Kiungo wa yanga Salum Telela akijaribu kumtoka kiungo na nahodha wa Mtibwa Sugar, Shaaban Nditi wakati
wa mechi ya Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara iliyofanyika juzi kwenye
Uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Yanga ilishinda mabao 2-o.
KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm amesema siri kubwa ya kikosi chake
kufanikiwa kuvunja mwiko wa kuifunga Mtibwa Sugar ilitokana na wachezaji
wake kucheza kwa nidhamu ya kiufundi.
Yanga iliondoka na ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa
kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro juzi ikiwa ni ushindi wake wa kwanza
uwanjani hapo tangu mwaka 2009.
Katika misimu iliyopita, Mtibwa Sugar wamekuwa wakionesha ubabe kwa
Yanga na kuwafunga, lakini mambo yamekuwa tofauti msimu huu ambapo Yanga
ilidhamiria kushinda na ikawa hivyo.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya mtandao, Pluijm alisema
amefurahishwa na kikosi chake kilicheza vizuri kwenye uwanja huo ambao
alikuwa akiuhofia kutokana na ubovu tofauti na alivyotegemea.
“Mchezo ulikuwa mzuri tofauti na nilivyotegemea kutokana na uwanja
jinsi ulivyo, wachezaji walicheza vizuri na kwa nidhamu ya hali ya juu,”
alisema kocha huyo Mholanzi. Alisema jambo lingine lililomfurahisha ni
wachezaji wake kuzingatia maelekezo yake na kuondoka na pointi tatu.
Ushindi huo umeendeleza rekodi ya Yanga ambapo tangu wameanza msimu
hawajapoteza mchezo hata mmoja wakiendelea kushika nafasi ya kwanza
kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa pointi 15 sawa na Azam FC
wakitofautiana katika mabao ya kufunga na kufungwa.
Baada ya mchezo huo, Yanga, Azam FC na Simba hawatakuwa na michezo
ijayo ya ligi kwa ajili ya kuwapa nafasi wachezaji walioteuliwa kwenye
timu ya Taifa kujiunga na kambi ya maandalizi ya mechi dhidi ya Malawi.
Kulingana na ratiba ya TFF, kesho Yanga ilikuwa icheze na African
Sports kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Azam FC dhidi ya Mtibwa Sugar
kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam na Ndanda FC dhidi ya
Simba mjini Mtwara, lakini mechi hizo zimeoneshwa zitapangiwa tarehe
nyingine.
Ratiba inaonesha timu zitakazocheza kesho ni Mgambo JKT dhidi ya
Coastal Union jijini Tanga, Majimaji itaialika Mwadui FC, Toto Africans
itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu wakati keshokutwa Stand United itacheza
dhidi ya Mbeya City na Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Tanzania
Prisons.
Baada ya mechi ya timu ya Taifa, Oktoba 17, mwaka huu, Yanga
watacheza na Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Simba
dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Saturday, 3 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment