Na Fredy Azzah, Karatu
MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward
Lowassa, jana aliutikisa Mji wa Karatu wakati akifanya mikutano yake ya
kampeni iliyohudhuriwa na maelfu ya wananchi.
Lowassa ambaye anaungwa mkono na vyama vinne vya upinzani ambavyo ni
Chadema, NCCR- Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na Natonal League for
Democracy (NLD) vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akitumia
kauli mbiu yake ya ‘Mabadiliko, Lowassa’ alionekana kuamsha hamasa
kubwa ya kisiasa kwa wananchi hao huku baadhi yao wakieleza kuwa
amefanikiwa kwa kiwango kikubwa kufunika nyayo za Dk. Willbrod Slaa,
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema na mbunge wa Karatu kwa kipindi cha
miaka 15.
Kabla ya Lowassa kuanza kutoa hotuba katika Uwanja wa Mbowe,
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alitumia muda mrefu
kuzungumzia safari ya kisiasa na Dk. Slaa ndani ya chama hicho huku
akianika sababu za kuondoka kwake kuwa ni shinikizo kutoka kwa mke wake.
Mbowe ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, aliyasema hayo jana
katika Uwanja huo wenye jina lake la Mbowe ulio Kata ya Karatu wilayani
humo.
Alisema jana ilikuwa siku yake ya kwanza kuhutubia Karatu baada ya
miaka 20 bila kuwa na Dk. Slaa aliyemwita rafiki na msiri wake.
“Sio jambo la kujivunia kupoteza askari mmoja ukiwa vitani, lakini
hatuwezi kurudi nyuma, tunachopigania ni zaidi ya Dk. Slaa, Mbowe na
Lowassa. Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Dk. Slaa alikuwa CCM,
alikuwa mwana CCM mpaka mwezi mmoja na nusu kabla ya uchaguzi akaja
Chadema tukiamini kuwa ni mtu mwema na mkweli.
“Alikuwa mwema na kweli tukaendelea na safari pamoja, mwanzo sikuomba
kuwa mwenyekiti wa Chadema lakini niliombwa na wazee nikakataa
wakanilazimisha nikawaambia nitakubali uenyekiti kama chama kitaruhusu
Dk. Slaa awe Katibu Mkuu,” alisema Mbowe.
Alisema baada ya sharti hilo na Dk. Slaa akawa Katibu Mkuu wa chama na wakaanza kile alichokiita safari ya kujenga chama.
Alisema baada ya kumaliza miaka mitano akaombwa tena kuongoza chama
kabla ya mwaka 2000 kusimamisha mgombea urais kwa mara ya kwanza.
“Nasema haya ili kila mmoja akiondoka hapa aondoke akijua historia,
mwaka 2000 nikaombwa tena kugombea nikatoa tena sharti la kuwa na Dk.
Slaa kuwa Katibu Mkuu, ilipofika 2010 nikapendekeza agombee urais,
akaniambia sihitaji madaraka nikamwambia nenda Watanzania watakusaidia.
“Dk. Slaa akawa mgombea, nafasi ya urais unapewa na wenzio baada ya
kuwekwa kwenye kipimo. Mwaka huo huo katika mazingira anayoyajua Mungu,
ndugu yangu, rafiki yangu kwa mapenzi yake alianza mahusiano yake ya
kifamilia, akawa sio yule anayemjua Mbowe, ilivyofika 2014 akasema
mwenyekiti naomba safari hii uwe mgombea.
“Nikasema hapana, Dk. Slaa bado una nafasi, kwa hiyo tumekaa vikao
vya chama nikapeleka pendekezo kwamba mgombea awe yeye, Kamati Kuu ya
chama wakaniambia mwenyekiti kwanini unaleta pendekezo, nikasema ndani
ya Chadema hatuwezi kugombania uongozi kwa sababu wapo waliokufa na
walioachika kwa sababu ya chama, kuna gharama kubwa tumetumia kujenga
chama hiki na hiyo siyo ya Mbowe ni ya Watanzania wote.
“Nitakuwa mtu wa mwisho kuona chama hiki kinapasuka kwa sababu ya mtu
yeyote, nikaiambia Kamati Kuu ni lazima tunavyotoka na jina la mgombea
tuwe salama, tukitoka na jina tusiwe na aibu ya kulitekeleza,” alisema
Mbowe.
Alisema Chadema kinajengwa kisayansi na si kwa ushabiki hivyo
kiliamua kufanya utafiti kwa gharama kubwa kwa kuzitumia kampuni kutoka
Marekani na Afrika Kusini pamoja na mshauri kutoka Uingereza ambao
hawakuwa wakimjue yeye Mbowe, Dk. Slaa wala Lowassa.
Alisema walichotakiwa kufanya watafiti hao ni pamoja na kuangalia
uwezo wa Chadema kushika uongozi wa Serikali katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015 ikiwa na Dk. Slaa, kujua mambo ya msingi ambayo Watanzania
wanafikiri ni kipaumbele kwa Serikali ijayo na tatu ni mgombea gani wa
CCM atakayeisumbua Chadema kwenye kuleta mabadiliko.
Mbowe alisema jambo jingine walilopaswa kufanya wachunguzi hao ni
kuangalia kinachopaswa kufanyika ili kufanikisha kwa usalama uchaguzi
mkuu.
“Majibu hayakuwa mazuri na Dk. Slaa anajua, wakatuambia Chadema mna
nguvu lakini hamuwezi kuwa na nguvu mkiacha CCM salama, wakasema tufanye
juu chini, tukeshe tukiomba CCM isiingie uchaguzi mkuu ikiwa imara.
Pasueni CCM, katika utafiti ule, hata Lowassa sijamwambia, katika
utafiti ule tuliambiwa atakayetusumbua akiwa CCM ni mtu mmoja tu, ni
Lowassa, wakatuambia mkiwa na mgombea wenu, Dk. Slaa na Lowassa akawa
CCM ana watu CCM na ndani ya Chadema watamuunga mkono. Siku hiyo tulikaa
na Dk. Slaa tukiangaliana kwa dakika 10 hakuna wa kuongea,” alisema
Mbowe.
Alisema baadaye Dk. Slaa alimfuata na kumwambia iwapo Lowassa
atakatwa na CCM wamchukue ama la na yeye alimjibu kwa kumuuliza ikiwa
hivyo anataka nafasi gani na kwamba alichagua kuendelea na nafasi yake
ya Katibu Mkuu hivyo alimwachia mengine akaendelea nayo, lakini
aliporudi nyumbani balaa likaanzia hapo.
“Dk. Slaa akiona wakati wowote bado kuna nafasi na akijisikia kuja
tumpokee, kama ataona watu wote ambao ni kinywa cha Mungu ila yeye na
mkewe ndio wako sawa tumsamehe tuende mbele, tuliamua tumkamate Lowassa
na tayari ameisaidia Chadema.
“Kwa sababu ya Lowassa sasa hivi tunaye Waziri Mkuu wa zamani,
Frederick Sumaye na Mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru. Naomba
hoja ya Dk. Slaa tuiweke pembeni kwa kuwa mabadiliko ya nchi yetu ni
muhimu kuliko Slaa na Mbowe,” alisema.
Kwa upande wake, Mzee Kingunge alisema ingawa alisomeshwa na Tanu na
kuitumikia lakini ameamua kuhama CCM iliyozaliwa na Tanu kwa sababu
imebinafsishwa.
“Siwezi kuendelea kuwa huko kwa sababu siwezi kukubali watu ambao
hawaheshimu katiba yao wenyewe na wana CCM ambao ni wanachama wa dhati,
wajifikirie wenyewe mmoja mmoja na kuamua,” alisema Kingunge.
Naye Lowassa aliposimama kuzungumza na wananchi wa Karatu, alisema
umati wa watu uliojitokeza kumsikiliza unashabihiana na uliokuwa Arusha
juzi na aliwaomba wananchi hao kumpa kura ili aweze kushinda na hatimaye
abadilishe maisha yao kwa kuanza na elimu anayoamini ni msingi wa kila
kitu.
Wakati huo huo mwandishi, Safina Sarwatt anaripoti kutoka Moshi kuwa,
shughuli za uzalishaji na usafiri mjini Moshi jana zilisimama kwa
muda baada ya wafuasi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kujitokeza kwa maelfu barabarani wakishangilia ujio wa mgombea
urais kupitia chama hicho, Edward Lowassa.
Wananchi hao walianza kujitokeza barabarani saa 1:30 asubuhi wakiwa
na mabango na bendera ya vyama vinavyoundwa na Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), wakizunguka katika mitaa mbalimbali ya mji wa Moshi na
kusababisha shughuli za uzalishaji uchumi kusimama.
Created by gazeti la Mtanzania
Sunday, 11 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment