Tuesday, 13 October 2015

Tagged Under:

Uzee ni baraka, uthaminiwe

By: Unknown On: 23:49
  • Share The Gag
  • Mtaalam wa tiba anayeshughulikia wazee katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Dk Alex Ngimba, akimsikiliza mteja wake, Hatakiwi Ally alipofika katika chumba maalumu kwa ajili ya tiba kwa waz

    OKTOBA mosi kila mwaka ni Siku ya Wazee Duniani.
    Siku hiyo ni maalumu kuihamasisha jamii kutambua haki, mahitaji na changamoto zinazowakabili wazee na kutafuta namna ya kukabiliana nazo. Dhana ya uzee inaelezea hatua ya mwisho ya makuzi ya binadamu kuanzia utoto, ujana hadi kufikia umri wa uzee unaoanzia miaka 60. Uamuzi wa Umoja wa Mataifa (UN) kuwa na siku ya wazee duniani unatokana na sababu nyingi ikiwemo ya kutoa nafasi kwa mataifa yote duniani kutafakari hali ya maisha ya wazee na kuangalia mapungufu yaliyopo.
    Inahitajika mipango kushughulikia kundi hilo ili kuboresha maisha yao na kuwawezesha wazee waishi kwa heshima kwa kuwapatia mahitaji yao muhimu. Tanzania imeungana na nchi nyingine kuadhimisha siku hiyo na kila mwaka unatolewa ujumbe maalumu kulingana na mahitaji ndani na nje ya nchi. Katika maadhimisho ya mwaka huu nchini, kaulimbiu ni “Mipango ya Maendeleo iweke Mazingira Shirikishi kwa Wazee”.
    Kauli mbiu hiyo inazingatia maisha sanjari na kutambua kwamba wazee wana uwezo na vipaji hivyo wanahitaji kushirikishwa kwa manufaa ya jamii. Uzee unaonesha thamani ya maisha marefu waliyopewa zawadi na Mwenyezi Mungu, ni umri uliopitia mengi, una uzoefu mkubwa, na upeo mpana hivyo kundi hilo ni hazina kubwa kwa taifa. Wazee ni rasilimali na hazina kubwa ya ufahamu, busara, ushauri, maarifa na uzoefu wa vitu muhimu kwa maendeleo ya taifa hili.
    Mkurugenzi wa Shirika la Wazee mkoa wa Morogoro, Samson Msemembo, anasema, wazee ni dawa, na ni watu muhimu katika jamii yetu. Msemembo anayasema wakati wa mkutano wa nusu mwaka kati ya shirika hilo na wafuatiliaji wa masuala ya wazee uliofanyika hivi karibuni mjini Kilosa mkoani Morogoro. Anasema wazee wanastahili kuenziwa katika ngazi zote na watumike kwa kadri itavyowezekana kwa mustakabali wa taifa letu katika kusimamia misingi ya maadili mema na kudumisha amani.
    Msemembo anasema, kwa kutambua umuhimu wa wazee, Serikali ya Tanzania imetunga Sera ya Taifa ya Wazee kwa lengo la kutatua kero zinazowakabili wazee. Msemembo anasema, ingawa sera hiyo imetungwa tangu mwaka 2003, haitekelezwi kwa sababu hakuna sheria inayosimamia utekelezaji huo. Anasema licha ya kukosekana kwa sheria, Serikali imeweka mikakati na kutoa matamko yanayohusu wazee na kwamba hiyo inaonesha kuwa inatambua umuhimu wa kundi hilo.
    Mikakati na matamko hayo vimewazesha wazee kupata tiba bure, kuwekwa kwa madirisha maalumu kwa wazee katika hospitali na vituo vya afya vya umma kote nchini na kuwepo kwa madaktari wa magonjwa ya uzee. Mkutano wa Kilosa umetathimini utekelezaji wa matamko hayo, ufanisi wa huduma ya afya kwa wazee, uwepo wa dirisha la wazee na chumba cha kuchunguzia afya zao.
    “Tumeangalia utekelezaji wa matamko na mikakati iliyotolewa na serikali, wilaya ya Kilosa imeonesha ufanisi mkubwa kwa kukamilisha mambo haya, isipokuwa tumeona bado changamoto kubwa ni upatikanaji wa dawa,” anasema Msemembo. Anasema, changamoto kubwa hivi sasa ni kwa mabaraza ya wazee kumaliza tatizo la wazee kukosa dawa katika vituo vya afya, zahanati na hospitali licha ya dawa hizo kuwepo za kutosha kwenye maeneo hayo.
    Msemembo anasema, wazee wanahitaji vitambulisho kwa ajili ya kupata huduma ya matibabu bure kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF). Anasema, wazee pia wanahitaji elimu wajikinge na hatari ya maambukizi ya Ukimwi kwa kuwa wanashiriki kuwahudumia watoto na wajukuu wenye virusi vinavyosababisha Ukimwi (VVU). Msemembo anasema, wazee wanahitaji kushirikishwa katika uamuzi, wawe na mabaraza yao kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa hadi taifa sanjari na kujengewa uwezo wa kipato kupitia halmashauri wanakoishi kwa kuwaanzishia miradi ya kiuchumi.
    Anasema suala la pensheni kwa wazee liendelee kupata msukumo kwa kuzingatia tangazo la Serikali la kuwapatia pensheni wazee wenye umri wa kuanzia miaka 70 na kwamba kumbukumbu zao ziandaliwe kuanzia sasa. “Pensheni kwa wazee wote iandaliwe sasa ili kupata takwimu sahihi za kuwezesha zoezi hili kuingia kwenye utekelezaji wake ili kuondoa vikwazo,” anasema Msemembo.
    Anasema, utekelezaji wa mambo utapata msukumo zaidi baaada ya kutungwa sheria itakayosimamia kuboresha maisha ya wazee na kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa huduma za jamii kwa kundi hilo na zitambuliwe kisheria. Kwa mujibu wa Msemembo, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imekubaliana na taasisi isiyo ya kiserikali ya Health Promotion and System Strengthening (HPSS) kushirikiana uboreshaji wa mfuko wa CHF ili kuongeza idadi ya wanachama.
    Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Dk Dennis Ngaromba, anasema, kuna maboresho katika uundwaji bodi ya CHF itakayowajumuisha Mganga Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Mkuu wa Wilaya. Katika maboresho hayo, meneja wa mfuko na mhasibu watateuliwa kwa ajili ya kazi za kila siku ili kuongeza idadi ya wanachama watakaonufaika na huduma za afya. Dk Ngaromba anasema, lengo la uanzishwaji wa CHF ni kutoa huduma za tiba kwa jamii iliyopo katika sekta isiyo rasmi mijini na vijijini.
    Anasema, ili kuhakikisha kuwepo kwa fedha za kutosha za kuwezesha utoaji wa huduma bora za afya, jukumu kubwa ni kuboresha usimamizi wa huduma hiyo kwa jamii ifanye uamuzi wa kuchangia katika masuala ya ustawi wa afya zao. “Kupitia ushirikiano huo, CHF inaanzisha vituo vya Tehama ngazi ya tarafa kwa maofisa tarafa, maendeleo ya jamii na wa afya pamoja na kutoa motisha kwa kila kijiji kitakachowezesha kuingiza wanachama wengi zaidi” anasema Dk Ngaromba.
    Anasema mpango huo unawawezesha wanachama wa CHF kupata matibabu kila zahanati, kituo cha afya na hospitali zilizopo ndani ya wilaya ya Kilosa baada ya taarifa zake kuingizwa kwenye mfumo ya simu za kiganjani. “Mpango huo utatoa faida kwa kuwawezesha wanachama wa CHF wakiwemo wazee kupata matibabu ndani ya zahanati, vituo vya afya na hospitali zilizomo ndani ya wilaya na nje ya mkoa ambazo zimeunganishwa na taasisi hii ya Singida, Dodoma na Morogoro kwa mtandao Tehama kupitia taasisi ya HPSS,” anasema Dk Ngaromba.
    Anasema, kuanzia sasa wilaya inapoagiza dawa, kati ya mahitaji asilimia 30 zitakuwa ni za magonjwa yasiyoambukizwa kwa ajili ya wazee wanaosumbuliwa na maradhi ya mifupa, kisukari, shinikizo la damu na matatizo katika njia ya mkojo. Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wilaya ya Kilosa, Leah Nzali, anasema wazee wengi wanakabiliwa na matatizo ya lishe kwa kuwa hawali vizuri hivyo wanakabiliwa na matatizo ya magonjwa.
    “Suala la lishe kwa wazee liwekewe mkazo, liwekewe ajenda ya kutoa uhamasishaji kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa kwa sababu lishe bora ndiyo inayowezesha wazee kupata nguvu,“ anasema Nzali. Ofisa Ustawi wa Jamii wa wilaya ya Kilosa, Said Katalamu, anasema idara ya ustawi wa jamii kwa kushirikiana na idara ya afya imetenga dirisha maalumu la wazee pamoja na daktari katika hospitali ya wilaya ya Kilosa.
    Anasema idara hiyo kwa kushirikiana na watendaji wa serikali za kata na vijiji hadi sasa imefanikiwa kuwatambua wazee 22,447, kati ya hao 11,268 ni wanaume na wanawake 11,179 na zoezi hilo ni endelevu .Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, John Henjewele, anasema kuna umuhimu wa ushiriki wa wazee katika vikundi vya vikoba vitakavyowakomboa kwa kuwanufaisha na mikopo watakayoitumia kuzalisha mali.
    Anasema kundi la wazee lina mahitaji maalumu hivyo wakiwa vikoba na kuingizwa katika mfumo wa matibabu bure kupitia CHF itawasaidia kupata huduma bora na vipato vya kuendesha maisha yao. Henjewele anasema, serikali imetunga sera zikiwemo za kuyatambua makundi ya watoto yatima na wazee na kwamba, wazee wenye umri wa kuanzia miaka 70 wameandaliwa utaratibu wa kulipwa pensheni.
    Katalamu anasema Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, kupitia idara ya ustawi wa jamii na idara ya afya ametengeneza vitambulisho 10,150 kwa wazee vikiwemo 6,293 vya wanaume na 4,837 vya wanawake. Anasema halmashauri hiyo kupitia idara zake kwa kushirikiana na watendaji wa serikali za vijiji na kata pia zimefanikisha kuundwa mabaraza ya wazee katika kata wilayani humo.
    Katika wilaya hiyo idadi ya kaya zilizojiunga CHF hadi kufikia Desemba 2014 ni 3,286 ambayo ni sawa na asilimia saba kati ya kaya 48,135 zilizolengwa kulingana na takwimu za mwaka 2012.
    Katalamu anasema, kaya 44,766 sawa na asilimia 93 bado hazijajiunga katika mfuko huo wa CHF na juhudi zinaendelea kutoa elimu ya faida ya mfuko huo katika jamii. Anataja baadhi ya changamoto zinazoukabili mfuko wa CHF kuwa ni upungufu wa dawa na vifaa tiba muhimu kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za afya , upotevu wa kadi za kuwapatia huduma kwa wazee na kukosekana kwa wodi maalumu kwa ajili ya kulaza wazee.

    Cretated by Gazeti la HabariLeo


    0 comments:

    Post a Comment