JESHI la Polisi mkoani Simiyu linawashikilia watu sita, wanaotuhumiwa
kuwaua kwa kuwacharanga mapanga watu watano wa familia moja hivi
karibuni katika kijiji na kata ya Bugarama, wilayani Maswa.
Pia jeshi hilo lilieleza kuwa chanzo cha tukio hilo katika hatua za
awali kimegundulika kuwa ni mgogoro wa ardhi na imani za kishirikina na
kati ya watuhumiwa hao, mmoja ni mganga wa kienyeji.
Akitoa taarifa ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu,
Gemini Mushy alisema mbali na kukamatwa watu hao bado watuhumiwa wengine
wawili wanatafutwa baada ya kutenda kosa na kufanikiwa kutoroka.
Katika tukio hilo, waliouawa kwa kukatwa mapanga ni George Charles
(30) ambaye ni baba wa familia, mkewe Siku John (23) na watoto wao,
Mchambi George (7) Tuma George (5) na Amos George aliyekuwa na umri wa
miezi tisa.
Kwa mujibu wa Kamanda Mushy, waliokamatwa wakituhumiwa kwa mauaji
hayo ni Ntange Jisesa (30), Tarange Migata (25), Paul Joseph (23),
Migata Lusalaga (50), Jiherya Migata (30) akiwemo na mganga huyo wa
kienyeji.
Naye Mwenyekiti wa kijiji hicho, Christopher Kulwa alisema chanzo cha
tukio hilo kimeonekana kuwa watuhumiwa wote ambao walipigiwa kura ya
siri na wananchi, walikuwa na chuki juu ya familia iliyotendewa unyama
huo.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 6 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment