*Amtaka amfuate Ukawa au amsamehe
*Atangaza atakuwa dikteta wa maendeleo
Na Fredy Azzah, Monduli
MGOMBEA Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward
Lowassa, ambaye anaungwa mkono na vyama vya upinzani vinavyounda Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jana alitangaza kuitua mbeleko aliyokuwa
akimbebea Mgombea Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Monduli,
Namelok Sokoine.
Vyama vinavyounda Ukawa ni pamoja na Chadema yenyewe, Chama cha
Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).
Lowassa alitangaza uamuzi wake huo katika mkutano wa kampeni
uliofanyika Uwanja wa Barafu, uliopo Mto wa Mbu, Wilaya ya Monduli,
baada ya baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kumhoji namna
anavyowaacha na Namelok ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, Hayati
Edward Moringe Sokoine.
Akijibu swali hilo, Lowassa alisema atakutana na Namelok kumshawishi
ili abadili msimamo wake wa kuendelea kuwa CCM na badala yake ajiunge
naye kwenye vuguvugu na mabadiliko katika Ukawa.
“Nimeongoza jimbo hili kwa miaka 20, nastahili kumfahamu atakayekuja
badala yangu, sasa kuna maneno maneno, wamepotea mabasi, wamepotea
malori, niachieni kidogo nifanyie kazi.
“Kesho nitakwenda Pemba nitarudi jioni, nitakutana na madiwani na
Namelok ili mambo yetu tuliyoongea tuulizane yamekuwaje. Nasema hivyo
kwa sababu nisingetaka kuvunja umoja wetu. Katika uchaguzi uliopita
tulikuwa na kauli, ‘tulihuzunika pamoja, tulifurahi pamoja na tutasonga
mbele pamoja,’ ningependa tubaki na kauli hiyo, kwa hali hiyo, hili
mniachie kesho tutakubaliana, akikataa kuingia basi la wengi, basi
itakuwa bahati mbaya,” alisema Lowassa.
Lowassa alitumia pia mkutano huo kumnadi Mgombea Ubunge wa Chadema wa
Jimbo la Monduli, Julius Kalanga, akimtaja kuwa ni jembe huku akikwepa
kumtaja kwa namna ya kumshambulia kisiasa au kuwashawishi wapigakura
kutomchagua Namelok.
Baadaye jioni Lowassa alifanya mkutano wa kampeni zake huko Babati,
mkoani Manyara na kueleza kuwa Serikali yake itakuwa rafiki kwa mama
ntilie, bodaboda na watu wote ambao wanahangaika kutafuta maendeleo.
“Katika serikali yangu mtu atakayesumbua hawa watu, mtu anaingiza
daladala yake barabarani anakamatwa huyo atakayemkamata nitamfunga,
najua watasema mimi ni dikteta, lakini ni dikteta wa maendeleo,” alisema
Lowassa.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, ambaye
amekuwa bega kwa bega na Lowassa katika shughuli za kampeni, alisema
anawashangaa baadhi ya viongozi wa CCM wanaodai kuwa amekuwa
akiilalamikia serikali wakati aliwahi kuwa huko.
Alisema alipotoka madarakani mwaka 2005 bei ya sukari ilikuwa Sh 500, lakini hivi sasa haikamatiki.
“Nilipoondoka niliacha unga wa sembe ukiwa Sh 200, lakini leo
haukamatiki, mchele Sh 600 lakini leo haukamatiki, kipande cha sabuni Sh
50 lakini leo hakikamatiki. Nimeondoka huko kwa kuwa serikali
imeshindwa kujibu hayo mambo,” alisema Sumaye.
Akimzungumzia Namelok, Sumaye alimtaja mwanasiasa huyo kijana kuwa ni
mdogo, ndugu yake na kwamba hana ugomvi naye, lakini kwa sababu
anagombea ubunge kupitia gari ambalo halina matairi afahamu kuwa yupo
kwenye genge ambalo halifai.
“Tutaongea naye aachane na hiyo kambi ya kijani aje, msije mkampigia
kura kwa sababu hatashinda, aje aungane na Lowassa. Lowassa atashinda
kwa zaidi ya asilimia 80, Magufuli mwenyewe amekata tamaa na CCM ndiyo
maana anasema ni kitanda chenye kunguni, CCM ni chama kilichojaa rushwa,
ufedhuli, Namelok kwa kuwa bado ni binti msikivu tutaongea naye,”
alisema Sumaye.
Mkutano wa kwanza wa Lowassa akiwa mpinzani
Lowassa, ambaye amekuwa Mbunge wa Monduli kwa miaka 20, jana alifanya
mkutano wa kwanza katika Jimbo la Monduli akiwa chama cha upinzani.
Licha ya mkutano wake wa jana kupangwa kufanyika saa 5:00 asubuhi,
tangu saa 1:30 asubuhi wananchi walianza kujitokeza uwanjani, huku
Lowassa mwenyewe akifika eneo la mkutano saa 7:58 mchana.
Akizungumza juu ya uongozi wake jimboni hapo na hatima yake, alisema:
“Nimesema napita Mto wa Mbu niwapungie mkono kwa sababu nitakuja kuaga
rasmi, watu uliokaa nao miaka 20 huwaagi hivi hivi. Nilishawahi kusema
watu tulihozunika pamoja tutafurahi pamoja.
“Nataka kila mwana Monduli anitafutie kura popote Tanzania, ni muhimu
kupata kura nyingi mno. Hawa jamaa ni mahodari wa kuiba kura kwa hiyo
lazima tupate kura nyingi,” alisema Lowassa.
Alisema kwa sasa hatakuwa tena mbunge wa jimbo hilo, ila atakuwa
mbunge wa zamani wa Monduli, hivyo anataka kuendelea kushirikiana nao
katika kutatua matatizo ya jimbo hilo.
“Nataka Monduli iendelee kubaki na amani ile ile, tusaidiane,
tuzikane, hata asiyekuwa kwenye chama chetu tumuelimishe siyo kutengana,
tuache ugomvi kati ya wakulima na wafugaji,” alisema.
Chanzo Gazeti la Mtanzania
Sunday, 4 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment