Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa. |
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Utumishi, Hab Mkwizu alisema madeni ya mishahara ya kuanzia Desemba 2013 hadi Agosti mwaka huu, yanahusu walimu 60,322 sawa na madai ya Sh bilioni 29.8 yaliyowasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali kwa ajili ya uhakiki na tayari halmashauri 103 zimeshahakikiwa.
Alisema uhakiki wa halmashauri zilizobaki unatarajiwa kukanilika Oktoba 11 mwaka huu na fedha zote zitatumwa kwa halmashauri husika mara baada ya uhakiki kukamilika. Kati ya kiasi hicho cha fedha wanazodai walimu, Sh bilioni 21 ni za waalimu shule za msingi ambao ni 44, 715 na Sh bilioni 8.6 wa shule za sekondari ambao ni 15,607.
“Walimu 45,453 wanadai malimbikizo ya mishahara Sh bilioni 32 hadi kufikia Septemba mwaka huu. Serikali ilikuwa imewalipa walimu 3,979 Sh bilioni 2.3 na wengine ambao bado wanadai watalipwa mwezi huu,” alisema Mkwizu.
Alisema madeni ya Sh bilioni 1.73 ya walimu 1,667 ndio yatalipwa mwezi huu huku wengine wakiendelea kulipwa kila mwezi kadiri ya uhakiki unavyokamilika na kwamba madeni yasiyohusu mishahara yamekuwa yakilipwa kupitia fungu la matumizi mengineyo.
Mkwizu akifafanua madeni ya waalimu, alisema Serikali imeagiza pia kila halmashauri kufanya vikao vya kuwapandisha madaraja walimu mapema iwezekanavyo kabla ya Novemba mwaka huu. “Walimu waliokaa kwenye cheo kimoja kwa muda mrefu na wale wanaokaribia kustaafu watapewa kipaumbele katika upandishaji vyeo,” alisema Mkwizu.
created by Gazeti la HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment