Thursday, 8 October 2015

Tagged Under:

Magufuli afichua mpango mawakala CCM kuhongwa

By: Unknown On: 03:04
  • Share The Gag

  • Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli.

    MGOMBEA Urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli ameelezea kuandaliwa kwa mpango wa kugawa fedha kwa mawakala siku ya upigaji kura ili kushawishi kuchaguliwa kwa mmoja wa wagombea urais wa upinzani na hivyo amewataka watakaofikiwa na fedha hizo kuzichukua lakini bila kumchagua mgombea huyo.
    Katika hatua nyingine, siku chache baada ya Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi ambaye pia ni kiongozi mshirika wa Ukawa, kuelezea wasiwasi wa kambi hiyo kwamba upo uwezekano wa kuzuka vurugu baada ya Uchaguzi Mkuu, Dk Magufuli amesema hayupo tayari kuwa Rais katika Tanzania isiyo na amani.
    Tangu alipoingia katika Mikoa ya Kanda ya Kaskazini, ambayo awali ilikuwa ikidhaniwa kuwa ngome kuu ya upinzani nchini, Dk Magufuli amekuwa akifichua siri hiyo ya kuwepo mpango huo mchafu wa kutumia fedha siku ya uchaguzi, lakini akasisitiza kuwa atashinda urais licha ya mbinu hizo.
    Juzi akiwa wilayani Monduli katika miji ya Mto wa Mbu, Monduli Mjini na jana alipofanya ziara mkoani Kilimanjaro katika Wilaya za Siha, Hai, Dk Magufuli alisema wapo watu watapangwa jirani na vituo vya kupiga kura kwa kazi hiyo ya kugawa fedha ili kushawishi mgombea mmoja wa upinzani kuchaguliwa.
    Bila kumtaja jina ni mgombea yupi anayeratibu mpango huo, Dk Magufuli aliwataka wananchi watakaobahatika kukumbana na fedha hizo kuzichukua, lakini watakapofika ndani ya chumba cha kupiga kura, wamchague yeye ili awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
    Akizungumzia amani ya Tanzania, ikiwa ni siku chache tangu Mbatia alipodai kuwepo kwa uwezekano wa kuzuka kwa vurugu baada ya uchaguzi kwa kile alichoita uwezekano wa CCM kuiba kura na au kukataa kukabidhi nchi pale Ukawa watakaposhinda urais, Dk Magufuli alisema hayupo tayari kuwa Rais wa Tanzania isiyo na amani.
    Aidha, mgombea huyo anayetajwa na wadadisi wa masuala ya kisiasa kutoa hotuba nzuri na yenye majibu ya matatizo ya wananchi ikiwemo ajira, huduma za jamii, uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla alipohutubia katika mikoa ya Kaskazini amesisitiza kuwa hataki urais ili kujilimbikizia ‘urais’.
    Katika hatua nyingine; mlezi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema Dk Magufuli ni aina ya Rais anayehitajika hivi sasa ili kukomesha serikali kuendeshwa na watu aliowaita ‘wapiga dili’.

    Created by Gazeti la HabariLeo

    0 comments:

    Post a Comment