Kikosi cha JKT Ruvu.
TIMU ya JKT Ruvu msimu huu imeanza vibaya michuano ya Ligi Kuu
Tanzania Bara. Imeanza vibaya kwa sababu imecheza michezo sita,
imepoteza mitano na sare moja ukilinganisha na misimu mingine mambo ni
tofauti kabisa.
Ukiangalia msimu uliopita, ni miongoni mwa timu za Jeshi ambazo
zilionesha mwelekeo kwa kufanya vizuri katika michezo yake ya awali na
hadi msimu unakwisha ni JKT Ruvu. Kocha Minziro Pia, katika historia ya
Kocha wa JKT Ruvu, Fred Minziro na timu hiyo hawajahi kufanya vibaya
kiasi hicho, jambo ambalo hata yeye mwenyewe ni kama ameshtuka na kutaka
kujivua kuendelea kuifundisha timu hiyo.
Timu hii ya JKT Ruvu msimu uliopita ilionesha upinzani wa hali ya juu
kwa maana kwamba, iliwahi kukimbizana na Mtibwa Sugar kwa kuongoza ligi
kwani ilikuwa ikijitahidi kufunga katika mechi za ugenini na nyumbani
wakati huo wakiwa wanatumia uwanja wa Azam Complex, Chamazi. Tangu
Minziro alijiunge na timu hiyo miaka kadhaa iliyopita, alipata mafanikio
lakini inashangaza msimu huu hali imekuwa tofauti kabisa, ambapo hadi
sasa inashika mkia katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16.
Kufungwa sana Ukilinganisha na timu nyingine, hii imefungwa mabao
mengi wakati ndio kwanza wamecheza mechi sita hadi sasa huku ikishikilia
mkia ikiwa na pointi moja moja iliyoipata katika sare. Kiujumla timu
hiyo haijawahi kushinda mchezo wowote hadi sasa na imeshafungwa mechi
tano na kutoka sare mara moja tu. Katika mchezo wao wa hivi karibuni
dhidi ya Toto Africans uliochezwa Mwanza, JKT Ruvu ilifungwa bao 1-0.
Aidha, pointi moja waliyonayo ilitoka katika mchezo dhidi ya Kagera
Sugar ambapo walitoka sare ya bila kufungana katika mchezo uliopigwa
Tabora. Walicheza na Stand United katika uwanja wao wa nyumbani msimu
huu wa Karume wakafungwa bao 1-0. Wakafungwa na Yanga mabao 4-0,
wakafungwa na Mbeya City mabao 3-0, wakafungwa na Majimaji 1-0 huko
Songea. Ndio timu pekee ambayo inaongoza kwa kufungwa mabao 10 huku
ikiwa haijafunga hata bao moja.
Timu nyingine inayofuatia ni Coastal Union yenye pointi tatu
inayohitaji kubadilika ili kufanya vizuri. Coastal nayo imekuwa tofauti
msimu huu kwa kupoteza michezo ya nyumbani na ugenini. Kama timu hizo
hazitabadilika huko zinakokwenda hali itakuwa mbaya kwao kwani kila timu
inajitahidi kuhakikisha inajiweka kwenye mazingira mazuri. Usajili wake
Kama ni usajili mzuri timu hii imejitahidi kwa kusajili wachezaji
wanaofahamika na wenye uwezo mkubwa kiasi fulani.
Katika kujiimarisha ilimsaili Gaudence Mwaikimba ambaye alitemwa Azam
baada ya mkataba wake kuisha, ilimsajili mchezaji matata wa JKU
Zanzibar, Omar Janja ambaye alifanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la
Mapinduzi msimu uliopita. Maandalizi awali JKT Ruvu ilifanya maandalizi
mazuri kabla ya kuanza kwa msimu mpya huku wakisafiri mikoa tofauti na
kucheza mechi za kirafiki.
Kwa hakika mechi ambazo walikuwa wakicheza ziliwapa mwanga kwamba
watakuwaje katika kukabiliana na upinzani wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Changamoto kubwa katika maandalizi yao ni kubaki wachezaji wengi raia
wakikaa kwa pamoja katika michezo hiyo huku wengine ambao ni wanajeshi
wakiwa katika kundi lingine linalojiandaa na michuano ya Majeshi
iliyofanyika Uganda.
Kikosi cha JKT Ruvu chenye wachezaji mchanganyiko wa wanajeshi na
raia hakika huwa kinakuwa kwenye mazingira magumu kama hayo hasa wengine
wanapoondoka kwenda mashindano ya Majeshi, wengine wanapokwenda kwenye
kozi za Kijeshi. Watawezaje kucheza soka la ushindani kama kuna
mgawanyiko huo ndani ya timu moja ambayo inasaka nafasi ya kuchukua taji
la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kama ilivyo kwa timu nyingine.
Ni wazi kuwa uongozi wa timu hiyo unahitaji kuwa na jicho la pili
kama kweli wanataka timu yao kufanya vizuri, la sivyo itabaki kuwa
mshiriki tu na mwisho wa siku wanashuka daraja. Kauli ya Minziro Kocha
Fred Minziro anasema anapenda timu ifanye vizuri, lakini kuna changamoto
nyingine ziko nje ya uwezo wake anashindwa kusema lakini zinachangia
kwa kiasi kikubwa timu kushindwa kufanya vizuri. Anasema kitu
kinachomshangaza zaidi ni timu yake kufanya mambo tofauti.
Inapokuwa kwenye mazoezi hufanya vizuri kama inavyoelekezwa, lakini
wanapoingia uwanjani mambo huwa tofauti kabisa. “Sijui kinachotokea ni
kitu gani, lakini nimekuwa nikijitahidi kuwasisitiza wachezaji wangu
kufanya yale ninayowaelekeza lakini wanapoingia uwanjani hucheza
wanavyojua wao,” anasema. Minziro anasema kwa matokeo hayo hata yeye
mwenyewe hakuridhika na yuko tayari kuwajibika kama itahitajika hivyo.
Anasema kuliko kuendelea kufundisha timu na kupata matokeo mabaya ni
afadhali kuachia ngazi kwani hapendi matokeo mabovu. Baada ya mchezo
dhidi ya Stand United uliochezwa kwenye uwanja wa Karume na kufungwa bao
1-0, kocha huyo alitaka kujivua kibarua chake. Kocha huyo alikataa
kusafiri na timu kwenda Tabora na kumuachia Kocha wake Msaidizi Greyson
Haule.
Licha ya Minziro kutaka kuachia ngazi, Ofisa Mteule Daraja la Pili
Constatine Masanja anasema kuwa bado suala lake linafanyiwa kazi na sio
kweli kama amechia ngazi. Anasema anaendelea kufanya mazungumzo na
uongozi wa timu hiyo na kama itashindikana itawekwa wazi wakati wowote.
“Minziro bado ni kocha wetu na ana mkataba wa kuifundisha JKT Ruvu, bado
hajaachia ngazi kama baadhi ya vyombo vya habari vilivyotangaza, kama
kuna lolote litatokea tutawaeleza,” anasema
Hata hivyo, hakuna sababu yoyote ya wao kukata tamaa isipokuwa
waangalie ni wapi wamekosea kwani bado ndio kwanza ligi imeanza na hiyo
ni michezo michache kama watajirekebisha mapema wanaweza kubadilisha
matokeo. Uongozi wa timu uzungumze na kocha na pengine wachezaji
watagundua matatizo yaliyojificha ambayo wengine hawayafahamu.
Kama kweli wamedhamiria kucheza michuano ya Ligi Kuu sio tu katika
kujiburudisha bali pia, soka ni biashara na kwa jinsi ambavyo watapigana
na kuendelea kubaki watanufaika. Ikiwa wataruhusu timu hiyo kushuka
daraja itajiweka kwenye mazingira magumu ya kupambana ili kupanda tena.
Mapungufu yao yanahitajika kurekebishwa kuanzia sasa na kurudisha Ruvu
mpya ya wakati ule.
Kufanya marekebisho kuanzia sasa inawezekana kuibadilisha timu hiyo
na kurudisha kiwango chake, lakini kama itaendelea kufanya vibaya, basi
itakuwa sawa na sikio la kufa ambalo alisikia dawa.
Created by Gazeti la HabariLeo
Sunday, 11 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment