Na Mwandishi Wetu, Kidatu
SIKU moja baada ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kusimamisha
uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Mtera, kituo cha kuzalisha umeme cha
Kidatu kilichopo mkoani Morogoro kinategemewa kuzimwa wakati wowote
baada ya kupungua kwa kina cha maji.
Bwawa la Kidatu linazalisha megawati 204 lakini hivi sasa baada ya kina cha maji kupungua linazalisha megawati 27.
Taarifa ya kuzimwa kwa mitambo ya kuzalisha umeme ya Kidatu ilitolewa
jana na Meneja wa kituo hicho, Mhandisi Justus Mtolera, katika mkutano
wake na waandishi wa habari waliotembelea eneo hilo.
“Bwawa la Kidatu tunazalisha megawati zaidi ya 200 lakini kwa sasa
tunazalisha megawati 27 tu kwa kuwa bwawa la Mtera limekauka. Kujaa kwa
bwawa la Mtera husababisha kujaa maji katika bwawa la Kidatu hivyo
tunalazimika kusubiri mvua ienyeshe ndipo tuwashe.
“Hivi sasa tumelazimika kuwasha mashine moja kati ya nne. Kima cha
juu cha ujazo wa bwawa hili ni lita za ujazo milioni 450 kutoka usawa wa
bahari na ili mashine zote zenye uwezo wa kuzalisha megawati 50 zifanye
kazi, zinahitaji kufikia ujazo huo lakini hadi kufikia jana kulikuwa na
ujazo wa lita milioni 441.88,” alisema Mtolera.
Alisema kiwango cha maji kilichopo kina uwezo wa kuwasha mashine zote
nne kwa siku nne tu, hivyo wamelazimika kuzima mashine tatu ili
kubakisha moja inayozalisha megawati 27 na endapo maji yatapungua zaidi
nayo itazimwa.
Mtorela alisema bwawa la Kidatu pia linapata maji kutoka mto Iyovu na
Likosi ambayo pia yameanza kukauka na kuathiri uzalishaji umeme katika
bwana hilo.
“Watanzania wanapaswa kuamini kuwa uhaba wa maji ndio unasababisha
kuwepo kwa hali hii hivyo ni muhimu pia kwa watu wengine kufika katika
eneo hili kujionea wenyewe hali halisi,” alisema Mhandisi Mtolera.
Juzi Tanesco ililazimika kusitisha uzalishaji wa umeme katika Bwawa
la Mtera baada ya mitambo yake kuzimwa kutokana na kupungua kwa kina cha
maji katika bwawa hilo linalozalisha megawati 80 ambacho ndicho kiwango
cha juu kabisa kuzalishwa na bwawa moja hapa nchini.
Created by Gazeti la Mtanzania
Sunday, 11 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment