Mufti wa Tanzania, Shekhe Abubakar Zuberi Ally.
SERIKALI imepokea majina matatu ya mahujaji wengine wa Tanzania,
waliokufa kutokana na tukio la kukanyagana lililotokea eneo la Mina,
katika mji Mtakatifu wa Makka, Saudia Arabia Septemba 24, mwaka huu,
hivyo kufanya idadi ya mahujaji wa Tanzania waliopoteza maisha nchini
humo kufikia 11.
Hayo yalithibitishwa jana na Serikali kupitia taarifa ya Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa iliyotolewa kwa vyombo vya
habari. Taarifa hiyo iliwataja watatu zaidi waliokufa kuwa ni Yusuf
Ismail Yusuf kutoka kikundi cha Khidmat Islamiya, Rahma Salim Suweid
kutoka kikundi cha Ahlu Daawa na Issa Amir Faki.
Ilisema mahujaji hao walitambuliwa baada ya kupitia taarifa zao za
vidole zilizotolewa na Serikali ya Saudi Arabia. Serikali ilisema vifo
hivyo vinaendelea kuwa pigo kwa taifa na kwamba, vimepokelewa kwa
masikitiko makubwa.
“Aidha, Ubalozi unaendelea kushughulikia taratibu za maziko kwa
mahujaji ambao wamefariki dunia na miili yao kutambuliwa. Tunapenda
kufafanua kuwa mali za marehemu ikiwemo mizigo waliyokuwa nayo wakati wa
Hijah zitawasilishwa nyumbani Tanzania na vikundi walivyokuja navyo na
kukabidhiwa kwa jamaa wa marehemu,” ilieleza wizara.
Pia ilieleza kuwa Ubalozi unaendelea kufuatilia orodha mpya ya
taarifa za vidole, iliyotolewa na Serikali ya Saudi Arabia kwa ajili ya
kuwabaini mahujaji wa Tanzania ambao hawajatambuliwa. Mpaka sasa zaidi
ya mahujaji 30 wa Tanzania hawajulikani walipo.
Created by Gazeti la HabariLeo
Thursday, 8 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment