Mamia
ya wafanyakazi katika mashirika na taasisi mbalimbali za umma
zinazoendeshwa kwa hasara likiwamo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
wako hatarini kufutwa kazi kufuatia amri ya serikali ya awamu ya tano
chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli ya kupunguza mzigo wa gharama za
uendeshaji katika taasisi hizo.
Mashirika
hayo yameelezwa licha ya kuwa na watumishi wengi, lakini bado
uzalishaji na utendaji wake umekuwa hauna tija kwa taifa.
Hayo
yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Msajili wa Hazina, Laurence
Mafuru, katika kikao na wenyeviti wa bodi na wakurugenzi wa taasisi na
mashirika ya umma.
“Kuna
kampuni ambazo zimepewa mtaji na serikali, lakini zinashindwa
kuzalisha. Zinaandika barua kuomba msaada Serikali Kuu. Kama unaona
(mkuu wa taasisi) una wafanyakazi wengi na huzalishi kwa namna
inayotarajiwa, ni vyema upunguze watu,” alisema Mafuru.
Kadhalika,
licha ya kutoa maelekezo hayo, Mafuru alizitaja taasisi kadhaa
zinazoendeshwa kwa hasara au kuzalisha chini ya kiwango kinachotarajiwa
kuwa ni Tanesco, Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), Kampuni
ya Reli Tanzania (TRL), Shirika la Ndege (ATCL), Kampuni ya Simu
Tanzania ( TTCL) na Shirika la Bima la Taifa (NIC).
Maafuru
alizitaja taasisi na mashirika mengine yasiyofanya vizuri kuwa ni
Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Mamlaka ya Bandari (TPA),
Kampuni ya Miliki ya Rasilimai za Reli (Rahco) na Chuo cha Usimamizi wa
Fedha (IFM).
Mafuru
alisema Serikali haihitaji kuvuna fedha katika taasisi hizo, bali jambo
kubwa ni kuona kuwa zinajiendesha na kutimiza malengo yanayotarajiwa na
umma wa Watanzania.
“Serikali
haihitaji kuchukua fedha katika taasisi hizi. Isipokuwa tunataka
(taasisi za umma) zifanye kazi na ziwe nguzo za uchumi wa nchi. Tuache
bajeti inayotengwa (na serikali) ifanye kazi nyingine ya maendeleo kwa
Watanzania,” alisema, huku akiyataja Tazara na TRL kuwa ni vinara wa kuomba fedha kwa Serikali Kuu ili kulipa mishahara ya wafanyakazi wake.
“Kwa
mfano Tanesco, kwa kipindi chote ilichoanza kufanya kazi mpaka sasa
tulitarajia iwe imefanya kazi nzuri ya uzalishaji, lakini badala yake
tunaona kinyume chake na hapo isitegemee kwamba endapo itaendelea
kufanya hivyo serikali itakuwa inaangalia tu,” alisema.
“Ni
vema kama kuna shirika au taasisi ya umma ambayo inaona haizalishi na
ina wafanyakazi wengi iwapunguze wafanyakazi hao. Kama tunaona
tunashindwa, ni vyema tupunguze watu au turudi nyumbani tukapumzike,” alifafanua Mafuru.
Mafuru
aliongeza kuwa baadhi ya sababu za kufanya vibaya kwa taasisi na
mashirika ya umma ni uzembe wa baadhi ya watumishi ambao hawafanyi kazi
kwa kiwango kinachotarajiwa na wala kuwajibika ipasavyo katika kutimiza
majukumu yao.
Alisema
tatizo jingine ni viongozi wa baadhi ya taasisi na mashirika hayo ya
umma kuchukulia nafasi za uteuzi wanazopewa kuwa ni zawadi, fikra ambazo
hivi sasa wanapaswa kuzifuta mara moja na kutanguliza zaidi uwajibikaji
hasa kwa kutambua kuwa serikali ya awamu ya tano inaangalia zaidi
utendaji wenye matokeo chanya kwa umma na siyo kinyume chake.
“Msifikiri
kwamba nyie ndiyo wapishi (wajuzi) pekee… wapo watu wengine wanaojua
zaidi, kwa hiyo mjiandae kufanya kazi. Kila mtu atawajibika kwa nafasi
yake,” alisema.
Alisema
pamoja na kwamba serikali imezipa mali taasisi hizo kujiendesha,
lakini zimendelea kuwa mzigo kwa serikali kwani baadhi hushindwa
kuzalisha na kuwa vinara wa ‘kutembeza bakuli’ kwa maana ya kuomba
msaada kwa Serikali Kuu mara kwa mara.
Mafuru
alikitaja Chuo cha IFM kuwa ni mojawapo ya taasisi za serikali
zinazoshangaza kwani licha ya kuwa na fursa ya kuzalisha, bado kimekuwa
kikiendeshwa kwa hasara na kuwa miongoni mwa vinara wa kuomba msaada kwa
Serikali Kuu.
“Kwa
mfano Chuo Kikuu binafsi cha Tumaini, kinajiendesha kutokana na ada za
wanafunzi pekee. Kwa nini IFM inashindwa kufanya hivyo?” alihoji.
Alisema
taasisi zinazojiendesha kwa hasara zimekuwa mzigo mzito kwa serikali,
hivyo ni lazima sasa kwa wakuu wa taasisi husika kuhakikisha kuwa
wanaongeza ufanisi ili kujikwamua kutoka katika hali mbaya kiuchumi
waliyonayo.
“Hivi
sasa serikali ina taasisi 220 kutoka 600 zilizokuwapo awali. Pamoja na
kwamba taasisi za serikali zimepewa assets (mali) za kuzalisha, bado
(baadhi) zimeshindwa kufanya hivyo, badala yake nyingine kila siku
zinaandika barua kuomba fedha katika Mfuko Mkuu wa Serikali kuongezewa
mtaji,” alisema.
Katika
hatua nyingine, Mafuru alisema inasikitisha kuona kuwa Mamlaka ya
Bandari Tanzania (TPA) ni miongoni mwa taasisi zisizozalisha kwa kiwango
kinachotarajiwa na kwamba hadi sasa, hakuna faida yoyote ambayo imekuwa
ikirudisha serikalini.
Alisema kama TPA inafanya vizuri, ilitakiwa kufanya maendeleo mengine ikiwamo kujenga bandari nyingine.
Aliitaka taasisi hiyo na nyinginezo kama TPDC kujifunza kutoka kwa taasisi binafsi juu ya namna ya kuongeza uzalishaji.
Alisema
kutokana na uendeshaji wa hasara kwa baadhi ya taasisi na mashirika ya
umma, matokeo yake mashirika na taasisi hizo, kwa pamoja huchangia
asilimia 22 tu ya pato la Taifa kwa mwaka, hali ambayo haipaswi
kuendelea.
Wakati
huo huo, Mafuru alitoa agizo kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) kuwasilisha ripoti ya ukaguzi wa taasisi za umma ifikapo
Desemba 15, zikiwamo zote zilizobainika kuwa hazikuwa zikifanyiwa
ukaguzi hapo kabla.
Credit; Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment