Hivi
karibuni zimeibuka taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii
zikimnukuu Waziri wa Nishati na Madini, George B. Simbachawene akisema
kuwa mitambo yote ya uzalishaji umeme nchini inamilikiwa na Kampuni
binafsi.
Tunapenda
kuutaarifu Umma kuwa taarifa hizi ni za uongo kwani Waziri Simbachawene
hajawahi kutoa tamko la kuwa mitambo ya kuzalisha Umeme yote nchini ni
ya kampuni binafsi bali alichosema ni kuwa, baadhi ya mitambo ni ya
kampuni binafsi na mingine inamilikiwa na Serikali.
Mitambo inayomilikiwa na Serikali ni:-
1. Kinyerezi I (Gesi) yenye uwezo wa MW 150 ambapo MW 35 zimewashwa leo 12 Oktoba 2015;
2. Ubungo I (Gesi) yenye uwezo wa MW 102 ambayo kwa sasa inazalisha MW 85;
3. Ubungo II (Gesi) yenye uwezo wa MW 105 ambayo kwa sasa inazalisha MW 70;
4. Tegeta (Gesi) yenye uwezo wa MW 42 ambayo kwa sasa inazalisha MW 42;
5. Nyakato (Mafuta) yenye uwezo wa MW 60 ambayo kwa sasa inazalisha MW 42;
6. Kidatu (Maji) yenye uwezo wa MW 204 ambayo kwa sasa inazalisha MW 27;
7. Kihansi (Maji) yenye uwezo wa MW 180 ambayo kwa sasa inazalisha MW 45;
8. Pangani (Maji) yenye uwezo wa MW 68 ambayo kwa sasa inazalisha MW 17;
9. Nyumba ya Mungu (Maji) yenye uwezo wa MW 8 ambayo kwa sasa inazalisha MW 5;
10. Hale (Maji) yenye uwezi wa MW 21 ambayo kwa sasa inazalisha MW 4; na
11Mtera (Maji) yenye uwezo wa MW 80 ambapo mitambo yake imezimwa (MW-0);
Kwa
hiyo, Jumla ya kiasi cha umeme kinachopatikana katika mitambo hiyo kwa
sasa ni Megawati 337 kati ya Megawati 870 zinazotakiwa kuzalishwa.
Mitambo inayomilikiwa na watu binafsi ni:-
1. IPTL (Mafuta) yenye uwezo wa MW100 ambayo kwa sasa inazalisha MW 80;
2. Aggreko (Mafuta) yenye uwezo wa MW 70 ambayo kwa sasa inazalisha MW 70;
3. SONGAS(Gesi) yenye uwezo wa MW180 ambayo kwa sasa inazalisha MW 158; na
4. Symbion (Gesi) yenye uwezo wa MW 112 ambayo kwa sasa inazalisha MW 74.
Hivyo mitambo hii ya watu binafsi inazalisha umeme wa kiasi cha Megawati 382 kati ya Megawati 462 zinazohitajika.
Ieleweke
kuwa Serikali inajitahidi kuiwasha mitambo hiyo yote inayomilikiwa na
Serikali na Binafsi ili izibe pengo la umeme wa maji ambao umepungua
kutoka MW 561 hadi MW 88. Ili nchi isiwe na mgawo wa umeme zinahitajika
MW 1332 ambapo kwa sasa kiasi cha umeme kinachopatikana ni Megawati 719.
Awali
tulikuwa na upungufu wa megawati takribani 450 lakini tumefanya juhudi
za kuwasha mitambo mbali mbali tangu wiki iliyopita na sasa upungufu
uliobaki ni kati ya MW 200 na 250.
Serikali
kupitia TANESCO inatoa rai kwa Watanzania kuendelea kuvumilia kipindi
hiki cha mpito kwani inajitahidi kwa hali na mali kuwasha mitambo
iliyobaki ya gesi ya Kinyerezi yenye uwezo wa kuzalisha umeme wa kiasi
cha megawati 150 hivyo hadi ifikapo tarehe 20 Oktoba, 2015 hali ya
upatikanaji wa umeme itaanza kutengemaa.
Asanteni na poleni kwa usumbufu unaojitokeza.
Imetolewa na;
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
OCTOBER 13, 2015
Credit; Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment