TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inatarajia kutumia mfumo mpya wa
kielektroniki katika kujumlisha matokeo ya kura kwa lengo la kuondoa
makosa mbalimbali ya kibinadamu, yanayoweza kutokea kwa bahati mbaya
wakati wa kujumlisha matokeo hayo katika uchaguzi mkuu.
Mfumo huo mpya wa Menejimenti ya Matokeo (RMS), unatumia mashine za
kisasa zenye uwezo wa kuchapisha na kunukushi karatasi za kupigia kura
zaidi ya 60 kwa dakika moja.
Mkurugenzi wa NEC, Kailima Kombwey alisema jana kwamba Oktoba 11,
mwaka huu, waliwaalika wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(Tehama) kutoka vyama vyote vya siasa na mfumo huo ukapitishwa.
Akiwasilisha mada ya maandalizi ya uchaguzi, Kombwey alitaja makosa
yanayoweza kutokea katika kujumlisha kura ni pamoja na matokeo ya kituo
kimoja, kujumlishwa zaidi ya mara mbili, kukosea uandikaji wa namba na
usahihi wa ujumlishaji.
“Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 mfumo huu ulisanifiwa upya na
kutumika, hata hivyo kasoro chache zilioneshwa. Kwa uchaguzi wa mwaka
huu, tume imeboresha mfumo huu na kuondoa upungufu katika maeneo yote
yaliyokuwa na changamoto mwaka 2010,” alisisitiza Kombwey.
Alisema pamoja na mfumo huo, pia tume hiyo imeandaa mfumo mbadala,
alioutaja kuwa ni Spreadsheet Excel RMS, ambao utatumika iwapo kutakuwa
na changamoto katika kutumia mfumo uliondaliwa.
Aidha alisema tume hiyo inafanya maandalizi ya kutumia Mkongo wa
Taifa wa Mawasiliano kwa ajili ya kutuma matokeo yote, badala ya kutumia
mtandao wa simu za mkononi. “Katika uchaguzi wa mwaka 2010, utumaji wa
matokeo ulikuwa na changamoto nyingi. Kati ya majimbo 239 ni majimbo 150
tu yaliweza kutuma matokeo kwa mfumo uliokuwa umeandaliwa, ambao ni
kupitia mtandao wa simu za mikononi, matokeo yaliyobaki yalitumwa kwa
nukushi ,” alifafanua.
Alisema kitendo cha kutumia mkongo huo wa taifa, kitasaidia
upatikanaji wa matokeo mapema kama inavyokusudiwa, ingawa pia njia
mbadala ya kutuma matokeo kwa nukushi imeandaliwa na halmashauri zote
zimepatiwa vifaa, vitakavyowezesha utumaji wa matokeo kwa haraka
kufanyika.
Aidha, tume imekubaliana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuhusu kutumia Mkongo wa Mawasiliano wa
Tamisemi, kusaidia utumaji wa taarifa za matokeo kutoka katika
halmashauri hadi NEC. Kuhusu elimu, Kombwey alisema jumla ya asasi za
kiraia 451 ziliomba kutoa elimu ya mpiga kura.
Kati ya hizo ni asasi 447 zilikidhi vigezo na hivyo kupewa kibali cha
kutoa elimu hiyo. Alisema asasi hizo zimesaini Maadili ya Utoaji wa
elimu ya Mpiga kura na kukubali kutumia mwongozo wa Elimu ya Mpiga kura.
Created by Gazeti la HabariLeo
Tuesday, 13 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment