Friday, 2 October 2015

Tagged Under:

IMF yavutiwa na uchumi wa Tanzania

By: Unknown On: 23:47
  • Share The Gag

  • Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum.

    SHIRIKA la Fedha Duniani (IMF) limesema kuwa limevutiwa na kukua kwa uchumi wa Tanzania. Limesema uchumi wa Tanzania unakua kwa asilimia 7 na utaendelea kukua kwa kiwango hicho katika miezi iliyobakia mwaka huu hadi mwakani.
    Hayo yamo katika taarifa ya Ujumbe wa IMF, uliotembelea Tanzania kuanzia Septemba 17 hadi Septemba 30 mwaka huu. Ujumbe huo ulioongozwa na Herve Joy na ulikuja kufanya mapitio ya uchumi wa Tanzania.
    “Pato la Taifa lilitarajiwa kukua kwa asilima 6.5 katika robo ya kwanza ya mwaka huu na ongezeko kubwa katika uchumi lilitoka katika huduma za usafirishaji, uzalishaji wa umeme, teknolojia ya habari na mawasiliano na huduma za fedha,” ilisema taarifa hiyo.
    Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema katika hotuba yake ya Bajeti ya Serikali mwezi Juni mwaka huu kwamba uchumi utakua kwa asilimia 7 mwaka huu na asilimia 7.3 mwaka ujao.
    Ujumbe huo wa IMF pia ulisema mfumko wa bei wa Tanzania, ulipanda kidogo katika miezi michache iliyopita hadi kufikia asilimia 6.4 mwezi Agosti mwaka huu, na sababu kubwa ilikuwa ni ongezeko la bei ya vyakula na kushuka kwa viwango vya ubadilishanaji wa fedha.
    Ujumbe huo uliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuchukua hatua madhubuti za kuinua na kuboresha uchumi , ikiwemo kuweka sera nzuri za fedha na kuongeza mazao yanayouzwa nje ya nchi, hatua ambazo pia ziliimarisha Shilingi.
    Hatua hizo pamoja na nyinginezo, ziliboresha masoko ya ubadilishaji wa fedha za kigeni na biashara kati ya benki mbalimbali. Kwa sasa Shilingi ya Tanzania inakaribia kurejea katika hali yake ya kawaida, ilieleza taarifa hiyo ya IMF.
    Hata hivyo, ujumbe huo wa IMF ulieleza kuwa serikali haikufanikiwa kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yake ya hadi mwezi Juni mwaka huu ya ukusanyaji wa mapato.

    Created by GazetiLeo.

    0 comments:

    Post a Comment