Saturday, 3 October 2015

Tagged Under:

Lowassa aahidi kuanzisha benki ya mikopo nafuu

By: Unknown On: 00:48
  • Share The Gag

  • Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chadema, Edward Lowassa akiwasili katika viwanja vya Mwembe Yanga Temeke katika mkutano wa Kampeni jana.

    MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema anayeungwa mkono na vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, Edward Lowassa amesema akiteuliwa kuwa rais ataanzisha benki ya maendeleo kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wananchi wa kipato cha chini.
    Akihutubia katika viwanja vya Mwembeyanga, Dar es Salaam jana, Lowassa alisema kumekuwepo na ugumu wa kupata mikopo kwa wananchi wa kipato cha chini na hivyo akiteuliwa kuwa rais, ataanzisha benki itakayotoa mikopo kwa makundi hayo.
    “Natambua kuwa wananchi wa kipato cha chini wanapata tabu sana katika kupata mikopo na wengine hawapati kabisa, mimi mkiniteua kuwa rais wenu wa awamu ya tano, nitaanzisha benki ya maendeleo itakayowahudumia bila ubaguzi,” alisema Lowassa.
    Lowassa ambaye amekuwa akidai anakerwa na umasikini, ameendelea kusisitiza azma yake kuwa endapo wananchi watampatia ridhaa ya kuwa rais, ataondoa umasikini uliokithiri nchini na kumfanya kila Mtanzania kunufaika na rasilimali za nchi yake.
    Aidha, alisema ili aweze kufanikisha malengo aliyojiwekea pamoja na ilani ya chama chake, atahakikisha elimu inakuwa bure kwani hakuna maendeleo bila ya kuwepo na watu waliosoma na kuelimika.
    Lowassa alisema nchi ya Tanzania ina fedha nyingi pamoja na rasilimali za kutosha hivyo ahadi anazozitoa ana uhakika wa kuzitekeleza kwa kutumia fedha za ndani na sio kutegemea misaada ya wahisani.
    Naye mgombea ubunge wa Jimbo la Temeke kupitia CUF, Abdallah Mtolea alisema endapo atateuliwa kuwa mbunge wa Temeke, atahakikisha jimbo hilo linakuwa na maendeleo stahiki kulingana na rasilimali zilizopo katika jimbo hilo.
    Mtolea alisema ataboresha huduma za afya, elimu pamoja na maji ili wananchi wanufaike na matunda ya uongozi bora ndani ya nchi yao. Katika ziara zake za kutafuta uungwaji mkono na wananchi, Lowassa jana alifanya mikutano yake jijini Dar es Salaam katika maeneo ya Mwembeyanga (Temeke), Segerea (Ilala), Sinza katika Jimbo la Ubungo na Jimbo la Kawe katika Manispaa ya Kinondoni.
    Created by Gazeti la HabariLeo

    0 comments:

    Post a Comment