KAMATI
ya Migogoro na Usuluhishi ya Bunge la Afrika Mashariki (EALA), imepanga
kuanza kusikiliza maelezo ya Serikali ya Burundi na chama tawala dhidi
ya hoja za wanaharakati wa haki za binadamu na vyama vya kiraia kutaka
ifutiwe uanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Vikao
hivyo vinatarajiwa kuanza Januari 25 hadi Februari 4, mwaka huu kama
njia ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu baada ya wanaharakati hao
kuwasilisha maombi mbele ya kamati hiyo ya Bunge.
Katika
hoja yao, wanaharakati hao wanaliomba Bunge hilo likutane, kujadili na
kutoa azimio la mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini humo, baada ya
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza kutangaza kujiongezea muhula wa
utawala.
Akizungumza
mjini hapa juzi mara baada ya kukamilika kwa hatua ya kusikiliza,
kujadili na kuwahoji wanaharakati hao Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Migogoro na Usuluhishi, Dk. Abdullah Mwinyi, alisema tayari wameshafanya
mawasiliano na Serikali ya Burundi kwa ajili ya kikao hicho.
Alisema siku ya kwanza walalamikaji ambao ni vyama vya kiraia walipata fursa ya kuwasilisha malalamiko yao ambayo yalisikilizwa.
Mwenyekiti
huyo alisema siku ya pili ilifuatia zamu ya wadau ambao ni watu kutoka
taasisi na asasi zisizo za kiserikali, walisikilizwa na kuhojiwa.
“Tulipokea
barua yao na tukawashukuru kwa kukubali kufika. Lakini tumewaomba
wafike Januari 25, mwaka huu kwa ajili ya kuwasikiliza, watasema
watakayoyasema na tutawauliza maswali baada ya hapo tutakaa kamati yetu
kupitia yote yaliyozungumzwa,” alisema Mwinyi na kuongeza:
“Baada
ya hapo tutatayarisha ripoti tutakayoiwasilisha ndani ya Bunge ambako
nako itajadiliwa na wabunge kisha kupitisha maazimio yatakayowasilishwa
kwenye Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao nao
watawasilisha mbele ya wakuu wa nchi wanachama,” alisema.
Alisema
dhamira ya kamati yake ni kuhakikisha wanamaliza kusikiliza pande zote
wakati wa vikao vya Bunge vinavyotarajiwa kuanza Januari 25, mwaka huu
mjini Arusha.
Chanzo Mtanzania.
0 comments:
Post a Comment