Saturday, 17 October 2015

Tagged Under:

Magufuli ataja tiba ya ajira, foleni Dar

By: Unknown On: 08:59
  • Share The Gag




  • Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli akihutubia mkutano wa kampeni Jimbo la Ukonga, eneo la Moshi Baa, Dar es Salaam jana. (Na Mpigapicha Wetu).

    MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli ameelezea mbinu atakazozitumia kumaliza tatizo la ajira nchini na kukabili foleni katika Jiji la Dar es Salaam akichaguliwa kuingia Ikulu huku pia akiahidi kujenga Bandari Kavu Kisarawe mkoani Pwani.
    Katika hatua nyingine, amewapongeza vijana waliopiga deki barabara ya lami ili kumkaribisha Mgombea Urais kupitia Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa mjini Musoma, kwa kile alichosema hatua hiyo inasaidia kutunza barabara za lami alizozijenga na hivyo kuomba utaratibu huo uwe endelevu.
    Aliyasema hayo katika mikutano ya kampeni iliyofanyika Kisarawe mkoani Pwani na Ukonga jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na maelfu ya mashabiki na wapenzi wa chama hicho.
    Kuhusu tatizo la ajira, Dk Magufuli alisema suala hilo limekuwa likiitafuna nchi katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kufa kwa viwanda na kuwaahidi wakazi wa Kisarawe na Ukonga kuwa atatumia nguvu zake zote katika kufufua viwanda vilivyokufa na kujenga vipya.
    “Nataka niwahakikishie wana Kisarawe, nitajenga Bandari Kavu hapa ambayo itatoa ajira kwa vijana na makundi mengine na pia itawezesha kukuza uchumi wa wana- Kisarawe.
    “Nafahamu pia kuwa mmetenga eneo maalumu kwa ajili ya maendeleo ya viwanda katika eneo la Visegese. Nitalitumia eneo hilo ipasavyo maana dhamira yangu ni kuhakikisha kuwa tunakuwa na Tanzania ya viwanda,” alisema Dk Magufuli.
    Akizungumzia nguvu ya viwanda katika kukuza ajira, Dk Magufuli alisema ni ndoto kwa Taifa kukuza ajira kwa watu wake kwa kutegemea rasilimali kama madini kwa vile mchango wake ni mdogo.
    “Ninapozungumza hili nazungumza kwa uhakika. Nikiwa nasimamia Wizara ya Ujenzi, niliweza kuzalisha ajira milioni 1.13 kila mwaka. Nilikuwa natoa ajira 8,500 kwa makandarasi, ajira 15,000 kwa wahandisi na nyinginezo nyingi".
    Foleni barabarani Dar
    Katika hatua nyingine, Dk Magufuli alitoboa siri akisema kuchelewa kujengwa kwa barabara za juu jijini Dar es Salaam kumetokana na msimamo wake wa kutaka kumaliza kwanza ujenzi wa barabara zote za kuunganisha mikoa kwa kiwango cha lami ili kufungua njia kuu za nchi.
    Alisema mpango uliopo sasa ni kuanza kujengwa kwa barabara za juu (fly over) saba kwa kasi kwa kuanzia eneo la Tazara ambapo jana mchana alisaini mkataba wa kuanza ujenzi huo.
    “Kuanzia Januari mwakani (2016) tutaanza ujenzi wa barabara ya lami ya njia sita kutoka Dar es Salaam- Mlandizi hadi Morogoro kwa gharama ya Sh trilioni 2.3, ambayo pia itasaidia kupunguza foleni Dar kwa vile magari yataweza kuingia na kutoka kwa urahisi kuliko sasa,” alisema.
    Waliodeki barabara
    Katika tukio lisilotarajiwa, Dk Magufuli alitumia mikutano ya jana, kuwapongeza vijana waliodeki barabara ya lami mjini Musoma ili kumkaribisha Lowassa na akasema wameweza kufanya hivyo kwa vile barabara hiyo ni ya lami, na kwamba wasingeweza kuipiga deki kama ingekuwa ya vumbi.
    Baada ya kumaliza ziara katika miji hiyo ya Kisarawe na Ukonga, Dk Magufuli aliendelea na ziara yake ya kampeni Kisiwani Pemba kwa kufanya mikutano mingine ya kampeni jioni jana.

    Created by Gazeti la HabariLeo

    0 comments:

    Post a Comment