kwa ajili ya taratibu za mazishi. Hata huko Muhimbili sikuruhusiwa kuiona miili ile na hata mimi sikutaka kuiona kwani nilikuwa nikiteseka sana kutokana na matatizo ya shinikizo la damu.
    Mke wangu alikuwa ndiyo dira yangu. Alikuwa mdogo lakini kaniongoza na kanistahimili kwa mambo mengi. Mke wangu alikuwa kiongozi wangu mambo mengi yeye ndiye alikuwa akiyafanya.
    Maalim Seif awasili
    Wakati mahojiano yakiendelea alifika Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inayoendeshwa kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Seif Sharrif Hamad.
    Maalim Seif aliwasili msibani hapo saa 5.46 asubuhi  na akatoa salamu za rambirambi akiwataka wafiwa kumtumaini Mungu na kuwaombea dua waliofariki. “Huyu (Masoud) siku yake ilikuwa haijafika ndiyo maana wakati haya yakitokea hakuwapo. Lakini hawa siku yao ilikuwa imefika. Hivyo tuwaombee dua kwa Mwenyezi Mungu.

    Created by Gazeti la Mwananchi

    0 comments:

    Post a Comment