Mwenyekiti wa TASWA Juma Pinto akimkabidhi tuzo Rais Jakaya Kikwete kwa kutambua mchango wake
katika kuendeleza michezo nchini wakati wa utawala wake kwa miaka 10.
Hafla hiyo Ilifanyika Dar es Salaam juzi.
RAIS Jakaya Kikwete ameitia moyo timu ya Taifa, Taifa Stars na
kuwataka wasikate tamaa kwani wanaweza kuifunga Algeria. Taifa Stars
inatarajia kucheza hatua ya pili dhidi ya Algeria katika mchezo wa
kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi katika mchezo utakaochezwa
Novemba 14, mwaka huu Dar es Salaam.
Akizungumza juzi kwenye sherehe za utoaji wa tuzo kwa wanamichezo
bora 10 waliofanya vizuri kwenye utawala wake, zilizoandaliwa na Chama
cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Kikwete alisema
licha ya kuwa Algeria ndio timu bora Afrika, wasikate tamaa kwani
wanaweza kuvuka.
“Mkwasa ameanza vizuri tuendelee kumpa muda, tusikate tamaa kama
wenzetu wameweza na sisi tutaweza kama sio leo itakuwa kesho,” alisema.
Alisema Algeria ndio timu pekee ya Afrika iliyojitahidi kufanya vizuri
katika michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika kule Brazil.
Kikwete alisema hata bahari kuu huvukwa, hivyo hata taifa Stars
pamoja na ubora wa timu hiyo kubwa Afrika wakijitahidi wanaweza kuivuka.
Taifa Stars ilitinga hatua ya pili baada ya kuifunga Malawi kwa jumla
ya mabao 2-1 katika hatua ya kwanza ya michuano hiyo ya kufuzu Kombe la
Dunia, ambapo katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam, Stars ilishinda 2-0
kabla ya kufungwa 1-0 katika mchezo wa marudiano.
Aidha, alikabidhi tuzo kwa wanamichezo 10 waliofanya vizuri wakati wa
utawala wake pamoja na kukabidhi tuzo kwa viongozi mbalimbali
waliofanya vizuri pamoja na wafanyabiashara na asasi zilizomuunga mkono
katika kupiga jeki maendeelo ya michezo nchini.
Wanamichezo waliopata tuzo ni wanariadha Samson Ramadhan aliyepata
Medali ya Dhahabu mwaka 2006 katika Michezo ya Jumuiya ya Madola, Martin
Sule aliyepata Medali ya Fedha katika Michezo ya Afrika mwaka 2007 na
Mary Naali aliyepata Medali ya Shaba mwaka 2008.
Kikosi cha Taifa Stars kilichocheza CHAN ya kwanza mwaka 2009
kilipata tuzo, mchezaji Nitiboli Mwanaidi Hassan, bondia Francis Cheka,
kocha Charles Boniface Mkwasa kwa kuiwezesha timu ya wanawake, Twiga
Stars kucheza fainali za Afrika na mshambuliaji Mbwana Samatta kwa
mafanikio yake TP Mazembe wote walipata tuzo.
Wengine waliopata tuzo ni mchezaji wa mpira wa kikapu nchini Marekani
Hasheem Thabit, timu ya taifa ya gofu wanawake iliyoshika nafasi ya
pili mashindano ya Afrika mwaka 2010, na Twiga Stars waliofuzu All
African Game.
Upande wa viongozi Jenerali Mstafu George Waitara kwa kujenga Uwanja
wa Gofu, Kanali Mstaafu Iddi Kipingu kwa uwekezaji wake katika michezo
ya vijana, Dioniz Malinzi kwa kujenga Uwanja wa Gofu Bukoba, Leodegar
Tenga kwa kuifanya TFF kuwa taasisi yenye kuheshimika na Mtangazaji
Abdallah Majura kwa kuweza kuanzisha kituo chake mwenyewe cha Redio
(ABM). Makampuni na wadau waliopewa tuzo ni pamoja na Bakhresa Limited
kwa mchango wao mkubwa michezoni na Majeshi..
Created by Gazeti la habariLeo
Tuesday, 13 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment