MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli
amesema endapo uchaguzi utafanyika leo, atashinda kwa asilimia 80,
lakini akasema anachokifanya sasa ni kupita kwa wananchi ili kuongeza
idadi ya kura kufikia asilimia zaidi ya 90.
Aidha, amesema dhamira yake, pamoja na kuwa lengo la kuifanyia nchi
mambo mengi, anataka kuhakikisha anarejesha hadhi ya Jiji la kitalii la
Arusha ambalo katika miaka ya hivi karibuni limekuwa likikabiliwa na
maandamano ya mara kwa mara, lakini pia ameeleza kuguswa na kuzorota kwa
hadhi ya wilaya la Monduli, aliyoiita anaiheshimu mno kutokana na
kuwahi kutoka Waziri Mkuu mwadilifu na mchapakazi, Hayati Edward Moringe
Sokoine.
Kutokana na hayo, amewaomba wakazi wa Jimbo la Monduli, Longido na
Arusha kutopoteza kura zao kwa vile endapo watamchagua mgombea wa
Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa watapoteza kura zao.
Katika hatua nyingine, Dk Magufuli amewapa pole wakazi wa Mto wa Mbu
na Monduli kwa jimbo lao kukabiliwa na kero nyingi za wananchi, akisema
wapo wagombea wa CCM ambao huwa wabaya na ambao hawajali matatizo ya
wananchi wanaowachagua.
Aliyasema hayo alipohutubia mikutano ya hadhara katika miji
mbalimbali ya mkoa wa Arusha, ukiwamo mkubwa katika Uwanja wa Sheikh
Amri Abeid katikati ya Jiji la Arusha. “ Naomba mnichague kwa kura
nyingi. Nitafanya kazi kama Sokoine aliyewatumikia Watanzania kwa bidii
na moyo wake wote.
Sokoine alichukia ufisadi na aliupiga vita,” alisema Magufuli. Kuhusu
uhakika wa ushindi, Dk Magufuli alisema; “Naomba niwaombe wananchi wa
Monduli na Arusha, mnichague mimi, maana ni lazima nitakuwa Rais, hivyo
ni vyema mkanipa hizo kura zenu ili zisipotee.
“Endapo uchaguzi utafanyika leo, nitashinda kwa zaidi ya asilimia 80,
ninachofanya sasa ni kupita ili kuomba kura zaidi ili zifike kura
asilimia zaidi ya 90,” alisema Dk Magufuli. Mgombea huyo wa CCM
aliwahakikishia wakazi wa Arusha kwamba endapo atachaguliwa kuwa rais,
atafanya kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa bila kuwabagua wananchi kwa
utofauti wao wa vyama, dini, makabila wala maeneo wanayotoka.
Aidha, aliwapa pole wakazi wa Jimbo la Monduli katika Mji wa Mto wa
Mbu, waliojitokeza na kueleza kilio chao kwa kukosa huduma muhimu za
jamii ikiwemo maji, masoko, benki, mabwawa ya maji kwa mifugo na ofisi
ya malipo ya umeme, hatua inayowafanya kusafiri hadi wilaya jirani ya
Karatu kupata huduma hizo.
Mmoja wa wananchi hao, Donosia Thomas kutoka kijiji cha Mnazi Mmoja
wilayani Monduli, alimwambia Dk Magufuli kuwa mbali ya matatizo hayo
wananchi wanalazimishwa kuchangia debe la mahindi, kilo tano za
maharage, kilo moja ya chumvi, kwa ajili ya chakula cha mchana kwa
wanafunzi na kwamba wazazi wanaposhindwa, watoto wao hufukuzwa shule.
Alisema umasikini uliopo Monduli unatokana na kuwepo kwa wanaCCM
wabaya ambao huchaguliwa na wananchi bila kujua kuwa wapo wanaCCM wabaya
zaidi na ambao hawapaswi kuchaguliwa kwa vile hawana uchungu na
matatizo ya wananchi.
Dk Magufuli alisema ili kumuenzi Sokoine akiwa Rais atafufua upya
mabwawa ya maji kwa mifugo ambayo yalikufa baada ya kifo cha Waziri Mkuu
huyo wa zamani kilichotokana na ajali ya gari Aprili 12, 1984 mkoani
Morogoro.
Kutaifisha viwanda Dk Magufuli anayesifika pia kwa uchapakazi,
ameongeza kuwa akichaguliwa kushika wadhifa huo, atataifisha viwanda
vyote ambavyo wamiliki wake wameshindwa kuviendesha.
Aliahidi pia kuwachukulia hatua kali watendaji wa Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) kutokana kukatikakatika kwa umeme na kwamba anafanya
utafiti kubaini kama kitendo hicho ni hujuma dhidi yake na ikibainika
hivyo atawafukuza mara moja watendaji wa shirika hilo baada ya
kuapishwa.
Aliwataka Mawaziri wanaosimamia sekta ya umeme akiwemo Waziri wa
Nishati na Madini, George Simbachawene ambaye kwa sasa anaomba kura za
ubunge katika Jimbo la Kibakwe mkoani Dodoma, kufuatilia kujua chanzo
cha kukatikakatika kwa umeme haraka.
Mkutano wa Arusha Akihutubia maelfu ya wananchi wa mji wa Arusha
waliohudhuria mkutano wa kampeni wa CCM jana, Dk Magufuli alisema
wamiliki wa viwanda waliovichukua viwanda hivyo baada ya kubinafsishwa
wahakikishe kuwa viwanda hivyo vinafanya kazi kabla ya kuapishwa.
Alisema serikali yake kamwe haitakubali kuona wananchi wakikosa ajira
wakati vipo viwanda vilibinafsishwa na waliovichukua wamevitelekeza na
alitolea mfano viwanda vya General Tyre na Kilitex kuwa wamiliki waanze
kuzalisha haraka ili kuwapatia wananchi ajira.
“Siwezi kukubali katika uongozi wangu, watu wachache wa juu wafaidi
kutokana na ufisadi huku wananchi wengi wakiwa masikini, nawaahidi kuwa
serikali yangu itakuwa ni kazi tu,” alisema Dk Magufuli.
Alisema atakapoingia madarakani ataufanya mji wa Arusha kuwa kitovu
cha utalii na ushirikiano wa mataifa ya Afrika Mashariki, hatua
aliyosema itachangia maendeleo ya haraka kwa mji huo huku akisema katika
kipindi cha miaka mitano iliyopita sifa ya Arusha imetetereka kutokana
na fujo za mara kwa mara.
“Nawahakikishia viongozi wenzangu wa Afrika Mashariki wasiwe na
wasiwasi na Magufuli, tutaendeleza ushirikiano ulioanzishwa na
watangulizi wangu ili kuhakikisha kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki
inakuwa bora zaidi na uchumi wa mataifa yote unaimarika,” alisema.
Alitoa ahadi kwa wafanyakazi kushusha chini makato ya mshahara kutoka
asilimia 11 ya sasa, huku akisema kazi hiyo imeshaanza kufanywa
kutokana na kuwepo kwa Tume inayoendelea kutathmini malipo ya mishahara
kwa wafanyakazi ili Watanzania wote wapate mishahara mizuri.
“Tutafuatilia hili la mishahara kwa karibu sana, maana asilimia
99.999 ya wafanyakazi wanafanya kazi nzuri na hawapokei rushwa lakini
wapo wachache sana ambao ni mabingwa wa rushwa na hao naomba
wajirekebishe haraka kabla sijaingia madarakani,” alisema.
Aliahidi pia kusimamia ili kubadilishwa kwa sheria ili wahitimu wa
vyuo vya elimu ya juu na kada nyingine wasitakiwe kuwa na uzoefu wa
miaka mingi kama kigezo cha kupata kazi serikalini na kwingineko akisema
hatua hiyo imekuwa inawafanya Watanzania kukosa kazi na wageni
kunufaika.
Alisema pia ataboresha miundombinu ya mji wa Arusha ikiwemo maji,
barabara za lami, ajira kwa vijana huku akisema suala la ajira kwa
vijana halihitaji ahadi za matumaini bali hatua madhubuti ambazo alisema
serikali yake ndiyo yenye majibu kwa mageuzi katika soko la ajira
nchini.
Kuhusu sekta ya mifugo aliahidi kuanzishwa kwa viwanda vya nyama ili
kuwezesha wafugaji kupata soko la mifugo yao na kuongeza kipato chao,
huku akisema Tanzania chini ya utawala wake itakuwa na kiwanda cha ngozi
Arusha kitakachozalisha ajira.
Alisema uwepo wa kiwanda hicho kutafanya kuzaliwa kwa viwanda vya
nyama, viatu, mikanda, maziwa na vinginevyo na hivyo kufanya bidhaa hizo
kuachwa kuagizwa kutoka nje hatua ambayo pia itakuza uchumi, kipato cha
wananchi na pia kuongeza pato la serikali.
Kinana na posho Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema mara
baada ya kuingia madarakani, CCM itamuomba Magufuli kufuta posho za
maofisa serikalini, na kuondoa kero kwa wananchi za uzembe na ufisadi,
akitolea mfano suala la mgawo wa umeme aliosema umekuwa kero kubwa kwa
wananchi.
Kinana alimuomba Magufuli pamoja na kutaifisha viwanda vya mijini na
vijijini, ambavyo wamiliki wake hawaviendeshi baada ya serikali
kuvibinafsisha, pia akomeshe mara moja vikao na posho serikalini kwa
kufuta vitu hivyo na kuwabana watendaji kufanya kazi, tofauti na ilivyo
sasa.
“Nchi hii sasa imekuwa ya vikao. Vikao ni vingi sana. Watumishi wengi
wanapoteza muda mwingi na pesa katika vikao,” alisema Kinana na
kumwomba Magufuli atakapochaguliwa kukomesha tabia hiyo.
Kinana alisema kuna tabia ya urasimu katika ofisi nyingi, ambapo
wananchi wanaotaka huduma katika ofisi hizo, wamekuwa wakizungushwa bila
kuhudumiwa na kupewa kauli za ‘njoo kesho’. Aliomba Magufuli kuondoa
urasimu huo.
Kuhusu mabadiliko, Kinana alisema wapo watu wanaodanganya kuwa
wataleta mabadiliko nchini. Alisema mabadiliko ya kweli yataletwa na Dk
Magufuli na CCM. “Kuna watu wanazungumza juu ya mabadiliko. Tunaomba
wananchi mtambue kuwa mabadiliko bora na ya kweli yataletwa na CCM na
Magufuli.
Serikali ya CCM ya Rais Jakaya Kikwete imeleta mabadiliko mengi ya
kiuchumi na kijamii na mabadiliko bora na ya kweli, yataendelea kuletwa
na Magufuli,” alisema Kinana na kuomba Watanzania kumpigia kura nyingi
Magufuli na wagombea ubunge na udiwani wa CCM.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 6 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment