*Wanaume wadaiwa kuiba za wake zao
NA ARODIA PETER, DAR ES SALAAM
ZIKIWA zimebaki siku 14 kabla ya Watanzania kupiga kura, baadhi ya
watu katika Kisiwa cha Goziba wilayani Muleba mkoani Kagera wanadaiwa
kununua vitambulisho vya kupigia kura vilivyotolewa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC).
Wakazi wa kisiwa hicho walipiga simu katika gazeti la MTANZANIA
wakimtuhumu mmoja wa wagombea udiwani wa Kata ya Goziba kupitia Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Masaba Nkunami, kuwa ndiye kinara wa ununuzi huo wa
vitambulisho hivyo kinyume cha sheria.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Rogers Mutalemwa alisema mgombea
huyo kwa kushirikiana na katibu wa chama chake (jina tunalo) wamekuwa
wakiwarubuni baadhi ya wananchi kwa kununua kadi zao kwa gharama kati ya
Sh 50,000 hadi 100,000 kila moja.
Mutalemwa alisema kadi hizo zimekuwa zikinunuliwa usiku kwa watu ambao hawana msimamo mkali wa kisiasa na wenye tamaa ya pesa.
Mkazi huyo alisema baada ya dau hilo kuwa kubwa baadhi ya wanaume
wameamua kuiba vitambulisho vya wake zao kwa ajili ya kujipatia fedha.
“Mimi ni mmoja wao, nasikitika kitambulisho changu sikioni nyumbani,
awali nilidhani nitakipata, lakini nilikuja kushtuliwa na wanawake
wenzangu walionieleza kuwa nao wameibiwa vitambulisho hivyo na waume
zao, ninaomba serikali itusaidie, tunaona haki yetu imepotea,” alisema
mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Marygolethi.
“Tunasikia diwani kwa kushirikiana na viongozi wengine wananunua
vitambulisho hivyo, tulisharipoti matukio hayo polisi, lakini hakuna
hatua zozote zilizochukuliwa kukomesha vitendo hivyo.
“Tulitoa taarifa kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Msaidizi wa Goziba
aitwaye Afande Jose, ambaye alipiga marufuku watu wasitembee usiku,
lakini bado mgombea huyo na watu wake wanaendelea na zoezi hilo,”
alisema Mutalemwa.
Mwananchi mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini
alisema baada ya vitendo hivyo kukithiri, walitoa taarifa kwa Mwenyekiti
wa Kijiji cha Goziba, Renald Mapesa, lakini hakutoa ushirikiano wowote.
Mwenyekiti huyo alipopigiwa simu alisema hawezi kuzungumzia suala
hilo, kwani yuko Mjini Bukoba kwenye semina. “Sina taarifa ya suala
hilo, sijawahi kulisikia, hata hivyo niko kwenye semina Mjini Bukoba,”
alisema.
Katika hatua nyingine, Nkunami ambaye anatuhumiwa kununua
vitambulisho vya kupigia kura alikamatwa na wananchi juzi saa nne usiku
akidaiwa kuwa kwenye harakati za kutoa rushwa kwa kundi la kina mama.
Mgombea huyo anadaiwa kukamatwa katika eneo la Zahanati, Kitongoji
cha Bwiminga, akiwa na kundi la wanawake na kusababisha taharuki na
vurugu kubwa kisiwani humo.
Baada ya kukamatwa, Nkunami alipelekwa katika Kituo cha Polisi Goziba ambako alihojiwa na kuandikisha maelezo yake.
Akisimulia tukio hilo, Ndozi Maboko ambaye ni kati ya vijana
walioshiriki kumkamata Nkunami, alisema walipata taarifa kutoka kwa
mmoja wa akina mama ambao waliandaliwa kwenda kukutana na mgombea huyo
wa CCM kwa lengo la kupewa pesa.
“Tulipopata taarifa hizo tuliwataarifu polisi ambao walitwambia
twende katika eneo hilo tuweke mtego wa kumkamata Nkunami, tulifanya
hivyo na tulifanikiwa kumkamata na kumpeleka kituo cha polisi.
Hata hivyo, Maboko alisema yeye na wenzake wawili, James Dotto na
Masha Pamba jana walikamatwa na kuhojiwa na polisi wakidaiwa kumvamia
Nkunami akiwa katika shughuli zake za kampeni.
Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, Nkunami alikiri kukamatwa na
wananchi ambapo alidai kuvamiwa akiwa katika matembezi ya kawaida.
“Niko hapa polisi naandikisha maelezo, ni kweli kuna vijana
walinivamia na kunikamata nikiwa eneo la Zahanati saa 2:30 usiku katika
shughuli zangu za kawaida, na si kweli kwamba nilikuwa nagawa rushwa.
Kuhusu kununua vitambulisho vya kupigia kura, Nkunami alisema:
“Siwezi kufanya hivyo, hayo ni maneno ya wanasiasa wanaonihofia baada ya
kuona ninawashinda,” alisema Nkunami.
MTANZANIA lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine
Olomi, ili azungumzie suala hilo, ambapo alisema alikuwa Dar es Salaam
kuhudhuria semina ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
“Niko nje ya kituo changu cha kazi, suala hilo siwezi kulitolea
ufafanuzi kwa sababu silijui, hivyo nitakupa namba ya msaidizi wangu
aliyeko huko ili uongee naye,” alisema Kamanda Olomi.
created by Gazeti la Mtanzania
Sunday, 11 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment