*Sasa waongoza kumshambulia
*Wasema hana uwezo wa kuongoza nchi
*Watoa msimamo kuwa chaguo sahihi ni Magufuli
Mwandishi Wetu
MASWAHIBA wa karibu wa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na
anayewakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
Edward Lowassa wamemtosa rasmi tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu
unaotarajia kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ni kwamba siku
za kufanyika uchaguzi mkuu zimebaki 16, ambapo Watanzania watakuwa na
jukumu la kufanya uamuzi wa kuwachagua madiwani, wabunge na rais.
Kabla ya kuanza kwa kampeni Lowassa akiwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), alikuwa na maswahiba wake wa karibu wakati akiendelea na harakati
za kuwania urais ndani ya chama hicho kabla ya jina lake kukatwa na
kisha kuamua kutimkia Chadema na hatimaye kupata nafasi ya kugombea
urais kupitia chama hicho.
Baadhi ya maswahiba wa Lowassa ambao wamemtosa katika kipindi hiki
cha kampeni wakiwamo wale waliogoma kumfuata Chadema ni Mbunge wa Jimbo
la Mwibara mkoani Mara aliyemaliza muda wake Kangi Lugola na aliyekuwa
Mbunge Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Diana Chilolo.
Wengine ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Msukuma, Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida, mgombea ubunge Jimbo la
Ilala, Mussa Zungu, mgombea ubunge Jimbo la Nzega Mjini, Hussein Bashe
na mgombea ubunge Jimbo la Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba.
Maswahiba wengine ndani ya CCM walimtosa Lowassa kipindi hiki cha
kampeni na kubaki na msimamo wao wa kumfanyika kampeni mgombea urais wa
CCM ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sofia Simba,
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi na Adam
Kimbisa.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa tangu kuanza kwa kampeni hizo za
uchaguzi mkuu, miongoni mwa wanasiasa ambao wamekuwa wakitoa lugha za
kejeli dhidi ya Lowassa ni baadhi ya maswahiba wake ambao kwa sehemu
kubwa walikuwa wanaijua mikakati yake na harakati zake za kusaka urais
ndani ya CCM kabla ya kutimikia Ukawa.
Kwa sehemu kubwa baadhi ya maswahiba wa Lowassa wanapokuwa jukwani
wamekuwa wakizungumzia mambo mengi yanayomhusu mgombea huyo
anayewakilisha Ukawa na kuongeza wanamjua vizuri Lowassa, kwani walikuwa
naye wakati wa mchakato wa kutafuta wadhamini ndani ya CCM.
Maswahiba hao kwa nyakati tofauti tangu kuanza kwa kampeni wamekuwa
wakieleza mabaya ya Lowassa na kwa sehemu kubwa wamekuwa wakinukuliwa
kwenye vyombo vya habari na mikutano mbalimbali ya kampeni kuwa Lowassa
amekuwa akituhumiwa na upinzani wakidai hana sifa ya uadilifu na hivyo
hafai kuwa rais.
Kangi Lugola
Siku za karibuni mgombea aliyemazila muda wake Jimbo la Mwibara na sasa
anaomba tena ridhaa ya kuwatumikia wananchi kwa mara nyingine iwapo
watamchagua kwenye nafasi hiyo, Kangi Lugola alisema anamfahamu vizuri
Lowassa na anachoamini yeye ni kwamba mgombea huyo hana sifa ya kuwa
rais.
Lugola akiwa jimboni Mwibara wiki iliyopita wakati Mgombea Mwenza wa CCM
Samia Suluhu Hassan alipofika jimboni humo kumuombea kura mgombea urais
wa CCM, alitumia nafasi hiyo kuwaleza Watanzania kuhusu Lowassa ambapo
alidai kuwa mgombea huyo wa Ukawa hana uwezo wa kutia saini ya kumtoa
mwanamuziki aliyefungwa jela kifungo cha maisha Babu Seya.
Wakati wa mchakato ndani ya CCM, Lugola alisimama kwenye mkutano wa
hadhara wakati Lowassa akitangaza rasmi kugombea urais kupitia CCM kabla
ya kuondoka chama hicho na kudai kuwa mwanasiasa sahihi ndani ya CCM
anayefaa kuwatumikia Watanzania baada ya Rais Jakaya Kikwete ni Lowassa
lakini tangu alipoondoka CCM, amekuwa tofauti.
Pia, Lugola amekuwa akieleza kuwa wananchi wanaojaa kwenye mikutano ya
Lowassa wanakwenda ili siku moja wasiulizwe alipokuwa mgonjwa hawakwenda
kumtazama na alipokuwa na kiu hawakumpa maji.
Kwa sehemu kubwa Logola amekuwa akiwataka Watanzania siku ya uchaguzi
mkuu mwaka huu kumpigia kura ya urais mgombea urais wa CCM, Dk. John
Magufuli na kwamba mgombea huyo ana sifa zote za kuwa rais na kwa sehemu
kubwa utendaji wake wa kazi na usimamizi mzuri kwenye wizara mbalimbali
alizosimamia akiwa waziri na hasa Wizara ya Ujenzi imemjengea heshima
kwa wananchi.
Chilolo
Kwa upande wake, Diano Chilolo ambaye alikuwa swahiba mkubwa wa Lowassa
naye ameamua kumtosa katika kipindi hiki cha kampeni na siku za karibuni
akiwa mkoani Singida aliibuka na kudai Lowassa hafai kuwa rais kwa
madai kuwa anakashfa katika uongozi wake.
Alisema kutokana na kuwa na kashfa wakati wakiwa bungeni, Lissu ndiye
aliyekuwa akipambana naye na anashangaa kukubalika kujiunga Chadema na
kupewa nafasi ya kuwania urais.
Serukamba
Kwa upande wake, Serukamba ambaye wakati wa mchakato wa kumtafuta
mgombea urais kwa tiketi ya CCM, alikuwa ndio msemaji wa Lowassa, lakini
tangu kuanza kwa kampeni amekuwa kimya.
Surukamba ni miongoni mwa maswahiba waliobaki na msimamo wao kwa kubaki
CCM na kuendelea na kampeni zake za kuomba ridhaa ya kuomba kuwa Mbunge
wa Jimbo la Kigoma Kaskazini.
Kabla ya kugombea jimbo hilo, Surukamba ni mbunge anayemaliza muda wake
Jimbo la Kigoma Mjini ambalo sasa linagombewa na Zitto Kabwe wa
ACT-Wazalendo akichuana na mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya
CCM, Dk.Warid Kaburu.
Msukuma
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Msukuma amekuwa
akitumia mikutano mbalimbali akisema kuwa anamfahamu vizuri Lowassa na
wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea urais ndani ya CCM alikuwa naye
kwa karibu zaidi na anachoweza kueleza mgombea wa Ukawa ni mgonjwa bila
kueleza kama alimpima au laa!
Msukuma anakumbukwa na wananchi wengi kwani wakati Lowassa anatangaza
kugombea urais ndani ya CCM, alikwenda na usafiri wa helikopta jijini
Arusha. Hivyo wengi wanamkumbuka Msukuma kwa kutua uwanjani siku Lowassa
akitangaza safari yake ya matumaini ambayo yalikwama ndani ya CCM na
sasa yupo kwenye safari mpya ya mabadiliko ndani ya Ukawa.
Mwenyekiti huyo wa Geita amekuwa akieleza wazi katu hawezi kumfuata
Lowassa kwani anamfahamu na kwamba yeye ni mwanasiasa mwenye akili
timamu hivyo hawezi kuyumba kwa kumfuata mtu ambaye anajua fika hawezi
kuwa Rais wa Tanzania, kwani Watanzania wengi baada ya kutangazwa jina
la Dk. Magufuli kuwa ndio mgombea urais wa CCM wameshaamua na
wanachosubiri ni kumpigia kura awe Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Bashe
Kwa upande wake, Husein Bashe aliwahakikishia wananchi kuwa kura yake
kwa nafasi ya urais itakwenda kwa mgombea urais wa CCM ambaye ni Dk.
Magufuli kwa kuwa anamuamini ndiye mtu sahihi huku akiwajibu wale
waliokuwa wanaeneza kuwa atampigia kura mgombea wa Ukawa kuwa
wanajidanganya.
Bashe wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea urais ndani ya CCM alikuwa
swahiba mkubwa wa Lowassa na mfuasi muaminifu ambaye ameamua
kutoyumibishwa na upepo wa kisiasa na kubaki ndani ya chama chake
akiendelea kuomba kura na dalili za kushinda jimbo hilo kwa upande wake
ni kubwa.
Nchimbi
Uchunguzi wa Jambo Leo, tangu kuanza kwa kampeni umekuwa pia ukifuatilia
kwa karibu kauli za Dk. Nchimbi ambaye naye alikuwa rafiki mkubwa wa
Lowassa na ndio alitoa msimamo wa maswahiba wa Lowassa kuwa
hawakuridhika na mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM.
Lakini baada ya kupatikana kwa Dk. Magufuli naye aliamua kujisalimisha
ndani ya CCM na sasa ni miongoni mwa makada wanaotoa msimamo wao
hadharani na siku za karibuni amenukuliwa akieleza kuwa kwenda Ukawa kwa
ajili ya kumfuata Lowassa kwake ni jambo ambalo haliwezekani.
Dk. Nchimbi alisema yeye ni mwana CCM makini hawezi kuondoka chama hicho
na kuhoji akiondoka CCM aende wapi na kwenda Chadema au Ukawa itakuwa
ni rekodi ya dunia kwa kutoka chama makini na kwenda chama kinachoelekea
kufa.
Simba
Wakati kwa Waziri Simba naye amenukuliwa mara kadhaa akisema chaguo
sahihi la CCM kugombea urais ni Dk. Magufuli na kwamba Lowassa hana
nafasi ya kushinda kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.
Pia, Waziri Simba kwa nyakati tofauti amenukuliwa akieleza kuwa katu
hataondoka CCM na kwenda kwa Lowassa na kuongeza majukumu aliyonayo kwa
sasa ni kuendelea na kampeni za kumfanikisha ushindi wa kishindo wa
mgombea urais wa CCM.
Madabida
Kwa upande wake, Ramadhan Madabiba yeye amekuwa akiendelea na kampeni za
kumnadi, Dk. Magufuli na ndio amepewa nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa
Wenyeviti wa CCM nchini.
Kabla ya Lowassa kuondoka Madabida alikuwa swahiba mkubwa wa Lowassa, lakini naye amebaki CCM.
Wakati Lowassa anakwenda Chadema, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman
Mbowe alisema wameamua kumchukua Lowassa kwasababu wanafahamu kuna kundi
kubwa la wanaCCM wakimo viongozi mbalimbali watakwenda kwenye chama
hicho wakiwamo wabunge zaidi ya 80 na wenyeviti wa mikoa 15, lakini hadi
sasa wenyeviti wa CCM wa mkoa waliondoka hawazidi wanne.
Lukuvi afichua siri
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema
baadhi ya mataifa ya Ulaya na Amerika yalitoa onyo iwapo CCM ingemteua
Lowassa kuwa mgombea urais wa Tanzania.
Alisema angeteuliwa basi nchi ingewekwa wenye kundi la nchi mafisadi
duniani na kudai kutokana na kuhusika na kuwekeza fedha nyingi kwenye
nchi hizo. Hata hivyo, Lukuvi haueleza kuhusu sakata la Escrow kama
halihesabiwi ni ufisadi.
Lukuvi alitoa madai hayo kwa nyakati tofauti alipokuwa anatembelea Jimbo
la Isimani na kufanya kampeni katika vijiji mbalimbali vya Kata za
Mahuninga, Tungamalenga, Idodi na Mlowa.
Credit; Mpekuzi blog
Thursday, 8 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment