Mratibu wa mashirika ya umoja wa mataifana mwakilishi mkazi wa shirikala maendeleo (UNDP) Alvaro Rodriguez akimkabidhi Rais mstaafu, Benjamin Mkapa tuzo ya Umoja wa Mataifa kwa kutambua
mchango wake katika Malengo ya Milenia (MDGs). Anayeshuhudia ni Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe. Hafla hiyo ilifanyika Dar es saalam jana kitika ukumbi wa mkutano wa mwalim Julius Kambarage Nyerere
RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ametoa wito wa
kufanyika kwa mabadiliko katika mfumo wa uendeshaji wa Umoja wa Mataifa
ili kukidhi mahitaji ya sasa ya dunia.
Mkapa alisema hayo jana katika mdahalo kwenye juma la Umoja wa
Mataifa ambalo linamalizika leo, katika maadhimisho ya miaka 70 tangu
kuundwa kwa umoja huo. Mdahalo huo umefanyika katika Ukumbi wa Kimataifa
wa Mwalimu Nyerere jana.
Mkapa ambaye alichukua muda wake mwingi kuelezea na kuangalia maslahi
ya Umoja wa Mataifa kwa dunia na changamoto inazokabiliana nazo,
alisema kwa muda sasa dunia inataka mabadiliko katika uendeshaji wa
Umoja huo lakini wanaonufaika na mfumo wa sasa wamekuwa wagumu kukubali
mabadiliko.
Alisema kuna mambo sasa yanatokea yanayohatarisha usalama wa mataifa,
lakini hatua zinazopendekezwa zinashindwa kuchukuliwa kutokana na
kuendelea kuwapo kwa tabia ya vita baridi kati ya mataifa makubwa yenye
kura ya veto katika umoja huo.
Hata hivyo, Mkapa alisema kwamba masuala ya usalama wa dunia ni nyeti
sana kubaki katika mikono ya watu wachache na kutaka uwezo huo kupewa
dunia kwa kuiwekeza katika sheria ya kimataifa inayotaka uwajibikaji wa
pamoja katika masuala ya usalama.
Aidha alipongeza umoja huo katika miaka 70 Umoja huo umefanikiwa
kutokomeza ubaguzi wa rangi barani Afrika, kukabiliana na maradhi na
kupambana kutengeneza amani na kuzuia vita duniani.
Awali akimkaribisha Rais mstaafu kuzungumza, Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe alisema wakati umefika kwa
vijana kujua mustakabali wa dunia na maendeleo yake.
Alisema vijana ambao kwa sasa ndio wengi wanapaswa kushirikishwa
katika kubuni na kutekeleza mikakati ya kimaendeleo. Naye Mratibu wa
Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Alvaro Rodriguez pamoja na
kumshukuru Rais mstaafu kwa kukubali kuzungumza na vijana katika
maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja huo amesema hoja alizotoa rais huyo wa
zamani ni za msingi na zinazostahili kuangaliwa.
Alisema amefurahishwa na jinsi kiongozi huyo wa zamani
alivyouzungumzia Umoja wa Mataifa kwa kuangalia mwanzo wake na maazimio
ya awali ya kwanini umoja huo ni muhimu hasa katika suala la amani na
usalama duniani.
Aidha alisema mabadiliko aliyokuwa akizungumzia Rais Mkapa ya Umoja
huo ambayo yanatakiwa kuzingatia usalama wa dunia yatawezekana kutokana
na jinsi nchi zinavyowajibika.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 13 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment