Sehemu ya jiji la Dar es Salaam |
Gazeti hili limefanya utafiti katika taarifa rasmi zinazoonesha mabadiliko ya jamii ya Watanzania katika miaka iliyopita na ya hivi karibuni na kubaini kwamba kauli nyingi za wanasiasa kuhusu umasikini na ufukara wa Watanzania hazielezi hali halisi ya wapigakura.
Katika utafiti huo, gazeti hili limebaini kuwa madai ya wanasiasa kuhusu hali ya Watanzania ambayo yamekuwa yakipewa kipaumbele katika vyombo vya habari katika ubora wa makazi, upatikanaji wa maji, umeme na elimu yanapingana na hali halisi.
Makazi
Katika makazi ya Watanzania, utafiti huo ulijikita kupata taarifa za hali ya makazi kuanzia wakati wa Uhuru mpaka hivi sasa, baada ya baadhi ya wanasiasa kudai kuwa Watanzania wengi wanaishi katika nyumba za tembe na nyasi, huku wakiahidi kuziondoka katika kipindi kifupi kama wakipigiwa kura.
Tofauti na matarajio ya gazeti hili, takwimu nyingi za hali ya makazi ya Watanzania hazikupatikana kutoka wakati wa Uhuru, lakini kumepatikana taarifa za kutosha za hali ya makazi na mabadiliko ya hali hiyo kuanzia miaka ya mwanzo ya 1990, kabla ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mpaka sasa.
Makazi katika taarifa hizo, yamepewa tafsiri aina ya paa, kuta na sakafu ya nyumba ya Mtanzania, tofauti na namna wanasiasa wanavyozungumzia makazi hayo, kwa kujikita katika aina ya paa kwa kusema nyumba za tembe au nyasi.
Katika ubora wa paa za nyumba za Watanzania, Taarifa za Bajeti za Kaya zinazotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa, zinaonesha kuwa hali ya ubora wa paa za makazi ya Watanzania, imebadilika katika kiwango kikubwa kutoka mwaka 1991/1992 mpaka mwaka 2011, 2012.
Kwa mujibu wa taarifa hizo mwaka 1991/1992, nyumba zilizokuwa na paa la kisasa, kwa maana ya mabati, vigae na zege zilikuwa asilimia 36 ya nyumba zote za Watanzania, kwa maana ya kwamba asilimia 64 ya nyumba hizo zilikuwa za tembe na nyasi.
Kuanzia wakati huo, makazi ya Watanzania yalianza kubadilika na kuwa ya kisasa zaidi, ambapo ilipofika mwaka 2000/2001 nyumba zenye paa la kisasa ziliongezeka pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watu na nyumba na kufikia asilimia 43, (kutoka asilimia 36).
Taarifa ya bajeti ya kaya ya mwaka 2007, inaonesha kuwa ubora wa makazi ya Watanzania, uliendelea kuwa mzuri zaidi kwani pamoja na ongezeko la idadi ya watu na nyumba, lakini nyumba zenye paa la kisasa, ziliongezeka na kufikia asilimia 55 ya nyumba zote za Watanzania.
Kwa taarifa ya sasa ya Bajeti ya Kaya, tofauti na kauli zinazoendana na ahadi za wanasiasa kuwa hakuna kilichofanyika katika miaka 55 ya Uhuru, ukweli ni kwamba ubora wa paa za nyumba za Watanzania umekuwa mzuri kuliko wakati mwingine katika historia ya nchi, kwa kuwa asilimia 70 ya Watanzania nyumba zao zina paa bora zaidi.
Katika vigezo vingine vya ubora wa makazi, katika aina ya kuta mwaka 1991, nyumba zenye kuta bora zilikuwa asilimia 7.8 tu, lakini hali ikawa bora ambapo leo nyumba zenye kuta bora ni zaidi ya asilimia 48.2.
Kwenye kigezo cha sakafu bora ya nyumba, mwaka 1991 ilikuwa ni katika asilimia 20.8 tu ya nyumba za Watanzania, lakini leo nyumba zenye sakafu bora ya kisasa ni asilimia 39.4.
Huduma za maji
Katika huduma za maji kwa Watanzania ambazo zimekuwa sehemu ya mjadala katika baadhi ya vyombo vya habari, hali pia imebadilika kutoka mwaka 1991 mpaka mwaka 2012.
Taarifa zinaonesha kuwa mwaka 1991/1992 Watanzania waliokuwa wakipata maji kutoka katika vyanzo bora, walikuwa asilimia 46 tu na ilipofika mwaka 2000/2001, hali ikawa nzuri kwa zaidi ya nusu ya Watanzania, ambapo asilimia 55. 3 ya Watanzania walikuwa wakipata maji kutoka katika vyanzo bora.
Mwaka 2007, hali ilibadilika kidogo ambapo sehemu ya Watanzania waliokuwa wakipata maji kutoka katika vyanzo bora, ilikuwa asilimia 51.8 lakini juhudi zilizofanyika ilipofika mwaka 2012, asilimia 69 ya Watanzania wamekuwa wakipata maji kutoka vyanzo vilivyo bora.
Katika huduma hiyo ya maji, taarifa hizo zimefanya tathimini ya umbali kutoka katika makazi ya wananchi mpaka katika chanzo cha maji, kwa sasa asilimia 71.4 ya Watanzania wanapata maji kutoka vyanzo vilivyo katika umbali usiozidi kilometa moja.
Umeme
Katika nishati ya umeme ambayo imekuwa ikitumika kuboresha maisha ya watu, ambapo sio tu kwa ajili ya mwanga, bali pia kwa upatikanaji wa taarifa, ajira mpya na mahitaji mengine muhimu ya wananchi, hali pia imebadilika.
Taarifa hizo zinaonesha kuwa mwaka 2001, Watanzania waliokuwa wakitumia nishati hiyo walikuwa asilimia 9.8 tu, lakini hali ikawa bora zaidi baada ya juhudi za Serikali ambapo mwaka 2007, Watanzania wanaotumia umeme walifikia asilimia 12 pamoja na ongezeko la idadi ya watu.
Mwaka 2012 Watanzania waliofikiwa na kuanza kutumia huduma ya umeme, waliongezeka na kufikia asilimia 18.2 na mwaka huu idadi hiyo ikaongezeka zaidi ya mara mbili na kufikia asilimia 46.
Wakati hali ikiwa hivyo katika huduma hiyo, Serikali inayoondoka madarakani ya Awamu ya Nne chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, inaiachia Serikali ya Awamu ya Tano itakayochaguliwa Oktoba 25 mwaka huu, mradi wa awamu ya pili wa Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC), wenye Sh bilioni 992 kwa ajili ya kusambaza umeme kwa Watanzania waliosalia.
Elimu
Katika miundombinu ya elimu, taarifa za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, zimeonesha kuwa shule za msingi zimeongezeka kutoka 14,257 mwaka 2005 hadi 16,538 mwaka 2015.
Kutokana na kuboreka kwa miundombinu, wanafunzi wameongezeka kutoka 7,541,208 mwaka 2005 hadi 8,202,892 mwaka 2015 na kuwezesha asilimia 98 ya watoto wanostahili kupata elimu ya msingi, kuandikishwa.
Kwa upande wa shule za sekondari, zimeongezeka kutoka shule 1,745 mwaka 2005 hadi shule 4,753 mwaka 2015 na idadi ya wanafunzi ikaongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi wanafunzi 1,804,056 mwaka 2015. Katika kipindi hicho, vyuo vya ufundi viliongezeka kutoka 184 mwaka 2005 hadi 744 mwaka 2015 na wanafunzi katika vyuo hivyo wakaongezeka kutoka 40,059 hadi 145,511 mwaka 2015.
Idadi ya vyuo vikuu nayo imeongezeka kutoka vyuo 26 mwaka 2005 hadi 52 mwaka 2015 na idadi ya wanafunzi wa vyuo vikuu, ikaongezeka kutoka wanafunzi 40,719 mwaka 2005 hadi wanafunzi 218,959 mwaka 2014. Kati ya hao, wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu, wameongezeka kutoka wanafunzi 16,345 mwaka 2005 hadi wanafunzi 99,590 mwaka huu.
Created by Gazeti la HabariLeo
0 comments:
Post a Comment