Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewabeza wanaosema umaskini wa Watanzania unaweza kuondolewa ndani ya siku 100.
Akizungumza
na wakazi wa Usevya na vijiji vya jirani kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika Kata ya Usevya, Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, Pinda alisema
umaskini wa Watanzania si wa siku moja.
“Ninashangaa
kusikia watu wakijitapa kuwa eti wataendesha nchi kwa kasi ya ajabu na
kwamba, ndani ya siku 100 watamaliza shida zote na kuondoa umaskini
miongoni mwa Watanzania.
“Kazi
ya kuongoza nchi inataka umakini, uzoefu na watu waliobobea kwenye
uongozi. Hii si kazi ya majaribio hata kidogo. Eleweni kuwa changamoto
ni sehemu ya maendeleo,” alisema.
Mgombea
urais kupitia Chadema, Edward Lowassa, amekuwa akisema anachukia
umaskini na ataweza kuuondoa katika kipindi kifupi akiingia Ikulu.
Akimzungumzia mgombea urais wa CCM, Pinda alisema: “Tuaminini CCM na tupeni nafasi tufanye kazi kwa kumpa kura zote Dk Magufuli, mbunge wa CCM na madiwani wa CCM.”
Alimpamba
Dk Magufuli kuwa ni mchapakazi anayeweza kukabiliana na kero mbalimbali
za Watanzania na hakuna mwenye shaka na utendaji wake.
Kwa upande mwingine, Pinda amewaonya wanaobeza juhudi za kuleta maendeleo zilizofanywa na Serikali tangu wakati wa Uhuru.
Alisema
wapo wanaofananisha maendeleo ya Rwanda na Tanzania wakati ukubwa wa
nchi hiyo ni kilometa za mraba 27,000 wakati Tanzania ni 945,000 ambayo
ni kubwa mara 35 zaidi ya Rwanda. “Ukubwa wa Rwanda ni sawa na wilaya
moja tu ya Mlele ambayo ina zaidi ya kilometa 29,000.
Tuna
wilaya ngapi kubwa kuliko Rwanda?” Alihoji na kuongeza: “Acheni tabia
ya kulinganisha vi-nchi vidogo na Tanzania. Kazi ya kuleta maendeleo
siyo ndogo.”
Credit; Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment