Tuesday, 13 October 2015

Tagged Under:

Juhudi za Nyerere zilibadilisha watu kuamini mkoloni anang’oka

By: Unknown On: 23:33
  • Share The Gag

  • Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

    LEO ni miaka 16 tangu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipofariki dunia katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas nchini Uingereza alipopelekwa kwa ajili ya matibabu. Katika makala haya, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe na Mzee Sosthenes Ngize, wanaeleza wanavyomkumbuka Mwalimu Nyerere na mchango wake katika kupigania uhuru na kisha maendeleo ya nchi yetu kama walivyohojiwa na Mwandishi Wetu, ANGELA SEBASTIAN Mzee Sosthenes Ngize (80) mkazi wa Kagera ambaye ameshuhudia nchi hii inapata uhuru, anasema Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mtu aliyejali na kuheshimu utu wa mtu.
    Anamwelezea kama kiongozi mpenda maendeleo ambaye alitetea amani ya mwanadamu popote alipo akiamini kwamba yeye mwenyewe hawezi kujisikia mtu huru kama kuna watu wengine duniani hawana uhuru. Anasema Mwalimu Nyerere alipoanza mchakato wa kuzungukia nchi nzima kuhamasisha mwamko wa kudai uhuru, yeye alikuwa kijana na kwamba anachokumbuka ni kwamba Mwalimu alikumbana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na miundombinu hafifu ya usafiri iliyokuwepo.
    Hata hivyo, Mzee Ngize anasema Mwalimu hakukata tamaa, alizunguka nchi nzima akihubiria wananchi kuwa na mawazo mapya ya kufanya mabadiliko ya kuondoa woga wa kudai uhuru kutoka kwa wakoloni. Anasema kadri siku zilivyokuwa zikisonga mbele wapo waliodhani kupata uhuru ilikuwa ni ndoto, japo wengine wakiwa na mtazamo tofauti. “Baadhi ya babu zetu, bibi na hata baba zetu walikuwa katika mtanziko kwa vile walimuona mkoloni kama ndiye kila kitu na asiyewezekana kuondoka. Hii ni kutokana ya uelewa mdogo waliokuwa nao huku baadhi ya Madhehebu ya Kidini yakiwasaidia kuwakanganya wananchi ili wazidi kutawaliwa,” anasema Ngize.
    Anasema anazungumzia wakati ambao Watanzania wengi hawakuwa na uwezo wa kuwa na blangeti au mashuka ya kujifunika na kwamba wakati harakati za ukombozi wa nchi zinaanza wapo Watanganyika waliojifunika magome ya miti (embugu kwa Kihaya). Kwa mantiki hiyo sindano maalumu za kushonea magome zilikuwa ni zana muhimu sana kwa wananchi, vitu ambavyo walijua vinatoka kwa Wazungu (wakoloni).
    Anazidi kufafanua kwamba hizo ni zama ambazo watu wengi walikuwa wanasumbuliwa na funza kiasi kwamba kitu kama pini kilikuwa zana muhimu na hoja kuizungumzia kwa vile ilisaidia sana kutolea funza kwenye miguu. Kwa mantiki hiyo anasema wazee, hususan wa mkoani Kagera wapo waliohoji: “Hivi tukipata uhuru zana hizi (pini ya kitolea funza au sindano ya kuunganishia magome ya miti) tutavipata wapi tena?”
    Mzee Ngize anasema wazee wengi waliamini labda wakoloni wakiondoka hakutakuwa na uwezo wa kupata vifaa hivyo tena na wakiamini kwamba si rahisi jamii kuondokana na vitu kama funza. Anasema kuna waliokuwa na hofu kuwa kudai uhuru ni kumchezea mkoloni ambaye angekasirika na nchi kuingia vitani kama ilivyokuwa imewahi kutokea huko nyuma. Wengi walikuwa wanakumbuka vita ya kwanza na vita ya pili maarufu vita kuu ya dunia sambamba na vita ya majimaji.
    Anasema katika mazingira kama hayo ilikuwa ngumu kumshawishi mwananchi wa kawaida kuunga mkono harakati za ukombozi na kumwaminisha kwamba mkoloni anaweza kung’oka. Anasema hatimaye mwaka 1961 Tanganyika ikaibuka kidedea, nchi ikapata Uhuru bila kumwaga damu kwa juhudi za Mwalimu Nyerere. Mzee Ngize anasema nchi ilipopata uhuru yeye alikuwa na umri wa miaka 26.
    Ngize Pia anasema Mwalimu aliona mbali kuhusiana na masuala ya elimu, maana kabla ya uhuru na baada ya uhuru, shule nyingi zilikuwa ni za wamisionari na chache ndio zilikuwa za Serikali. Anasema kwa pale Bukoba, kwa mfano, Waislamu hawakuwa na shule, jambo ambalo Mwalimu aliona linaweza kuleta bughudha huko mbeleni, kwa vile wenye kusomea kwenye shule za wamisionari ndiyo wangenufaika na matunda ya Uhuru.
    Anasema ni kwa sababu hiyo Mwalimu aliamua kutaifisha shule za kidini na kuziweka kwenye mamlaka ya Serikali na kisha kupokea wanafunzi wa dini zote. Hata hivyo, Mzee Ngize anasema nyakati hizo elimu ilikuwa duni, jambo ambalo Mwalimu alilipigia kelele sana katika hotuba zake na kwa vile ukoloni uliwanyima Watanzania wengi elimu, Mwalimu akaamua kuanzisha elimu ya watu wazima nchini kote.
    Anasema Mwalimu aliendelea kukerwa na Tanzania kutokuwa na chuo kikuu kwani kilichokuwa kinavuma ni Makerere cha nchini Uganda ambacho yeye mwenyewe Mwalimu alisoma, ndipo mwaka 1964 kilizinduliwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. “Baada ya kuanzishwa kwa chuo chetu, Watanzania tulinufaika na hasa Wahaya tulinufaika sana na kupata wasomi wengi walioko ndani na nje mipaka.
    Hata sisi kuitwa Nshomile (nimesoma) ni kutokana na nguvu ya Nyerere. “Kwa vile Watanganyika enzi hizo uwezo wao ulikuwa mdogo kuwasomesha watoto wao, Mwalimu aliamua kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu,” anasema. Anasema katika hakarati za uchaguzi mkuu zinazoendelea, kila mwanasiasa anataja elimu bure jambo ambalo anaamini linawezekana kama tutaweka mbele uzalendo na kulipa kodi kama inavyotakiwa ili mapato yakiongezeka na rasilimali za nchi hii zikatumika kwa maslahi ya wanyonge.
    Naye Fabian Massawe, Kanali mstafu wa Jeshi la Wananchi na Mkuu wa Mkoa wa Kagera mstaafu anasema kuwa Mwalimu Nyerere alisema amani ya nchi hii inalindwa na wananchi wenyewe ambao ni wazalendo. “Kwa msingi huo, kazi ya kuwafichua wanaotaka kuvunja amani ya nchi ni ya kila mmoja wetu,” anasema. Massawe ambaye pia ni Mwalimu mstaafu wa shule ya sekondari ya Jitegemee, anasema Mwalimu Nyerere atakumbukwa kwa mambo mengi ambayo si rahisi kuyazungumzia yote.
    Anasema kati ya mengi yanayomtuma kumkumbuka Baba wa Taifa ni pamoja na kuonesha msingi wa kujituma tangu alipoanzisha vuguvugu la siasa ili kuondokana na minyororo ya wakoloni. Anasema Mwalimu alijituma kwa kutembea mikoa yote nchini wakati huo ikiwa 17 kabla haijaongezeka kama ilivyo sasa akisaka uhuru na amani ya nchi yake.
    Anasema wakati huo usafiri wa Rais haukuwepo kama ilivyo sasa, jambo ambalo lilimfanya muda mwingi kutembea kwa miguu akisaka haki na uhuru wa Watanzania. “Sio kama sasa watu wanatumia helikopta kusaka uongozi, ambapo huwafanya wananchi wakusanyike kwa kutaka kuona kifaa hicho lakini yeye sehemu nyingi ya nchi alitembea kwa shida sana ili kuwahamasisha wananchi kudai uhuru,” anasema.
    Anasema siku hizi kuna wanasiasa wengi ambao wamekuwa wakitumia kivuli cha Mwalimu kutafuta uongozi ikiwemo kuomba kura lakini matendo yao na sifa zao huwezi kuzilinganisha na za Mwalimu,” anasema. Anasema ubadhirifu, rushwa kununua madaraka imekuwa vitu ambavyo Mwalimu alivipigia kelele sana mpaka kumnyima usingizi. “Namkumbuka baada ya kupata Uhuru alijenga umoja imara ambao hadi sasa unatuunganisha pamoja kama nchi ambapo leo nikienda Mtwara naishi bila kubughudhiwa na kuulizwa mimi ni kabila gani wala dini gani, jambo ambalo linaendelea kukuza matunda ya amani ambayo tunapaswa kuilinda kwa kumuenzi,” anasema Massawe.
    Anasema Mwalimu pia aliona mbali kuhusiana na masuala ya elimu, maana kabla ya uhuru na baada ya uhuru shule nyingi zilikuwa ni za wamisionari na chache ndio zilikuwa za serikali na hivyo hatua ya kuzitaifisha ilileta afueni kwa makundi ya kijamii kujihakikishia kusoma. Kanali mstaafu Massawe anawashauri wananchi, hususani vijana, kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kujituma na kufanya kazi, kujenga umoja na mshikamano kwa kukaa pamoja na kuzungumzia maendeleo yao na Taifa lao.
    Pia anawashauri kutumia rasilimali zilizopo hususani ardhi kujipatia kipato kuliko kukaa mijini na kukaa vijiweni wakihubiri siasa bila kuwa na malengo ya miaka ijayo. Anasema kuwa Mwalimu alikufa mwili ila kiroho yu hai kwani Watanzania wengi bado wanamkumbuka kwa dhati kabisa.

    Created by Gazeti la HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment