Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jji Mstaafu, Damian Lubuva akiwa katika mkutano na viongozi wa vyama vya siasa nchini kujadili namna ya kutekeleza sheria za uchaguzi. |
SIKU 12 kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani nchini, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imebainisha idadi kamili ya Watanzania wanaostahili kupiga kura siku ya Oktoba, 25, mwaka huu), kuwa ni milioni 22.7 na si milioni 23.7 ya awali.
Hayo yamebainika baada ya tume hiyo kumaliza uhakiki na uchakataji wa Daftari la Wapiga Kura kupitia mfumo wa Biometric Voters Registarion (BVR). Kutokana na idadi hiyo mpya, tume hiyo imefuta na kuengua katika daftari hilo watu 1,031,266 kutokana na kukosa sifa za kuwepo kwenye daftari hilo.
Waliofutwa ni pamoja na wananchi 181, 452 waliojiandikisha zaidi ya mara moja hadi mara nane kwa mtu mmoja. Aidha tume hiyo, imevitaka vyama vya siasa nchini katika ngwe ya mwisho ya kampeni, kutumia majukwaa ya siasa kunadi sera ili wananchi waweze kushawishika na kuwachagua.
Vimetakiwa kuacha kutumia vibaya majukwaa, kuchafuana na kuichafua tume hiyo kwa kutoa taarifa zisizo sahihi. Hayo yalibainishwa na viongozi wa tume hiyo, ambao ni Mwenyekiti Jaji Damian Lubuva na Mkurugenzi wa tume hiyo, Kailima Kombwey, wakati tume hiyo ilipokutana na viongozi wa vyama vya siasa, kujadili mwenendo wa kampeni na maandalizi ya uchaguzi.
Akizungumza katika mkutano huo, Kombwey alisema kwa sasa tume hiyo imekamilisha maandalizi ya kuboresha daftari la wapiga kura. Alisema baada ya uhakiki na uchakataji wa taarifa za wapiga kura, Tume imebaini kuwa wapigakura milioni moja, hawakustahili kuwemo kwenye daftari hilo.
Alisema idadi ya wapiga kura milioni 23.7 ya awali, ilipatikana kutokana na taarifa zilizopatikana moja kwa moja kwenye vituo vya kupigira kura ; na baada ya uhakiki na uchakataji huo, idadi kamili ya wapiga kura wanaostahili kupiga kura Oktoba 25, mwaka huu ni milioni 22.7.
Alisema kati ya wapiga kura hao milioni moja, ambao taarifa zao zimeondolewa, wananchi 181,452 walibainika kuwa walijiandikisha zaidi ya mara moja hadi mara nane kwa mtu mmoja.
Aidha alisema baada ya uhakiki huo, tume hiyo ilibaini wananchi 845,944 ni wale waandikishaji wa mfumo wa Biometric Voter Registration (BVR), ambao jumla yao walikuwa 74,502 waliokuwa wakifanya mafunzo ya vitendo kabla ya kuanza uandikishaji wenyewe.
“Pia wananchi 3,870 wamebainika kuwa waliandikishwa wakiwa si raia wa Tanzania na hivyo vitambulisho vyao vimerejeshwa na taarifa zao kufutwa kwenye kanzidata ya Daftari la Kudumu,” alisema Kombwey.
Mkurugenzi huyo alisema katika maandalizi ya uchaguzi ambayo bado yanaendelea, tume hiyo imeandaa vituo vya kupigia kura 65,105. Kati ya hivyo, vituo vilivyopo Tanzania Bara ni vituo 63,525 na Zanzibar vituo 1,580, ambapo kila kituo kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wapigakura 450 na wasiozidi 500.
“Kituo kitakapokuwa na wapigakura zaidi ya 500 kitagawanywa katika vituo viwili kwa idadi sawa kwa kila kituo. Wapiga kura wanashauriwa kwenda katika vituo walivyojiandikisha kupiga kura siku nane kabla ya siku ya kupiga kura ili kujua vituo vyao halisi vya kupigia kura,” alisisitiza.
Pia alisema wananchi wataweza kupata taarifa zao, zilizoko kwenye kanzidata kwa kutumia simu zao za kiganjani kupitia ujumbe mfupi wa maneno, bila wao kulazimika kufika vituoni kupitia namba *152*00# na kufuata maelekezo.
Alisema kupitia uteuzi uliofanywa na tume hiyo, wagombea wa kiti cha urais waliopitishwa na tume hiyo, watakaoshindanishwa katika uchaguzi huo ni nane, ambapo mgombea mwanamke ni mmoja na wengine saba wanaume.
Alisema idadi ya wagombea ubunge, waliopitishwa kuwania majimbo 264 yaliyopitishwa na NEC ni wagombea 1,218, kati yao wanaume ni 985 na wanawake ni 233. Wagombea udiwani wanaowania kata 3,957 ni 10,879, ambapo wanaume ni 10,191 na wanawake 679.
Katika orodha hiyo, vyama vilivyosimamisha wagombea wengi katika nafasi za udiwani ni CCM, Chadema, ACT, CUF, ADC na NCCR-Mageuzi. Kombwey alisema tume hiyo imeteua na kuwapatia mafunzo watendaji 30 ngazi ya mikoa, 972 ngazi ya jimbo na 9,914 ngazi ya kata, ambao kazi yao ni kuratibu na kusimamia uchaguzi , wasimamizi wa vituo na makarani waongozaji.
Kwa upande wake, Jaji Lubuva alisema tume hiyo inasikitika kutokana na baadhi ya vyama vya siasa kutumia majukwaa yao vibaya na kuwaomba katika kipindi hiki cha kuelekea ukingoni mwa kampeni, kusisitizia zaidi sera zao na kutoa taarifa sahihi ikiwemo elimu ya uchaguzi kwa wananchi.
“Tume inawaomba kuepuka kutoa taarifa za shutuma zisizo sahihi kuhusu tume na badala yake mjikite katika kufikisha taarifa zilizo sahihi na zilizokusudiwa kwa wafuasi wenu na wananchi wote kwa ujumla,” alisema.
Alisema tume hiyo imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania mwenye sifa za kupiga kura, anapiga kura yake bila kubughudhiwa. “Tumesikia baadhi ya vyama vinashawishi wapiga kura wake kutoondoka vituoni baada ya kupiga kura, kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi hakuna mtu anayeruhusiwa kufanya mkutano, kuvaa sare au kuwa na kadi ya chama anachokiunga mkono katika sehemu ya kupigia kura,” alisema.
Akijibu hoja ya baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa waliotaka mfumo mpya wa matokeo uhakikiwe kwanza, Lubuva alisema mfumo huo ni bora na una lengo la kuondoa dhana nzima ya wizi wa kura. “Lakini pia mfumo huu umeletwa kwetu na watu huru wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), “ alisema.
Created by Gazeti la HabariLeo
0 comments:
Post a Comment