Maofisa wa manispaa ya Ilala wakikagua nyeti za ng’ombe walizokuta zimeanikwa kwenye
kiwanda bubu kilichopo Tabata Bima jijini Dar es Salaam jana ambapo
walikifungia na kukitoza faini ya Sh milioni 10.
SERIKALI imekifungia na kukitoza faini ya Sh milioni kumi kiwanda
bubu cha Wachina, kilichopo Tabata Bima, Dar es Salaam kwa kukiuka
taratibu za nchi. Kiwanda hicho kilikuwa kikijihusisha kukausha nyeti za
ng’ombe na kusafirisha bila kuwa na vibali.
Kibali chao cha kufanya kazi nchini, kilikuwa cha kuuza vyombo katika
eneo la Kariakoo, katikati ya jiji la Dar es Salaam. Kiwanda hicho
kilifungwa jana na timu ya maofisa kutoka Halmashauri ya Manispaa ya
Ilala.
Maofisa hao wa Manispaa walifika kiwandani hapo, baada ya kupokea
malalamiko kutoka kwa wakazi wa eneo hilo, kufuatia harufu kali ya nyeti
hizo, ambazo zilikutwa zimeanikwa ili kuzikausha.
Pia maofisa hao walikuta pembe za ng’ombe zimefungwa kwenye viroba.
Maofisa hao walipofika kiwandani hapo, waligonga kwa muda mrefu, kisha
walifungua vijana ambao walikuwa wakikusanya taka hizo na kwenda
kuzitupa. Baada ya ukaguzi wa kiwanda hicho, maofisa hao wa manispaa
walikuta raia wawili wa China, ambao awali walijifanya hawajui
Kiswahili.
Mmoja wao alianza kuongea, ingawa baadaye alimwita mkalimani.
Msimamizi wa kiwanda hicho, aliyejitambulisha kwa jina la Faing Zhou,
alisema nyeti hizo wanazipata machinjioni na zinakusanywa kwa ajili ya
kupelekwa China kwa ajili ya chakula cha mbwa.
Pia, alisema pembe za ng’ombe zinapelekwa China kwa ajili ya
kutengenezea vifungo vya nguo, vitana na vitu vingine ambavyo
hakuvitaja. Hata hivyo, vijana waliokuwa katika eneo hilo, walidai kuwa
nyeti hizo zinapelekwa China kwa ajili ya kutengeneza dawa za kuongeza
nguvu za kiume, jambo ambalo mchina huyo alisema sio kweli.
Wachina hao walipotakiwa kutoa vibali vya kufanya shughuli hizo,
walidai hawana kibali chochote na kwamba walikuwa katika mchakato wa
kupata vibali hivyo. Hata hivyo, Wachina hao walikuwa na vibali vya
kufanya biashara za vyombo vya ndani katika Mtaa wa Aggrey uliopo
Kariakoo.
Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Ilala, Feada Magesa akimfafanulia raia
huyo wa China ambaye ni msimamizi wa kiwanda hicho, alisema kulingana
na mazingira hayo kuwa machafu mno, yanayohatarisha maisha ya wakazi wa
eneo hilo, ikizingatiwa nje ya kiwanda hicho kuna shule ya msingi,
kiwanda kinafungwa sambamba na kupigwa faini hiyo.
Ofisa wa Afya wa Kata ya Tabata, Jacob Mjata alisema wamefanya
ukaguzi na kukuta hali mbaya katika kiwanda hicho, ambacho kinakausha
nyeti na pembe za ng’ombe kiholela.
“Tulifanya ukaguzi katika eneo la kiwanda hiki na kukuta uchafu wa
mazingira kupelekea majirani kuishi maisha magumu kufuatia harufu kali
na inzi wengi wanaotoka kiwandani hapo,” alisema Mjata.
Created by Gazeti la HabariLeo
Thursday, 8 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment