Rais Jakaya Kikwete. |
RAIS Jakaya Kikwete ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume ya Kimataifa ya Kuchunguza Jinsi ya Kugharimia Elimu Duniani (TICFGEO). Tume hiyo, inayoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Gordon Brown ambaye pia ni Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa (UN) wa Elimu Duniani, ina wajumbe 30, wakiwemo marais na mawaziri wakuu wa zamani, wataalamu wa elimu, wafanyabiashara kutoka sekta binafsi na wawakilishi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGOs) duniani.
Taarifa ya Ikulu iliyotumwa juzi kwa vyombo vya habari, imeeleza kuwa tume hiyo imeteuliwa na viongozi watano duniani wakishirikiana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon na ilitambulishwa kwa mara ya kwanza katika mkutano uliofanyika Septemba 29, mwaka huu mjini New York, Marekani.
Rais Kikwete alihudhuria mkutano huo wa kwanza wakati wa ziara hiyo Marekani, ambako pia alikuwa akiongoza Jopo ya Watu Mashuhuri Duniani wanaangalia jinsi dunia inavyoweza kujiandaa vizuri zaidi dhidi ya magonjwa ya milipuko.
Viongozi walioteua Tume hiyo ni Waziri Mkuu wa Norway, Erna Solberg; Rais wa Chile, Michelle Bachelet; Mkurugenzi Mkuu wa Unesco, Irina Bokoba; Rais wa Malawi, Peter Mutharika na Rais wa Indonesia Joko Widodo.
Tume hiyo ya elimu itawasiliana na kukutana na viongozi mbali mbali duniani, ili wabuni sera za elimu na watafiti wa masuala ya elimu ili kuiwezesha Tume hiyo kujenga hoja zinazokidhi umuhimu wa kuwepo kwa upatikanaji wa fedha za kutosha na uwekezaji katika kuleta usawa katika upatikanaji wa nafasi za elimu kwa watoto wa kike na kiume.
Aidha, Tume hiyo itaangalia jinsi gani dunia inavyoweza kuongeza uwekezaji katika elimu katika muda mfupi na katika muda mrefu na itapendekeza aina ya uwekezaji na hatua za kuchukuliwa.
Pia, Tume hiyo itapendekeza njia za kuwashawishi wakuu wa nchi na Serikali, mawaziri wa fedha, uchumi, elimu na ajira, magavana wa majimbo na serikali za mitaa pamoja na viongozi wa kibiashara na wawekezaji kuchukua hatua za kuwezesha ongezeko kubwa la fedha katika sekta ya elimu.
Miongoni mwa watu ambao watatumikia kwenye Tume hiyo pamoja na Rais Kikwete ni Rais wa zamani wa Mexico, Felipe Calderon, Rais wa zamani wa Kamisheni ya Ulaya, Jose Manuel Barroso, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Dangote Group, Aliko Dangote, Waziri Mkuu wa zamani wa Australia, Julia Gillard, Rais wa Benki ya Dunia, Jim Kim, na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Alibaba Group ya China, Jack Ma.
Wengine ni Mama Graca Machel wa Msumbiji, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Econet Wireless Group ya Zimbabwe,Strive Masiyiwa, Mwanamuziki Shakira Mebarak, Waziri wa zamani wa Fedha wa Marekani na Rais wa Heshima wa Chuo Kikuu cha Harvard, Lawrence Summers na Helle Thorning Schmitt, Waziri Mkuu wa zamani wa Denmark.
Created by Gazeti la HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment