Mgombea Ubunge wa jimbo la Kigoma Mjini ambaye pia ni Kiongozi wa ACT
Wazalendo, Zitto Kabwe akitoka kukagua shule ya msingi Mgumile.
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kwa tiketi ya Chama cha ACT
Wazalendo, Zitto Kabwe, anawaomba wananchi wa jimbo hilo kupiga kura kwa
wingi ili aweze kupata nafasi ya kuimarisha uchumi wa mkoa wa Kigoma.
Zitto ambaye amekuwa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa miaka 10 mfululizo anasema ana
mipango mingi ya kuleta maendeleo lakini hawezi kuitekeleza pasipokuwa
na mamlaka. Anasema Kigoma ni mkoa wenye rasilimali nyingi ambazo
zikitumika ipasavyo zitawawezesha wananchi kuendelea kiuchumi na kijamii
kwa kuwa ina fursa ya kufanya biashara na nchi jirani za Burundi, Kongo
na Zambia.
Zitto ambaye ni kiongozi mkuu wa chama hicho, anawaomba wananchi wa
mkoa wa Kigoma na hasa jimbo la Kigoma mjini kumpa ridhaa ya kuongoza
jimbo hilo kwa kipindi kimoja tu yaani miaka mitano na atakaposhindwa
kuleta mabadiliko aliyoyaahidi ahukumiwe. Anajigamba kwamba yeye ni
mbunge mjanja, anayetazama mbali na pia mwenye mtandao mpana hivyo
wananchi wamchague kwasababu anajua kila kona ya kupita kuhakikisha
jimbo la Kigoma Mjini linakuwa kitovu cha biashara.
“Tunahitaji mazingira mazuri ya kibiashara katika mkoa wetu wa
Kigoma, umaarufu wa mkoa huu ni mkubwa kwa sababu tuko mpakani na hii
kwetu ni fursa, sasa nawaambia mmepata mbunge mjanja, anaetazama mbali,
mwenye mtandao mpana kuweza kutanua mawazo yenu,” anasema Zitto.
Anasema tatizo kubwa la mkoa wa Kigoma ni ukosefu wa viwanda ambavyo
vitawawezesha wananchi kutengeneza rasilimali walizonazo kuzifanya kuwa
bidhaa zinazouzika na pia kutengeneza ajira kwa wananchi na hasa kwa
upande wa zao la michikichi na pia uvuvi wa samaki wanaopatikana katika
ziwa Tanganyika.
Kwa upande wa zao la mchikichi, kwanza linazalisha mafuta ya mawese,
ambayo yanatumika kwa kupikia chakula na pia kupaka, zao hilo pia
linazalisha chakula cha mifugo. Anasema hata hivyo kabla ya kupatikana
viwanda ni muhimu kwanza kutatua changamoto ya umeme ili uweze
kupatikana umeme wa uhakika na wa gharama nafuu ambao utawawezesha
wananchi wa mkoa huo kufanya biashara zao kirahisi.
“Lazima mradi wa mto Malagalasi ukamilike na tayari mpaka sasa mimi
binafsi kuna jitihada ambazo naendelea nazo nasubiri tu mnipe ridhaa ya
kuwa mbunge wenu ili niwe na nguvu niweze kusaini mkataba waweze kuanza
kujenga,” anasema Zitto katika mikutano yake ya hadhara Kigoma mjini.
Zitto anasema kwa sasa anashindwa kusaini na kuanzisha mradi wowote kwa
sababu ataulizwa anataka mradi huo yeye kama nani ingawa amekwisha
kamilisha upembuzi yakinifu katika mradi huo.
Anasema mkoa wa Kigoma unahitaji wabunge wenye umoja, ujasiri, na
umahiri ili kuweza kusukuma kwa kasi miradi ya maendeleo ili kuufanya
mkoa huo ufike mbali kimaendeleo kama mkoa kuufanya kupewa hadhi ya
jiji. Zitto anasema ameweza katika jimbo alilotoka kufanikisha
upatikanaji wa bandari ya Kagunga na ujenzi wa soko la kisasa katika mji
wa Kagunga.
Zitto anasema katika malengo ambayo yanaenda kutekelezwa kwa mkoa wa
Kigoma na chama chake, na suala la umeme wa mto Malagarasi limo. “Katika
kuhakikisha wananchi wanaweza kufanya biashara yenye uhakika, ni muhimu
kuhakikisha mradi wa umeme wa mto Malagarasi unakamilika ili kuondoa
tatizo la umeme katika mkoa wa Kigoma,” Zitto anasema.
Zitto anayataja mambo mengine ambayo yeye na chama chake wamepanga
kuyafanya kwa mkoa wa Kigoma kuwa ni pamoja na kushawishi uanzishwaji wa
benki ya wananchi wa Kigoma ili kuwezesha wafanyabiashara na wananchi
kuwa na chanzo cha mikopo kupanua biashara zao na kuongeza ajira kwa
wakazi wa mkoa huo. Endapo atachaguliwa kuwa mbunge, Zitto atashawishi
uanzishwaji wa chuo kikuu cha Kigoma (The University of Kigoma) ili
kupanua elimu ya juu na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa.
Pia atahakikisha vyuo vya ufundi vinaanzishwa kila halmashauri. “Pia
tumejipanga mimi na wenzangu kuwezesha vikundi vya wananchi ikiwemo
wakulima, wafugaji, wafanyabiashara ndogondogo kuwa na hifadhi ya jamii
na hivyo kufaidika na mafao kama mikopo ya riba nafuu na bima ya afya,”
anasema Zitto. Zitto anasema kwa kutumia fedha za mfuko wa jimbo
wataweza kuwapatia wananchi fedha ambazo zitaingia katika fedha
walizojiwekea kupitia vikundi vyao ili wawe na sehemu ya kukopa kwa riba
nafuu kuendeleza biashara zao.
“Hii inawafanya wananchi wenyewe kuchangia katika maendeleo yao
wenyewe, tutakachokifanya ni kupitia vikundi vyao watajiwekea fedha na
mimi kama kikundi kimejiwekea milioni mbili, basi na mimi nawaongezea
milioni mbili, nitafanya hivyo hivyo kwa vikundi vingine,” anasema
Zitto. Akichaguliwa kuwa mbunge Zitto atachochea kuanzishwa kwa viwanda
vya sukari na saruji ili kukuza ajira kwa wingi katika mkoa huo na
kuunda umoja wa wabunge watetezi wa maendeleo ya reli ya kati
inaimarishwa.
Kuhamasisha na kusimamia uendelezaji wa bandari za Kigoma ili
kuimarisha mkoa huo kuwa kitovu cha biashara ukanda wa maziwa makuu,
kuhamasisha utalii ili kuzalisha ajira kwa wingi kwa wananchi wake,
kupambana dhidi ya rushwa na ufisadi katika halmashauri za mkoa ili
kuhakikisha huduma za jamii kama maji, afya na elimu zinaimarika.
Anasema chama hicho kinaamini katika misingi ua Ujamaa wa
Kidemokrasia ikiwa na ngao nne ambazo ni undugu ni hifadhi ya jamii ya
asili kwa waafrika kila mtanzania na mwafrika anawajibu wa kumsaidia
mwenzake anayekabiliwa na tatizo bila kutarajia malipo yoyote.
Ngao nyingine ni kusimamia maendeleo ya nchi kwa kuwa ni haki na
wajibu wa kuendesha sekta nyeti katika jamii zenye maslahi mapana ya
kiusalama na kiuchumi bila kuathiri sekta binafsi.
Anasema ACT Wazalendo ina falsafa ya Nyerere ikiwa na dhamira ya
kurudisha misingi iliyoasisi taifa kama inavyoelezwa katika Azimio la
Arusha kuwa binadamu wote ni sawa, kila mtu anastahili heshima kila mtu
anastahili uhuru kamili wa kutoa mawazo yake kwenda anakotaka na dini
aitakayo bila kuvunja sheria Mbali na Zitto, ACT Wazalendo imeweza
kusimamisha wagombea ubunge katika majimbo mbalimbali mkoani Kigoma
ikiwa ni pamoja Leopold Huhagaze (Buyungu), Edga Francis (Muhambwe),
Moses Machali (Kasulu Mjini) ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa
tiketi ya NCCR Mageuzi.
Created by Gazeti la HabariLeo
Tuesday, 13 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment