Jeneza |
Akizungumza juzi katika makaburi ya Kawajense mjini baada ya maziko ya mmoja wa waumini wa kanisa hilo, Rose Paulo (83), Kamtupe aliyeongoza ibada ya maziko, alisema umefika wakati wanawake washiriki kazi hizo za maziko ili kukamilisha ajenda hiyo ya hamsini kwa hamsini na usawa katika jamii.
“Utaratibu wa ushiriki wa hamsini kwa hamsini wa wanawake tumeushuhudia ukifanyika katika ulingo wa siasa na kwenye uteuzi katika nafasi mbalimbali za uongozi nchini. “Sasa kwanini kwenye shughuli za maziko haiko hivyo? Kwa nini hapa ni akina baba tu wanaojitokeza kubeba mwili wa marehemu na kuuingiza kaburini kisha kuufukia? Mbona hapa hakuna huu utaratibu wa hamsini kwa hamsini wa ushiriki wa wanawake?” Alihoji Katekista huyo.
Kiongozi huyo wa dini, alishauri wanawake kutowaachia wanaume kazi hizo za maziko, bali wakiwaona wamebeba mwili, nao wajitokeze kushirikiana nao.
“Nawaomba akina mama na nyie mkiona wanaume wamebeba jeneza mabegani lililohifadhi mwili wa marehemu wakienda mazikoni, basi nanyi mshiriki kubeba jeneza hilo kwa zamu. “Pia wakati wa kufikia udongo kaburini na nyie wanawake mshiriki msiwaachie akina baba pekee yao kuifanya kazi hiyo,“ alisisitiza Kamtupe.
Hoja ya katekista huyo ilizua mjadala mkali makaburini hapo, ambapo akina mama walimpinga wakisisitiza kuwa kushirikiana shughuli za maziko kwa hoja ya hamsini kwa hamsini haitawezekana.
Walisisitiza kuwa kama wanataka shughuli zifanyike hamsini kwa hamsini, basi na wanaume nao walie msibani, kwani ni wanawake pekee wamekuwa wakisikika wakilia kwa sauti za juu na kuomboleza msibani.
“Iwapo wanaume watakubali kuangua kilio kwa kupaza sauti kama tunavyofanya sisi akina mama, basi na sisi tutakuwa tayari kushiriki katika maziko ya marehemu kwa kuchimba kaburi, kubeba jeneza na kufukia udongo kaburini,“ alisema mmoja wa wanawake hao kwa masharti ya kutoandikwa gazetini.
Created by gazeti la HabariLeo
0 comments:
Post a Comment