Wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, pamoja na kocha wao mkuu, Charles Mkwasa (kushoto
mbele), wakitoka katika ndege baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege
wa Julius Nyerere Dar es Salaam jana.
KOCHA Msaidizi wa Taifa Stars Hemed Morocco amesema baada ya kuvuka
hatua ya kwanza ya michuano ya kufuzu Kombe la Dunia, wanajipanga
kuimaliza Algeria katika mchezo ujao.
Taifa Stars imefanikiwa kuvuka hatua nyingine baada ya kuifunga
Malawi kwa juma ya mabao 2-1, wakifunga mabao 2-0 nyumbani na kufungwa
bao 1-0 ugenini. Akizungumza juzi baada ya mchezo dhidi ya Malawi
uliochezwa kwenye uwanja wa Kamuzu Banda jijini Blantyre Malawi, Morocco
alisema wanashukuru kwa kufanikiwa kuitoa Malawi, kwani wanarudi
kujipanga tena kwa ajili ya kuwamaliza Algeria.
Alisema licha ya kuwa Algeria ni timu bora Afrika, ikiwa watajipanga
wanaweza kufanya vizuri na kuwapindua. “Tunashukuru kuvuka hatua moja
bado tuna kazi ngumu na kubwa mbele yetu kuhakikisha tunaendeleza
ushindi katika mchezo ujao na kutengeneza historia mpya katika soka
letu,” alisema.
Hatua hiyo imeifanya Stars kutengeneza historia mpya ya kuifunga
Malawi, kwani kwa kipindi cha karibu mwaka mzima walichokuwa wakikutana
katika michezo ya kirafiki walikuwa wakitoka sare, ambayo kama siyo ya
kufungana basi ya kutokufungana.
Ushindi huo ni mwanzo mzuri wa Kocha Mkuu Charles Mkwasa na benchi
lake la ufundi ikiwa ni siku chache tangu kukabidhiwa mkataba wa kudumu
wa kuinoa timu ya Taifa. Kulingana na viwango vya Shirikisho la Soka
Duniani (FIFA) Tanzania inashika nafasi ya 136 wakati timu waliyoitoa
inashika nafasi ya 101 na timu wanayotarajia kukutana nayo ya Algeria
ikishika nafasi ya 19 kwa ubora duniani huku ikiwa ya kwanza Afrika.
Taifa Stars ilitarajiwa kuwasili jana ikitokea Malawi huku wachezaji
walioko katika kikosi hicho wakisubiriwa na timu zao kujiandaa na
michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoendelea mwishoni mwa wiki
ijayo.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 13 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment