Msanii
wa Muziki wa Kizazi Kipya, Naseeb Abdul, Diamond akipokewa kwenye
Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere alipowasili kutoka Afrika Kusini
alikotwaa tuzo ya MTV Mama.
BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) na msanii Ambene Yesaya `AY’
wamewapongeza wasanii wa muziki wa kizazi kipya walioshinda tuzo
mbalimbali kwenye Tuzo za African Music Magazine Awards (AFRIMMA)
zilizofanyika jijini Dallas, Marekani.
Wasanii hao ni Nassib Abdul maarufu kama Diamond pamoja na Vanessa
Mdee ajulikanaye kama V Money. Katika tuzo hizo Msanii Diamond ameshinda
tuzo tatu ambazo ni Video Bora ya Kucheza (Best Dance Video), Msanii
Bora wa Mwaka (Best Artist of the Year) na Msanii Bora wa Kiume wa
Afrika Mashariki (Best Male East African Artist).
Vanessa Mdee ameshinda tuzo ya Msanii Bora wa kike wa Afrika
Mashariki. Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mngereza,
kuteuliwa kwa wasanii hao na baadaye kushinda katika tuzo mbalimbali za
Afrika na duniani ni ishara kwamba wasanii wa hapa nchini wanakubalika
ndani na nje ya Tanzania na kwamba hawana budi kuhakikisha wanatumia
fursa hizi katika kupanua wigo wa fursa za masoko kitaifa na kimataifa.
“Baraza linatoa wito kwa wasanii na wadau wote wa muziki kuzidisha
ubunifu, nidhamu, bidii, mshikamano na weledi katika kazi wanazozifanya
ili wasanii wengi wa Tanzania waweze kuchomoza katika tuzo na majukwaa
mbalimbali ya kimataifa kwa lengo la kulitangaza Taifa na kukuza soko la
kazi zao,” alisema Mngereza.
Aliongeza kuwa “ni matumaini ya Baraza kwamba wasanii wataendelea
kutambua umuhimu wa kufanya kazi na mapromota wenye upeo na mapenzi
mema, kufuata Sheria, Kanuni na taratibu za kutambuliwa na Serikali na
zaidi kuhakikisha wanapokwenda nje ya nchi wanafuata taratibu zote
sambamba na kukabidhiwa bendera ya Taifa kama ishara ya uwakilishi wa
Taifa letu”.
Diamond amekuwa ni msanii ambaye anawakilisha vyema ndani na nje ya
nchi kwa kushinda Tuzo mbalimbali kubwa ambapo amekuwa akisifiwa kwa
kazi zake mbalimbali za uimbaji pamoja na uchezaji wake mahiri.
Ambwene aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Facebook akisema
“Ninawapongeza Diamond, Vanessa Mdee na Ommy Dimpoz kwa ushindi wao
kwenye tuzo za AFRIMMA 2015,”. Msanii huyo ambaye aliwahi kushiriki
kwenye tuzo za MTV lakini hakushinda alisema ushindi wa wasanii hao
umeipa heshima Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 13 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment