Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi akifanya mazoezi ya viungo baada ya
kumaliza matembezi ya kilometa tano ya Dar Rotary mwaka juzi katika
bwalo la Maofisa Polisi OysterBay.
MBIO za nne za Dar Rotary zitafanyika Jumatano Oktoba 14 siku ya
Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere. Mbio hizo ambazo hufanyika kila mwaka
zikiwa na lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya kuhudumia jamii,
zimekuwa zikiongezeka umaarufu wake, ikiwemo kuwashirikisha wanariadha
wengi zaidi.
Pia mbio hizo sasa zimekuwa zikiwashirikisha wanariadha wa ndani na
nje ya nchi, huku zawadi zake zikiboreshwa kila mwaka na kuwa kivutio
kikubwa kwa washiriki. Waandaaji wa mbio Mbio hizo zimekuwa zikiandaliwa
na Dar Rotary kwa kushirikiana na Bank M kwa kusaidiwa na wadhamini
mbalimbali, mbali na wanariadha pia hushirikisha familia kwa ajili ya
mbio tofauti tofauti.
Baadhi ya mbio ambazo hushindaniwa ni pamoja na mbio za kilometa 21,
mbio za baiskeli, mbio za kilometa 9 na zile za kutembea ambazo zina
umbali wa kilometa 5. Waandaaji wa mbio hizo wamekuwa wakishirikiana na
Riadha Tanzania (RT) kufanikisha mbio hizo zenye lengo la kukusanya
fedha kwa ajili ya kutatua matatizo mbalimbali ya jamii. Ujumbe wenyewe
Ujumbe wa mwaka huu ni Okoa Maisha, ambapo waandaaji wanakusanya fedha
kwa ajili ya kujenga hospitali ya kutibu magonjwa ya moyo.
Kwa muda mrefu wagonjwa wa moyo nchini kwetu wamekuwa wakipelekwa
nchini India kupata matibabu hayo ya moyo, ambayo ni ghali sana na
kuwafanya wagonjwa wengi kushindwa kwenda kutibiwa nje. Ushindani
wenyewe Mbio za mwaka huu zinatarajia kuwa na ushindani mkubwa zaidi na
tayari baadhi ya wanariadha kutoka nje ya nchi wameshathibitisha
kushiriki mbio hizo za aina yake.
Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Mkuu wa RT, Ombeni Zavalla, baadhi ya
wanariadha wa Kenya, Rwanda na Malawi wamethibitisha kushiriki mmbio
hizo. Zavalla aliwataja baadhi ya wanariadha hao kuwa ni pamoja na wale
wanaotoka Rwanda, Malawi, Kenya, Ethiopia na Afrika Kusini
wameshathibitisha kushiriki katika mbio za mwaka. Hakuna asiyejua kuwa
wanariadha wa Kenya, Ethiopia na hata wale wa Rwanda ni wazuri, hivyo
mwaka huu tunatarajia ushindani wa aina yake katika mbio za mwaka huu.
Kwa mujibu wa Zavalla, Rwanda imethibitisha kuleta wanariadha wanne,
ambao ni Robert Kajuga, Potien Ntawoyirushintege, Salome Nyirarunkundo
na Innocent Uwamohoro wakati Afrika Kusini ikimleta Vuyisile Tshoba.
Malawi inatarajia kuwaleta Happy Ndacha, Mcherenje, Francis
Khanje,Rashid Taimu, Godfrey Mpunga, Doris Fisho na Tereza Master wakati
Zanzibar wakitarajiwa kuwaleta Philipo Jacob Mambo, Abdallah Jecha
Abdallah na Asma Rajabu Mukhandi. Kenya imesema itawaleta Tom Mutie,
Patrick Mwika, Mwendwa Ngeti, Shelmith Muriuki, Josephine Masau na
Hellen Nzemba wakiwa na kocha Paul Mutwii na Ethiopia ikithibitisha
kuleta wanariadha watatu.
Kwa sasa wanariadha wa Tanzania wako katika maandalizi makali kabla
ya kushiriki mbio hizo ambazo hutoa zawadi nono kwa washindi kwa upande
wa wanawake na wanaume. Mgeni rasmi Rais mstaafu wa Awamu ya Pili Ali
Hassan Mwinyi ndiye atakuwa mgeni rasmi katika mbio za mwaka huu
zitakazoanzia na kumalizia kwenye viwanja vya The Green au viwanja vya
Farasi Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Mwaka jana Mwinyi ndiye pia alikuwa mgeni rasmi ambapo mbali na
kuzindua mbio hizo, kutoa zawadi kwa baadhi ya washindi, pia alishiriki
matembezi ya kilometa tano. Kwa mujibu wa taarifa, kauli mbiu ya mwaka
huu ni ‘Okoa Maisha’ ikiwa na lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya
kujenga kituo cha afya, ambacho kitakuwa kinahudumia watu wenye matatizo
ya moyo.
Mwaka jana karibu wanariadha 1,000 walishiriki katika mbio hizo,
ambazo kila mwaka zimekuwa na msisimko mkubwa. Kwa mujibu wa mwenyekiti
wa Kamati ya Maandalizi Sharmila Bhatt, mbio hizo zitafanyika Oktoba 14
jijini Dar es Salaam. Naibu Ofisa Mkuu wa Bank M, Jacqueline Woiso
alisema kwa mara nyingine wamekubali kushirikiana na Rotary Clubs jijini
Dar es Salaam kwa sababu lengo la mbio hizo ni kusaidia jamii.
“Bank M siku zote iko mstari wa mbele kusaidia jamii. Sera zetu
wakati wote ni kufanya kazi pamoja taasisi zigine kusaidia jamii kwa
njia tofauti,”aliongeza. Mwinyi pia ni mlezi wa Rotary Dar Marathon.
Created by Gazeti la HabariLeo
Sunday, 11 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment