Na Bakari Kimwanga, Bagamoyo
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John
Magufuli, amesema kugundulika kwa gesi wilayani Bagamoyo kutatimiza
ndoto yake ya kuijenga Tanzania mpya ya viwanda.
Dk. Magufuli ametoa kauli hiyo wilayani Bagamoyo, katika mikutano
yake ya kampeni aliyoifanya kwenye majimbo ya Chalinze na Bagamoyo.
Alisema Tanzania mpya yenye kutoa ajira kwa vijana na kuwawezesha
wanawake na wazee kiuchumi inakuja chini ya Serikali ya awamu ya tano,
ambayo alitabiri yeye kuwa kiongozi wake.
“Kwanza niwapongeze wananchi wa Bagamoyo kwa kugundulika gesi hapa
kwenu katika eneo la Ruvu. Na hii itasaidia sana kuijenga Tanzania mpya
ya Magufuli ambayo itachochea ujenzi wa viwanda.
“Ukishakuwa na gesi, barabara za kutosha na umeme wa uhakika ni wazi
vitasaidia sana ujenzi wa viwanda na kutoa ajira nyingi kwa vijana wa
Bagamoyo na Tanzania kwa ujumla,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema kugundulika kwa gesi kutasaidia Mkoa wa Pwani na maeneo ya jirani kupaa kimaendeleo.
“Tanzania yetu Mungu anaipenda sana ndiyo maana na mimi nikaomba
urais ili niweze kuijenga na hata kusimamia rasilimali za Watanzania kwa
uadilifu, kikubwa ninawaomba mniamini na kunichagua kwa kura nyingi ili
niwe rais wa Jamhuri ya Muungano,” alisema Dk. Magufuli.
Aidha Dk. Magufuli alimsifu Rais Jakaya Kikwete kuwa amefanya kazi
kubwa ya kuiletea maendeleo Tanzania na hasa kuiinua kiuchumi.
“Rais wa awamu ya nne ametoka hapa Chalinze, Bagamoyo ameongoza kwa
miaka 10, nami nimekuwa msaidizi wake kwa miaka 10. Alikuwa akinituma na
kazi hii nimeifanya kwa umakini mkubwa, ikiwemo ujenzi wa barabara.
“Nami sasa nimeteuliwa na chama changu (CCM) kuwania nafasi hii, wana
Bagamoyo na Watanzania kwa ujumla sitawaangusha, ninaomba mniamini
ndugu zangu kwa kunichagua kwa kura nyingi,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema anajua eneo la Chalinze watu wake hujishughulisha na kilimo,
kikiwemo cha mananasi na kwamba serikali yake itahakikisha inajenga
kiwanda cha kusindika matunda kama njia ya kupandisha thamani ya zao
hilo kwa kuwa na soko la uhakika.
“Ninawaomba mnichagulie Ridhiwani awe mbunge wa Chalinze, ninahitaji
kufanya naye kazi. Huyu ni mwanangu kabisa pamoja na kuwa ni mtoto wa
rais, lakini hana majivuno.
“Na kwa upande wa Bagamoyo ninamhitaji Dk. Kawambwa (Shukuru), ni
mchapa kazi mzuri jamani, ninawaomba mumchague kwa kura nyingi pamoja na
madiwani wa CCM,” alisema Dk. Magufuli.
Created by Gazeti la Mtanzania
Sunday, 11 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment