Rais Jakaya Kikwete akitembelea mradi wa kufua umeme kutokana na gesi asilia baada ya kuzindua mradi huo Kinyerezi Dar es Salaam jana. (Picha na Freddy Maro). |
RAIS Jakaya Kikwete amezindua kituo cha kufua umeme kwa mitambo ya gesi asilia cha Kinyerezi I na kutaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuchangamkia fursa ya upungufu wa umeme Afrika ili kuwa na uhakika wa mapato.
Alisema duniani umeme unaozalishwa ni megawati milioni 5,255,000 na mataifa makubwa matano yanazalisha asilimia 55 wa megawati hizo, ambayo ni China inaongoza kwa megawati milioni 1,146,000, Marekani milioni 139,000, Japan 287,000, Urusi 223,000 na India 280,000.
Alisema megawati zinazobakia, ndiyo nchi nyingine 193 zinazotambulika na Umoja wa Mataifa wanagawana, ambapo Afrika zinazalishwa megawati 111,786, idadi ambayo hata nusu ya India haifikii.
Alisema Afrika Kusini wanaongoza kwa kuzalisha megawati 44,260, Misri megawati 26,910, Algeria megawati 11,330, Libya megawati 6,763, Morocco megawati 6,620 na Nigeria megawati 5,600.
Rais Kikwete alisema katika nchi za Afrika Mashariki, Kenya inaongoza kwa megawati 2,465, Tanzania 1,498, Uganda megawati 850, Rwanda megawati 110 na Burundi megawati 53, hali inayoonesha kuna tatizo kubwa la upatikanaji wa umeme.
“Lakini kwa kuwa nchi yetu imejaliwa vyanzo vingi vya nishati ni fursa na kugeuza kuwa biashara, kwani Kenya wanahitaji megawati 1,000, Rwanda, Zambia na wengineo wanataka kwa haraka huku wengine wakitaka kujenga bomba la kupeleka gesi wenyewe,” alisema.
Alisema kwa sasa nchi inapita kwenye changamoto, kwani umeme wa maji unaingiza megawati 561 katika gridi ya taifa, lakini sasa zinazoingia ni megawati 105 na upungufu ni megawati 450.
Alisema alitegemea kutakuwa na vituo zaidi kuzalisha umeme, kwani bomba lina uwezo wa kusafirisha gesi kutengeneza megawati 3,000, lakini bado kuna nafasi kufikia malengo kwa kujenga haraka vituo vingine.
Alisema katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano unaokamilika mwakani mwishoni, lengo ni kufikisha megawati 2,780, lakini sasa kuna megawati 1,490, hivyo kudaiwa megawati 1,390. Alisisitiza kwamba jitihada zinahitajika kufikisha hizo mwakani.
Alisema baada ya kukamilika Kinyerezi I, mwezi ujao itakamilika Kinyerezi II na Januari mwakani Kinyerezi III, hivyo ni lazima kuongeza kasi. Kikwete aliwataka Tanesco kuongeza kasi ili kuchangamkia fursa na kuingiza umeme haraka na kupunguza mgao uliopo sasa.
Alisisitiza shirika hilo la umeme kuzingatia sheria ya manunuzi kwa umma. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Ngosi Mwihava alisema katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete, vituo vya kufua umeme vya megawati 484.8 vimejengwa na pia asilimia 47 ya mitambo ya kufua umeme imejengwa .
Alisema, miradi mingi ya kufua, kusafirisha na kusambaza umeme inaendelea na ujenzi. Alisema tangu Septemba 17 mwaka huu, walipoanza kuwasha mitambo ya gesi asilia, wameongeza megawati 200 ambazo hazikuwepo kabla ya gesi kuanza kusafirishwa, vinginevyo hali ingekuwa mbaya zaidi, kwani kungekuwa na ukosefu wa megawati 400.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema kituo hicho kimoja, kati ya vinne vinavyojengwa, vikikamilika , vina uwezo wa kutoa megawati 1,500. Kituo cha Kinyerezi I kimegharimu Sh bilioni 400.
“Kwa sasa mitambo miwili yenye uwezo wa kuzalisha megawati 70 ndiyo imeishajaribiwa na tayari inazalisha umeme na miwili iliyobaki ina jumla ya megawati 80 itaanza kujaribiwa na itakamilishwa na kuunganishwa mwisho wa mwezi huu,” alisema.
created by Gazeti la HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment