Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli. |
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli amesema hayupo tayari kuona viongozi wakigeuka kuwa walalamikaji. Badala yake, amesema viongozi hao watabanwa, wachukue hatua na uamuzi mgumu kwa maslahi ya taifa na wananchi wake.
Magufuli ameahidi kukomesha mapigano na mauaji baina ya wafugaji na wakulima kwa kusimamia haki za kila kundi kikamilifu. Aidha, amesema ataweka mfumo mpya wa utoaji wa ruzuku za dawa za mifugo na pia kutoa dawa kwa wafugaji na kuchimba mabwawa ya kunywesha na kuosha mifugo.
Alisema hayo alipozungumza na wakazi wa miji mbalimbali ya Mkoa wa Pwani akiwa katika ziara ya kampeni kwa mkoa huo. Baadaye alifanya mkutano mkubwa wa hadhara katika mji wa Mkuranga.
Kuhusu viongozi kuchukua hatua badala ya kulalamika, Dk Magufuli alisema katika uongozi wake, kamwe hataunda serikali ya viongoziwalalamikaji, badala yake wanaochukua hatua kwa malalamiko ya wananchi.
“Sitakubali wafanyabiashara walalamike, wakulima walalamike, wafugaji walalamike, wavuvi walalamike; halafu eti na viongozi wanalalamika. Sasa kiongozi ukilalamika, nani achukue hatua na uamuzi mgumu kama sio kiongozi ili kumaliza malalamiko ya wananchi?” alihoji Dk Magufuli.
Alisema akiwa Waziri wa Ujenzi, alikuwa analala katika makambi mbalimbali kusimamia ujenzi wa barabara na madaraja, hivyo atapenda kuwaona mawaziri atakaowateua washinde na kulala katika miradi ya sekta zao ili kulifanya taifa kupata mabadiliko ya haraka kwa maendeleo ya wananchi.
“Kama mimi nililala barabarani wakati wa kujenga barabara hii (Dar- Mtwara- Tunduru), ole wake Waziri wa Ujenzi nitakayemteua afanye kazi kwa kushinda ofisini. Mimi mawaziri wa ofisini hawana nafasi, mtu wa aina hiyo ni bora nikimteua akatae.
“Kama ni Waziri wa Elimu akeshe kuinua elimu, kama ni wa Miundombinu akeshe kwenye miundombinu, kama ni wa afya akeshe kwenye afya, kama ni wa maji akeshe kwenye maji. Kamwe sitakubali Waziri wa kuja kurudisha nyuma azma yangu ya kuwafanyia kazi Watanzania.
Kwangu mimi ni Kazi Tu,” alisema. Kuhusu kukomesha mauaji baina ya wafugaji na wakulima, Dk Magufuli alisema atasimamia kuundwa sheria mpya, zitakazosimamia kilimo na ufugaji ili kuanisha haki na mipaka kwa kila kundi ili kufanya makundi hayo yasiingiliane, hatua ambayo imekuwa chanzo cha mapigano na mauaji.
“Ni lazima wafugaji waheshimu wakulima na wakulima ni lazima waheshimu wafugaji, lakini pia wakulima na wafugaji ni lazima waheshimu wavuvi. Serikali yangu itatambua na kuheshimu kila kundi kisheria. Mimi ni mtoto wa mkulima na mfugaji hivyo natambua nini nifanye ili kuboresha makundi haya,” alisema.
Alisema kwa muda mrefu sasa, taifa limekuwa likishuhudia matukio ya mauaji baina ya wakulima na wafugaji na kwamba hali hiyo haiwezi kuachwa ikaendelea kutokea, kwa vile licha ya kusababisha hasara kwa mali za wakulima na wafugaji, pia husababisha mauaji kwa watu wasio na hatia.
Aidha, mgombea huyo alisema katika uongozi wake, atamwaga mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ili waweze kuongeza mitaji na kuendesha shughuli zao kwa lengo la kukuza pato lao na pato la taifa na hivyo kusukuma maendeleo ya taifa.
“Watu wamechoka na umasikini, wanahitaji ukombozi na mtu muafaka kwa Tanzania mpya na ya maendeleo ya kasi ni Dk Magufuli, hivyo nawaomba mnichague,” alisema Dk Magufuli.
Akiwa Kibiti, aliahidi kuboresha miundombinu ya barabara, maji na kujengwa kwa hospitali ya kisasa itakayokuwa na uwezo wa kupima magonjwa mbalimbali, lakini pia kusaidia katika ujenzi wa mji wa Kibiti baada ya kupandishwa hadhi kuwa wilaya.
Akiwa wilayani Kilwa mkoani Lindi mapema jana, Dk Magufuli aliahidi kuubadili mji wa Kilwa Masoko ili kuufanya kuwa kitovu cha utalii kwa lengo la kuongeza thamani ya maisha na bidhaa katika wilaya hiyo, yenye utajiriwa kihistoria nchini.
Pamoja na kuhutubia wakazi katika miji mikubwa, Dk Magufuli amekuwa akisimama na kufanya mikutano midogo katika vijiji mbalimbali vya wilaya, hatua ambayo imekuwa ikimwezesha kukutana na wapigakura wengi wa maeneo ya vijijini.
Created by Gazeti la HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment