Sunday, 11 October 2015

Tagged Under:

Simba waenda Mbeya

By: Unknown On: 07:41
  • Share The Gag
  • Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr
    KIKOSI cha wachezaji 20 cha Simba kinatarajiwa kuondoka leo kwenda Mbeya kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City utakaochezwa Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Sokoine.
    Akizungumza na gazeti hili jana kwenye mazoezi yaliyofanyika katika fukwe za Kunduchi, Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr alisema wanaenda kujificha jijini huko ili kuanza kuzoea mazingira ya baridi mapema kabla ya kuivaa timu hiyo.
    Kerr alisema wanakwenda Mbeya wakiwa na majeruhi wawili ambao ni Hamis Kiiza na Emery Nimuboma ambaye aliumia mkono kwenye mazoezi.
    “Tulikuwa na mazoezi makali, tunashukuru Mungu baadhi ya wachezaji wetu wako vizuri na wengine bado ni wagonjwa, tuna imani kwa wiki moja watakuwa wamepata nafuu na kuanza mazoezi,” alisema Mwingereza huyo.
    Kuhusu mchezo wa Mbeya City, Kerr alisema hawahofii hata kidogo kwani wana imani ya kupata pointi tatu.
    Alisema timu hiyo ya Mbeya haitawasumbua kwani tayari alifanikiwa kuiona katika mchezo wa Azam FC na kufuatilia kwenye DVD aina ya mchezo ambao wamekuwa wakitumia.
    Kerr alisema katika michezo iliyobaki hategemei kufanya vibaya tena kwani malengo yao ni kuchukua taji la ligi na kushiriki katika mashindano ya kimataifa.

    Created by Gazeti la HabariLeo


    0 comments:

    Post a Comment