NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya New Habari (2006) Ltd inayochapisha magazeti ya MTANZANIA,
RAI, Bingwa Dimba na The African, imelaani vikali, uzushi, uongo na
upotoshaji wa hali ya juu unaofanywa na watu wasio na nia njema na
kampuni
hiyo.
Jana watu hao wasio na nia njema na kampuni hiyo, hasa magazeti ya
MTANZANIA na RAI, walitengeneza mfano wa magazeti hayo kisha kuyaweka
kwenye mitandao ya kijamii, yakiwa na taarifa mbalimbali za uongo
na uzushi.
Akizungumzia hali hiyo jijini Dar es Salaam jana, Mhariri
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom
Kibanda, alisema ameshtushwa na hatua hiyo, lakini ni vema wasomaji na
wafuatiliaji wa magazeti ya MTANZANIA na RAI, wakapuuza magazeti
yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, kwani watu wanaofanya hivyo
wamelenga kuyachafua kwa masilahi yao binafsi.
Kibanda alisema watu hao wenye nia ovu na magazeti hayo,
juzi walitengeneza mfano wa gazeti la RAI likiwa na kichwa cha
habari kisemacho “Gwajima: Nina imani na Lowassa katika kutimiza
ndoto zangu” na jana wametengeneza MTANZANIA na kulisambaza kwenye
mitandao ya kijamii likiwa na kichwa habari “Lowassa,
Kagame wahusishwa kifo cha Mch. Mtikila”.
“Tumeshtushwa na hatua hii ya kurudia uovu wao, tulipoona kwa mara ya
kwanza wametengeneza gazeti feki la RAI ambalo lina sura inayofanana na
gazeti letu halisi na kuliweka kwenye mtandao ili kuwaaminisha watu
kuwa
gazeti linaloenda sokoni ndiyo lile ambalo lilikuwa na habari ambazo ni
potofu, zenye mwelekeo wa uchochezi, tulipuuza. Hata hivyo, wahusika wa
uovu ule wa awali tuliwabaini.
“Watu hawa wamerudia tena, sasa niseme inatosha, napenda kuwaambia
wasomaji wa gazeti la MTANZANIA ambalo huchapishwa kila siku na RAI kila
Alhamisi ya wiki kuwa, gazeti lililowekwa kwenye mitandao ya
kijamii si gazeti halisi la RAI wala habari zile hazijawahi kuandikwa na RAI hata mara moja.
“Na hata ukizisoma habari zilizomo kwenye gazeti linalosambazwa mtandaoni zimetawaliwa na dhamira ya
kulipaka matope gazeti halisi la RAI, wahariri na waandishi wake kwa malengo ambayo hatujayajua.
“Katika uchunguzi wetu tuliofanya baada ya gazeti feki kuwekwa
mitandaoni kwa mara kwanza, tuliona kazi hiyo haramu inafanywa katika
chumba kimoja cha habari ambacho watendaji na wahariri wake wana
mrengo fulani wa kihabari.
Tulikaa kimya wakati ule wa kwanza kwa maana tuliamini wangejifunza kutokana na upuuzi wao.
“Lakini baada ya kuona wamerudia, tumeona kuna wajibu wa kuwajulisha
wasomaji wetu ambao baadhi wanaingia kwenye mitandao ya kijamii kabla
ya kusoma magazeti, kwamba kile ambacho wanakiona kwenye mitandao si
magazeti halisi ya MTANZANIA na RAI.
“Kutokana na hali hiyo, tunaangalia namna bora ya kuwasiliana na
mamlaka husika za kiserikali ili kupata njia sahihi ya kuwashughulikia
hawa wanaokiuka sheria ya mitandao,” alisema. Kibanda, amewataka watu
hao wenye nia ovu na Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, kuachana
na mikakati yao hiyo miovu kwani haitawasaidia kufanikisha malengo yao
dhalimu.
Created by Gazeti la Mtanzania
Thursday, 8 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment