Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ametaka umma wa
Watanzania kutambua aina ya rais anayetakiwa kwa kusema, hachaguliwi
rais wa klabu ya mpira, bendi ya muziki au chama cha ushirika, bali
wanatakiwa kuchagua amiri jeshi mkuu aliye mwadilifu.
Mkapa, ambaye alimtaja Dk John Magufuli kuwa ndiye rais anayestahili
kuwa amiri jeshi mkuu kutokana na uadilifu wake, alisema hayo jana
kwenye mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika kwenye viwanja vya Boma
mjini Masasi.
Alifafanua kwamba, kati ya wagombea wote 38 wa CCM hicho ambao
walifanikiwa kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa kugombea urais, Magufuli
ndiye alikidhi vigezo vilivyowekwa.
“Ndugu zangu wana Masasi… kwa kuwa hatuchagui rais wa klabu ya mpira,
hatuchagui rais wa chama cha ushirika na hatuchagui rais wa bendi ya
muziki, bali tunachagua rais ambaye atakuwa amiri jeshi mkuu wa majeshi,
muadilifu na huyo ni Dk John Magufuli,”alisema na kuongeza: “Naomba
sana msiniangushe… kumbukeni nchi yetu iko kwenye kipindi kigumu cha
uchaguzi hivyo nawaomba msifanye makosa.”
Alisema Magufuli ambaye ni mgombea urais wa CCM, ni kiongozi anayejua
shida za Watanzania, mchapakazi, mfuatiliaji na mwenye uchungu na
watanzania. Rais huyo mstaafu alieleza namna mchakato wa kumpata mgombea
wa CCM ulivyofanyika na kusema, ulikuwa halali na ulihusisha viongozi
wa baraza la wazee la chama hicho kinyume na inavyoelezwa na baadhi ya
wanachama waliokihama.
Alisema watanzania wasidanganywe na viongozi waliohama CCM kwa madai
kuwa hawakutendewa haki. Alisema CCM kinafuata kanuni zilizowekwa zenye
lengo la kuwapata wagombea wake wa nafasi mbalimbali ikiwemo nafasi ya
urais.
Alisema hata wakati wa mchakato wa kumpata yeye kuwa mgombea wa urais
mwaka 1995 hakuwa peke yake lakini wagombea wenzake wa nafasi hiyo
waliposhindwa hawakuhama.
Created by Gazeti la habariLeo.
Tuesday, 13 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment