Mgombea urais kupitia CCM, Dk John Magufuli
MGOMBEA urais kupitia CCM, Dk John Magufuli, ameanza kupangia kazi Sh
bilioni 992 zilizotolewa na Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) la
Marekani, kwa ajili ya kusambaza umeme nchini.
Akizungumza jana katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Bagamoyo,
alikowasili kuomba kura kwa wananchi, Dk Magufuli alisema kazi ya
usambazaji umeme itakayofanyika kwa kutumia fedha hizo na nyingine za
ndani, itaharakisha malengo ya kugeuza nchi, ikiwemo wilaya hiyo kuwa ya
viwanda vikubwa, vya kati na vidogo.
Katika hatua nyingine, mgombea huyo wa CCM, aliwaambia wakazi wa
Bagamoyo kuwa miaka 10 ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, Tanzania
imepiga hatua kubwa katika miradi ya maendeleo na kujijengea heshima
kubwa katika jumuiya ya kimataifa.
Kugundulika kwa gesi
Akizungumzia ugunduzi wa gesi katika wilaya hiyo ambayo ndiyo
anayotoka Rais Kikwete, Dk Magufuli alisema fursa hiyo imemuongezea
dhamira ya kuifanya Bagamoyo kuwa eneo la viwanda vikubwa, vya kati na
vidogo ili kusukuma azma ya kuifanya Serikali ya Awamu ya Tano kuwa ya
viwanda.
“Tutatumia gesi hiyo kwa uzalishaji viwandani. Ndani ya miaka
michache ijayo, wananchi wa Bagamoyo watashuhudia uzalishaji mkubwa wa
biadhaa za viwandani, zitakazouzwa ndani na nje ya nchi,” alisema Dk
Magufuli.
Katika kile kilichodhihirisha utashi wa kisiasa kwa Dk Magufuli
kuifanya serikali yake kuwa ya viwanda, alisema mbali ya umeme wa gesi,
atatumia sehemu ya Sh bilioni 992 za MCC ili kusambaza umeme katika
maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo maeneo yote ya jimbo hilo ili kukuza
uchumi na kuvutia uwekezaji.
Shirika la MCC lilimhakikishia Rais Kikwete alipokuwa akihudhuria
vikao vya Umoja wa Mataifa nchini Marekani hivi karibuni, kuwa Tanzania
imekidhi viwango vya kupata kiasi hicho cha fedha baada ya kuridhika na
hatua za kukabiliana na rushwa, kigezo pekee kilichokuwa kimesalia kwa
Tanzania kufuzu vigezo vyote.
Pongezi kwa Kikwete
Kuhusu miaka 10 ya uongozi wa Rais Kikwete, Dk Magufuli aliwaambia
wakazi wa Mbweni katika Jimbo la Chalinze na baadaye wakazi wa Bagamoyo
Mjini, kwamba Rais Kikwete amewezesha kukua kwa maendeleo na kuipa sifa
Tanzania katika jumuiya ya kimataifa.
“Naomba niwahakikishie kwamba nitaendeleza jitihada hizi za Rais
Kikwete katika kuwaletea wananchi maendeleo kwa kasi kubwa kadri
itakavyowezekana,” alisema.
Alizungumzia pia ujenzi wa barabara za lami huku akiahidi kujenga
barabara ya Makulunge kupitia Hifadhi ya Saadan hadi Tanga, ili kufungua
njia nyingine kuu ya mawasiliano baina ya Mkoa wa Pwani na Mkoa wa
Tanga, yenye urefu wa kilometa 173.8, hatua ambayo pia itaharakisha
maendeleo ya wananchi.
Alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, endapo atachaguliwa
kuwa Rais, atashughulikia matatizo ya maji katika mji wa Bagamoyo ili
kuufanya mji huo kuendelea kuwa kitovu cha utalii na kuvutia uwekezaji
kuliko ilivyo sasa.
Kuhusu fidia kwa wakazi wa wilaya hiyo, waliochukuliwa maeneo yao ili
kupisha viwanda kupitia Ukanda Maalum wa Uwekezaji wa Viwanda (EPZ), Dk
Magufuli alisema tathimini imeshaanza ili kuhakikisha wananchi hao
wanalipwa fidia zao ili waendelee na mipango yao ya maisha.
“Haiwezekani Bagamoyo kuwe na uhaba wa maji wakati mji unazungukwa na
bahari. Nitakapoingia madarakani hilo halitakuwa tatizo tena, na kama
mnavyonifahamu mimi si mtu wa maneno ni mtu wa vitendo, suala la maji
naomba mniachie mimi,” alisema.
Kama alivyoahidi katika maeneo mengine nchini, Dk Magufuli aliahidi
Serikali yake kuanza kutoa Sh milioni 50 za mikopo kwa wanawake na
vijana kwa kila kijiji na kata kuanzia mwaka ujao, na pia kuanza kutoa
posho kwa wazee wastaafu, ambao wanakisiwa kufikia asilimia 2 ya idadi
ya watu nchini.
Aliahidi pia kupanua daraja la Wami ili kupunguza ajali katika eneo
hilo na pia kutoa majengo ya kambi ya ujenzi wa barabara ya Bagamoyo
kwenda Msata, yatumike kwa matumizi mengine baada ya mradi kumalizika.
Created by Gazeti la HabariLeo
Saturday, 10 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment