MAELFU ya wakazi wa Dar es Salaam jana waliacha shughuli zao zote
na kujiunga katika msafara wa mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Edward Lowassa, ambaye alikuwa na mikutano ya kampeni katika majimbo ya
Temeke, Segerea, Ubungo na Kawe.
Lowassa aliwasili Temeke katika Uwanja vya Mwembeyanga saa 05:20
asubuhi ambako alilakiwa na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza.
Akifuatana na Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye alishuhdia
wananchi waliokuwapo uwanjani hapo, muda wote wakiimba nyimbo mbalimbali
za kumsifu mgombea huyo wa Ukawa.
“Rais…Rais…Rais…tuna imani na wewe Lowassa, tumechoshwa na CCM,
Lowassa wewe ndiye tegemeo letu…kura zetu umepata, angalia ulivyo
tishio, unakitesa chama ulichokiacha…Ikulu sasa ni yako,” waliimba
wananchi hao.
Baada ya mkutano huo wa Mwembeyanga, Lowassa na msafara wake
walielekea Segerea ambako vijana watembea kwa miguu na waendesha
pikipiki (bodaboda) na bajaji walisindikiza msafara huo na kusababisha
magari yote katika barabara za Sokota na Maendela hadi Buguruni
kutokupitika.
Msafara huo uliwasili huo uliwasili katika Uwanja wa Shule ya Shule
ya Msingi Liwiti na kukuta umati wa watu umefurika ukiwa na shauku ya
kumuona.
Baadhi ya wananchi waliofika kwenye uwanja huo walikuwa wamebeba
mabango yenye ujumbe: ‘Lowassa kwanza familia baadaye’, ‘Magufuli
jiandae kuwa mlinzi wa Lowassa’, ‘Uwezo tunao sababu tunazo wananchi
tunahitaji mabadiliko’ na ‘Segerea ni Mtatiro tu wengine nendeni
mkaendelee na urembo wenu’ na mengineyo.
Hata hivyo, wakati Lowassa anapanda jukwaani kuhutubia, ghafla
lilitokea kundi kubwa la wananchi ambao walitembea kwa miguu kutoka
Temeke huku wakirukaruka na kuimba: “Rais…Rais…Rais…tumeamua tukufuate
huku huku, sasa waseme kama unatupa hela…tumekufuata kwa mapenzi yetu,
angalia tulivyo wengi, acha wao wajaze wasanii na kuwabeba watu kwenye
malori sisi tumetembea kwa miguu yetu kutoka Temeke,”.
Saa 07:45 Lowassa na msafara wake walimaliza kuwahutubia wananchi hao
na ulianza safari kuelekea Manzese katika Uwanja wa TP Uzuri Sinza
kupitia barabara ya Mandela hadi Ubungo.
Msafara huo ulifunga barabara za Tabata, Mandela na baadaye Morogoro
eneo la Ubungo ambako umati mkubwa wa watu pamoja na waendesha bodaboda
wa maeneo hayo nao walijiunga kwenye msafara huo na kuufanya kuzidi
kuwa mkubwa.
Ulipofika Ubungo, umati mkubwa wa watu ulikuwa umefurika pembezoni
mwa barabara ya Mandela huku wakishangilia na kunyoosha vidole viwili
juu, alama ambayo hutumiwa na Chadema.
Nyimbo mbalimbali ziliendelea kuimbwa na wananchi hao wengine
wakimtaka Lowassa asimame na kuwapungia mikono. “Rais… Rais… Rais…
tunaomba tukuone, sisi malofa, wapumbavu na masikini wewe ndiye
mkombozi wetu,” waliimba wananchi hao.
Wakati hayo yakiendelea, barabara zote katika eneo la Ubungo
zilifungwa kwa zaidi ya dakika 20, ndipo Lowassa alipoamua kusimama
na kuwapungia mkono wananchi hao.
Lowassa aliendelea kusimama kwenye gari lake la wazi hadi eneo la
Shekilango, Sinza kuelekea viwanja vya TP Uzuri Sinza ambako pia
alihutubia mkutano mkubwa wa kampeni kabla ya kuondoka tena kwenda
Viwanja vya Tanganyika Peackers katika Jimbo la Kawe.
Kama ilivyokuwa maeneo mengine, umati mkubwa wa wananchi hao
waliokuwapo katika viwanja hivyo nao walikuwa wakiimba nyimbo
mbalimbali zikiwamo: “Lowassa wewe tayari ni rais wetu, angalia
tumeacha kazi zetu tumekuja hapa tangu asubuhi ili tukusikilize, huyo
Magufuli si anajidai anajua ubodigadi sasa tunaomba aje kuwa mlinzi
wako…”
Nacho kikundi kingine cha vijana kilikuwa kikiimba: “Huyo Masaburi
(Didas, aliyekuwa meya wa Dar es Salaam na sasa anagombea ubunge Ubungo
kwa tiketi ya CCM) akaombe kura Magogoni…sisi hatumhitaji, kasababisha
watu wafe kwa kipindupindu, yeye kanenepa halafu eti anataka tumchague
awe mbunge wetu… hizi si dharau jamani? Tutamchague Kubenea kuwa mbunge
wetu wa Ubungo na rais wetu ni wewe Lowassa”.
Kikundi kingine cha vijana walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali huku
wengine wakiitikia kwa kibwagizo cha ‘Lowassa kama Ronaldo’, Lowassa
tukikuona tunachanganyikiwa kabisa, Magufuli hana hata mvuto…yaani wewe
nyota yako ni hatari,’.
Ahadi za Lowassa
Akiwa katika Uwanja wa Shule ya Msingi Liwiti, Lowassa alishindwa
kuzungumza kwa muda kutokana na furaha aliyoiita mahaba, baada ya kukuta
umati mkubwa umefurika.
Kabla ya kuwasalimia wananchi, Lowassa alijikuta akitabasamu na
kushindwa kuzungumza kwa sekunde kadhaa huku umati wa wananchi hao
wakiendelea kumshangilia.
“Jamani haya ni mapenzi au mahaba… nina furaha isiyo kifani na
ninasema hivi umati huu na shangwe hizi ni salamu kwa Chama Cha
Mapinduzi (CCM)… napenda kuwapelekea salamu kuwa wananchi wamenipokea
kwa shangwe na wanahitaji mabadiliko,”alisema Lowassa huku
akishangiliwa.
Alisema, “mkusanyiko huo ni salamu tosha kwa CCM kuwa mnahitajika mabadiliko na mimi nawaomba mnipe kura na mzilinde”.
Lowassa alisema anauchukia umaskini na kueleza kuwa baada ya miaka 50
ya uhuru sasa wananchi wanahitaji hali bora na wataipata kupitia Ukawa
na si CCM.
“ Ninachukia umaskini ndugu zangu…nawaambia hivi nitaongoza nchi kwa
spidi 120… ambaye hataweza kwenda na kasi yangu ataachia ngazi yeye
mwenyewe,” alisema.
Alisema anawashukuru wauguzi na madaktari ambao wameona umuhimu wa
mabadiliko baada ya kuvutana na hatimaye wamekubali matokeo na kuona
hakuna namna mabadiliko yanahitajika.
Lowassa alisema akiingia Ikulu siku 100 za mwanzo za utawala wake
atahakikisha ameimarisha mambo 11 ambayo yamekuwa kero kwa wananchi.
Alitaja vipaumbele vyake kuwa ni mfumo bora wa kodi, kuundwa kwa tume
ya kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji, kupunguza kodi kwa
wafanyakazi, kuongeza maslahi ya Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ), kuondoa kodi za wafanyabiashara ndogondogo na bodaboda
na kufuta ada kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu.
“Uwezo tunao na nia tunayo.. ndugu zetu CCM salamu ni hizi, wazipate
kuwa hawawezi kuzuia mafuriko haya kwani wameunda mfumo wa Teknohama kwa
ajili ya kuwakomesha watoto wa maskini lakini mimi nitaweka usawa kwa
wote kupata elimu bora,”alisema Lowassa.
MNYIKA
Naye Mgombea ubunge waKibamba kwa tiketi ya Chadema, John Mnyika
alisema wanachokifanya sasa ni kuzuia bao la mkono kwa kuwa rais tayari
wanaye.
Alisema Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian
Lubuva kueleza kuwa Chadema inawapa shida anakosea kwa sababu wanaompa
shida ni wananchi ambao wanahitaji mabadiliko.
Mnyika alisema hadi ifikapo Oktoba 4 mwaka huu, NEC iwe imetoa
utaratibu wa kueleweka kuruhusu wataalam wa Ukawa waupitie mfumo wa
upigaji kura katika kompyuta zikazotumiwa katika Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba.
“ Ni lazima tujihakikishie mfumo wa kompyuta zao kama tulivyoomba ili
kudhibiti bao la mkono vinginevyo.. hatutakubali ikifika hiyo Otoba 4
mwaka huu,’’alisema Mnyika.
SUMAYE
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye alisema zaidi ya mikoa 20
aliyopita wananchi wanahitaji mabadiliko na CCM haina historia ya
kukumbukwa zaidi ya kuwakandamiza wananchi kwa miaka 50 yao.
“Huyo Magufuli, mgombea wa CCM akiwa rais ni maumivu tu, mtu ambaye
anafanya uamuzi kwa kulipuka bila kuangalia athari wakati akiwa waziri,
itakuwaje akiwa rais?
“Huyo huyo Magufuli alivunja majengo ya Wakala wa Barabara (TANROADS)
Ubungo, lakini sasa eneo hilohilo hivi sasa linajengwa jengo jingine,
hivi eneo hilo limehama au bado lipo?” aliuliza Sumaye huku wananchi
wakiitikia, “bado lipo…”
“ Hadi sasa nchi inadaiwa Sh trilioni 45… madeni kutoka nje ni jambo
la aibu sana na mkumbuke mkimchagua mgombea wao kitakachofuata ni kulipa
madeni tu,”alisema Sumaye na kuongeza:
“Kuna deni la wakandarasi zaidi ya Sh bilioni 900 tunadaiwa…
ninawaambia kuwa tukifanya kosa CCM wakarejea madarakani tutakuwa
tunajiangamiza sisi wenyewe”.
Mbowe awataka vijana kukesha
Naye Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe aliwataka watanzania
kukesha wakijiandaa na kutafakari siku ya kuamkia kupiga kura ili kuanza
maandalizi safari ya uhakika itakayorudisha heshima ya nchi.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni kwenye viwanja vya Tanganyika
Parkers jana, Mbowe alisema usiku wa oktoba 24 siyo siku ya kulala kwa
kuwa ni siku ya ukombozi wa taifa.
“Tarehe 24 siyo siku ya kukesha disco, ni siku ya kufanya maandalizi
ya ukombozi wa taifa hili, hakuna kurudi nyuma baada ya kupiga kura,
piga hatua 100 kutoka kituo cha kura halafu linda kura….hakuna kulala
mpaka matokeo ya udiwani, ubunge na urais yatangazwe, tutakesha hadi
matokeo ya urais yatangazwe,” alisisitiza Mbowe.
Mbatia akanusha uvumi wa ushirikina
Naye Mwenyekiti Mwenza wa Umoja huo, James Mbatia alikanusha uvumi
ulioenea katika mitandao ya jamii na maeneo mbalimbali nchini kuwa
amekamatwa akiwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi akiwa na fuvu la kichwa cha
mtoto.
“Mimi na familia yangu ni wacha Mungu hatuamini katika ushirikina
nimekulia katika familia ya wacha Mungu hivyo siwezi kufanya kitu kama
hicho labda wao CCM, maana wao ndiyo waliotengeneza picha hiyo na
kuiweka mitandaoni,” alisema Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi.
Habari hii imeandaliwa na Elizabeth Hombo, Christina Gauluhanga, Tunu Nassoro na Adam Mkwepu
In Gazzeti la Mtanzania
Saturday, 3 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment