Katika mechi ya kwanza iliyofanyika Jumatano wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Stars ilishinda kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Kwa matokeo hayo, Taifa Stars kesho inahitaji sare ya aina yoyote au isifungwe zaidi ya bao 1-0 ili kutinga hatua ya pili ya mchujo huo ambapo itakumbana na timu bora barani Afrika, Algeria.
Kwa hiyo, mechi ya kesho ya Taifa Stars ni muhimu sana kwa sababu ni ukweli kuwa bado uhakika wa kuingia hatua ya pili ya mchujo haupo kutokana na ukweli kwamba Malawi haijakata tamaa na ilionesha soka ya kuvutia katika mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa.
Hivyo basi, wachezaji wa Taifa Stars na benchi lao la ufundi chini ya Kocha Mkuu Charles Boniface Mkwasa halina budi kufahamu kuwa ndio kwanza safari bado mbichi kwani hawana uhakika wa kusonga mbele, na uhakika huo utapatikana kama wataingia uwanjani kesho wakipania kupata matokeo mazuri.
Tunafarijika na hatua ya Mkwasa kuwa ataingia kikosi chake uwanjani akilenga kushambulia na siyo kulinda mabao mawili aliyoyapata Dar es Salaam ili kuwa na uhakika wa kusonga mbele na kukumbana na Algeria.
Mkwasa amesema wameondoka nchini jana wakiwa na lengo la kupata ushindi, hali inayotia moyo na kujenga imani kuwa timu imepania kusonga mbele katika michuano hii mikubwa duniani na kufuzu kwa fainali zake.
Kwa mchezo uliooneshwa na kikosi cha Stars katika mechi ya kwanza, hatuna shaka kwamba inao uwezo wa kupata matokeo mengine mazuri ugenini na kujipatia tiketi ya kuikabili Algeria na kujisogeza katika hatua nzuri ya kucheza makundi ambayo ndio lengo kubwa na hatua muhimu ya kwenda Urusi 2018.
Ili haya yote yaweza kupatikana, ni lazima Taifa Stars ijipange kuanzia mechi ya kwanza na ya marudiano kesho ikifahamu kuwa kama tulivyoeleza katika maoni yetu wiki iliyopita kwamba kufuzu kwa fainali za Urusi 2018 inawezekana, lakini ikihitaji nidhamu ya hali ya juu mchezoni ili kupata ushindi.
Kwa uwezo uliooneshwa na kikosi cha Stars tangu kiwe chini ya mikono ya Mkwasa, hatuna shaka kuwa uwezekano wa kuitoa Malawi na kisha Algeria na kuingia hatua ya mwisho ya makundi, ni jambo linalowezekana na litafanikiwa kama Watanzania wote wataendelea kuiunga mkono timu yao na kupewa sapoti inayohitajika.
Wakati tukiipongeza Taifa Stars kwa ushindi dhidi ya Malawi na kuitakia kila la heri katika marudiano kesho, tunaitaka ifahamu kuwa safari ndio kwanza imeanza na bado ni ndefu, isibweteke, ikaze buti na ijitume ikipania kuweka rekodi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2018. Inawezekana kila mmoja akitimiza wajibu wake.
Created by Gazeti la HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment