Sunday, 15 May 2016

Tagged Under:

Uingereza Kusaidia Usambazaji wa Umeme Vijijini

By: Unknown On: 00:07
  • Share The Gag
  • Miezi  michache baada ya Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC) kujitoa kusaidia Tanzania katika usambazaji wa umeme vijijini, Serikali ya Uingereza kupitia taasisi yake ya Energy Africa Initiative, imetangaza utayari wa kutoa msaada huo.

    Waziri wa Uingereza wa Maendeleo ya Kimataifa, Justine Greening, ameeleza utayari huo mwishoni mwa wiki, katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliye nchini humo kumwakilisha Rais John Magufuli, katika mkutano wa kimataifa wa kupambana na rushwa duniani. Katika mazungumzo hayo, Greening alimhakikishia Waziri Mkuu Majaliwa, kwamba nchi yake iko tayari kuisaidia Tanzania kwenye mpango wake wa kupeleka umeme vijijini.

    “Tuko tayari kuwasaidia kutekeleza mpango huu kupitia taasisi ya Energy Africa Initiative ambayo inapata ufadhili kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID),” alisema. 
    Pia Waziri huyo wa Uingereza, alipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kupambana na rushwa na kwamba ndiyo maana Tanzania ilipewa mwaliko maalumu wa kushiriki mkutano huo, kwa vile baadhi ya mataifa yanaziona juhudi zinazofanywa na Serikali ya Rais Magufuli.

    Aidha, alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Mkuu kwa nia ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imeionesha katika kuwa na mpango wa kuendeleza viwanda. 
    Nguvu mpya Rea 
    Hatua hiyo ya Uingereza, imekuja wiki moja kabla ya kuwasilishwa kwa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini Alhamisi wiki ijayo, ambayo mjadala wake utafanyika kwa siku mbili za Alhamisi na Ijumaa, unatarajiwa kuibua hoja ya kufutwa kwa msaada huo wa MCC wa Dola za Marekani milioni 472, uliokuwa utumike kusambaza umeme vijijini.

    Mbali na mjadala huo ambao unatarajiwa kung’ang’aniwa na Kambi ya Upinzani Bungeni, hatua hiyo ya Uingereza itaongeza nguvu katika jitihada za Serikali zilizokwishaanza kwa mafanikio za kuwapatia Watanzania umeme wa uhakika.
    Taarifa za Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) zinaonesha kuwa, pamoja na MCC kujitoa Machi mwaka huu katika usambazaji umeme, Serikali katika Bajeti ya 2015/ 2016 inayoisha Juni mwaka huu, ilikuwa imeshatenga Sh bilioni 950 kwa ajili ya mradi wa Rea Awamu ya Pili.

    Mradi huo wenye lengo la kufikisha umeme kwa vijiji 2,500 na kuunganishia nishati hiyo wateja 250,000 nchi nzima, unatarajiwa kukamilika Juni 30, mwaka huu na kupisha kuanza kwa Rea Awamu ya Tatu, ambayo itaanza Julai mosi na kumalizika baada ya miaka miwili. 
    Jitihada zote hizo, lengo lake ni kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020, ambayo inataka hadi ifikapo mwaka 2020, wananchi waliounganishwa na umeme wafikie asilimia 60 na kiwango cha uzalishaji kifike megawati 4,915.

    Mbali na malengo ya Ilani hiyo, jitihada hizo pia zitachangia katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa inayotaka Tanzania iwe nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, ambayo imeweka lengo la usambazaji umeme liwe asilimia 50 mwaka huo mwaka 2025 na asilimia 70 mwaka 2033.

    Tayari Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameshaelezea nia ya Serikali kutaka sekta ya nishati itoe mchango mkubwa kufikia uchumi huo wa kati, kwa kuwa rasilimali za kufikia lengo hilo kupitia nishati zipo na kinachotakiwa ni dhamira na kasi ya kutekeleza.

    Katika kusisitiza kasi na dhamira hiyo ya Serikali, Waziri huyo amekuwa akielezea mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa dira hiyo, iliyotaka ifikapo mwaka 2015 uunganishaji umeme uwe umefikia asilimia 30. Lakini, kutokana na utekelezaji madhubuti wa dira hiyo, kiwango hicho kilivukwa lengo na kufikia asilimia 40 mwaka 2015.

    JPM na Marekani 
    Mbali na msaada huo wa Uingereza katika kusambaza umeme vijijini, Serikali ya Marekani pia imeelezea kuvutiwa na utendaji wa Rais Magufuli katika kupambana na rushwa, hatua iliyoanza kuvutia wawekezaji wa nchi hiyo.

    Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia Masuala ya Kimataifa, Sarah Sewall, katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu Majaliwa nchini Uingereza katika mkutano huo wa kimataifa, ameipongeza Tanzania kwa kupiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa.

    Alisisitiza kuwa kampuni nyingi za Marekani, zimeonesha nia ya kuja kuwekeza Tanzania. “Ninaamini uwekezaji huu utasaidia kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa watu. Tunampongeza Rais Dk Magufuli kwa juhudi anazofanya na nipende kusisitiza kwamba ushirikiano baina ya Tanzania na Marekani utaendelezwa katika maeneo yetu ya siku zote,” alisema.

    Majaliwa ashukuru 
    Akizungumza katika kikao chake na Waziri Sewall, Waziri Mkuu Majaliwa alimsisitiza asiache kusaidia kuwahimiza Wamarekani wengi waje kutalii Tanzania na wawekezaji zaidi waje kuwekeza nchini katika nyanja mbalimbali, ikiwemo uanzishaji wa viwanda, uongezaji thamani kwenye mazao yanayozalishwa nchini.

    Alimhakikishia kuwa Watanzania wamekuwa wakijifunza teknolojia mpya na za kisasa.

    Kuhusu mafanikio katika mapambano na rushwa, Majaliwa alisema mkutano huo wa kimataifa, uliojadili jinsi ya kupambana na rushwa duniani, ni kiashiria tosha kwamba tatizo la rushwa ni kubwa na linataka juhudi za pamoja katika kukabiliana nalo.

    Akizungumza na mawaziri hao, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kwamba viongozi wa Serikali wa Awamu ya Tano, wameamua kwa dhati kupambana na kila ovu, linalotokana na janga la rushwa na wameamua kuwajibika na kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.

    “Sasa hivi nchi yetu ina utamaduni mpya wa kufanya kazi na tumeamua kufanya kazi kwelikweli na siyo tena kwa mazoea, tumeamua kuweka utamaduni mpya wa kupiga vita rushwa, ili kuleta uwajibikaji na uwazi miongoni mwa watu wetu,” alisema.

    Alipoulizwa nini kimechangia kufanya Tanzania ing’are kimataifa katika vita hiyo, Waziri Mkuu alijibu kwamba Tanzania imetumia mambo manne ambayo ni kuzuia rushwa isitolewe ama kupokelewa, kampeni za kuelimisha jamii, kufanya mapitio ya sheria na kuwepo kwa utashi wa kisiasa.

    “Serikali inachukua hatua za kiutawala na kisheria, kama vile kuanzisha Mahakama Maalumu ya Mafisadi ambayo inatarajiwa kuanza kazi Julai mwaka huu,” alisema Waziri Mkuu.
    ==

    Credit; Mpekuzi Blog 

    0 comments:

    Post a Comment