Sehemu ya miundombinu ya kuchakata na kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara
na Songo Songo hadi Dar es Salaam kupitia Somanga, iliyoko katika eneo
la Madimba mkoani Mtwara.
RAIS Jakaya Kikwete jana alizindua miundombinu ya kuchakata na
kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar es Salaam
kupitia Somanga.
Alizindua mtambo huo katika hafla iliyofanyika eneo la Madimba mkoani Mtwara.
Akizungumza na wananchi wakati wa hafla hiyo, Rais Kikwete alisema
kuanza kazi kwa mitambo hiyo ni hatua muhimu kuelekea katika Taifa lenye
uchumi wa kati.
Alifafanua kwamba hatua hiyo inatokana na kuimarika kwa huduma za
nishati ya umeme pamoja na uchumi katika nyanja mbalimbali, ikiwemo
viwanda kwa kuwa gesi hiyo itamaliza tatizo la umeme.
Rais Kikwete aliwaagiza wa tendaji wa Shirika la Umeme nchini
(Tanesco) na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), kuwa makini katika
mchakato wa ununuzi mitambo ya kufua umeme, kwa kufuata sheria ili
matatizo yaliyowahi kulikumba Taifa kutokana na ukiukwaji wa taratibu
mwaka 2006 wakati wa uhaba wa umeme, yasijirudie tena.
Rais Kikwete aliishukuru Serikali ya China kwa kuwa tayari kujenga miundombinu hiyo.
Aliagiza mamlaka husika kutoa huduma muhimu za jamii, ikiwa ni pamoja
na upatikanaji wa maji safi na salama, pamoja na barabara kwa wakazi wa
Mtwara ili wanufaike na gesi hiyo.
TPDC Awali akitoa maelezo ya utangulizi, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC,
Dk James Mataragio alisema miundombinu hiyo imekamilika na tayari gesi
imeshaanza kusukumwa kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Dk Mataragio
alisema ujenzi wa miundombinu hiyo, umegharimu dola za Marekani bilioni
1.53, sawa na Sh trilioni 2.926 za Tanzania.
Alisema asilimia 95 ya fedha hizo, zimetokana na mkopo kutoka Benki
ya Exim ya China huku asilimia 5 ikitoka serikalini. Akizungumzia faida
za miundombinu hiyo, Dk Mataragio alitaja faida kadhaa za gesi hiyo,
ikiwemo itatumika kuzalisha umeme, jambo litakaloifanya Tanzania kuwa na
umeme wa uhakika.
Alitaja faida nyingine kuwa ni pamoja na kuongeza Pato la Taifa,
kutokana na uuzaji wa gesi hiyo nje ya nchi kuokoa fedha za kigeni,
ambazo hutumika kuagizia mafuta kutoka nje ya nchi. Nyingine ni kukuza
uchumi kupitia ukuaji wa sekta ya viwanda, kuongeza mapato ya
halmashauri kupitia mirabaha na kuchochea utafiti wa mafuta na gesi.
Alisema miundombinu hiyo, itakuwa na uwezo wa kusukuma gesi yenye
futi za ujazo milioni 784 kwa siku ifikapo mwaka 2020, kutoka uwezo wa
sasa wa kusukuma futi za ujazo milioni 80 pekee.
Akimkaribisha Rais Kikwete, Waziri wa Nishati na Madini, George
Simbachawene alisema kuwa huo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM, na kwamba
Serikali ina mpango wa kujenga mitambo ya umeme mkoani Mtwara,
itakayozalisha zaidi ya megawati 600 kwa ajili ya mikoa ya Kusini ya
Lindi na Mtwara.
“Mheshimiwa Rais tunakupongeza sana kwa jitihada zako, kuna watu
wanabeza na wanahoji eti utatuachaje, mimi nawaambia kwamba ulipoingia
ulitukuta na gesi ya futi za ujazo trilioni 8, lakini unatuacha na futi
za ujazo trilioni 52,” alisema. Simbachawene alisema kuwa ujenzi wa
miundombinu hiyo, utazalisha ajira zaidi ya 1,363 katika eneo hilo la
Mtwara.
created by Gazeti la HabariLeo
Sunday, 11 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment