Mbunge wa Bumbuli anayemaliza muda wake, Januari Makamba.
SERIKALI imeeleza kushangazwa na uzushi kwamba siku ya uchaguzi mkuu,
data za mawasiliano pamoja na umeme vitazimwa, jambo ambalo imetaka
wananchi kupuuza taarifa hizo potofu.
Taarifa hizo ambazo Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba ameziita ni uzushi, zinadaiwa kutolewa na
baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani wakidai kwamba serikali
imepanga kufanya hivyo ili wananchi washindwe kupata taarifa za matokeo
ya uchaguzi.
“Kwanza napenda ifahamike kuwa hakuna chama chochote cha siasa
kitakachofaidika kikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM), endapo data za
mawasiliano zitazimwa, hivyo nawaomba wananchi wasiamini maneno ya
uzushi yasiyo na ukweli hata chembe,” alisisitiza January.
Alisema huduma ya data zina umuhimu mkubwa katika uchumi wa Tanzania
kuliko siasa, kwani kwani ofisi nyingi zikiwemo taasisi za kibenki
zinategemea data hizo katika shughuli zake za kila siku.
“Sasa ukisema tutazima data ni sawa na ku-paralyze (kusimamisha)
uchumi kwani watu hawataweza hata kutoa fedha zao benki, jambo ambalo ki
ukweli haliwezi kufanyika,” alisisitiza.
Alisema ni Wizara yake na Serikali kwa ujumla, imekuwa ikilinda na
kurekebisha mitandao kuhakikisha inafanya kazi vizuri hasa katika
kipindi hicho cha uchaguzi kutokana na ukweli kuwa kutakuwa na taarifa
nyingi zinazohitajika kufikia wananchi.
“Hatutegemei watu kutumia vibaya mitandao ya kijamii na kusababisha
taharuki lakini hata wakifanya hivyo, Sheria ya kudhibiti mitandao ipo,
itatumika kudhibiti na si kuzima data kama inavyodaiwa,” alisema
January.
Aidha alisema taarifa hizo zilizosambazwa ambazo hata yeye ameziona,
zinasambazwa na wanasiasa wenye nia ya kutengeneza hamaki kwa wananchi
jambo ambalo si sahihi. Wakati huo huo, msemaji wa Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco), Adrian Severine, alisema kwa sasa shirika hilo,
haliwezi kuzungumzia jambo hilo, hadi pale wanasiasa wote wanaodai
mtaani kuwa wanazo taarifa za kuzimwa umeme nchini siku ya uchaguzi
watoe uthibitisho.
“Huu ni wakati wa uchaguzi, hawa wanasiasa watasema mengi tu, sasa
sisi kama shirika hatuwezi kusema lolote wala kukanusha taarifa hizi
mpaka hao wanaodai kuwa wana taarifa kuwa tumeamriwa tuzime umeme
watuthibitishie. Siwezi kukanusha kitu ambacho hakina uthibitisho,”
alisisitiza Severine.
Alisema kwa sasa shirika hilo, limeamua watu wote watakaozusha
taarifa kuhusu utendaji au shughuli za shirika hilo na kuthibitika kuwa
ni uongo, wataburuzwa mahakamani ili iwe fundisho. “Kuna watu tayari
tumewafungulia mashitaka kwa ama kuandika au kuzungumzia taarifa za
uongo kuhusu Tanesco, kesi zinaendelea mahakamani,” alisema.
Juzi katika mkutano wa viongozi wa siasa ulioandaliwa na Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdallah Safari, alidai
kuwa chama hicho kinazo taarifa za uhakika kuwa siku ya uchaguzi umeme
na data vitazimwa ili wananchi washindwe kupata taarifa za uchaguzi.
Pamoja na kiongozi huyo, kutoa kauli hiyo, pia baadhi ya mitandao nayo
imekuwa ikisambaza taarifa hizo.
Created by Gazeti la HabariLeo
Tuesday, 13 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment