Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki amewataka waliovamia na
kujigawia maeneo ya watu wengine likiwamo la Waziri Mkuu mstaafu,
Frederick Sumaye na aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Ritha Mlaki
waondoke mara moja kwa kuwa wamevunja sheria.
Alisema
zaidi ya watu 2,000 wakiwamo waliobomolewa nyumba katika baadhi ya
maeneo jijini Dar es Salaam wamevamia na kujigawia mashamba hayo
yaliyopo Tegeta na Goba kinyume cha sheria.
“Kisa
wamevunjiwa nyumba zao walizojenga kinyume cha sheria ndiyo wameamua
kuvamia maeneo yasiyo yao, hili ni kosa kama makosa mengine, nawataka
waondoke haraka vinginevyo tutawachukulia hatua kali za kisheria,” alisema mkuu huyo wa mkoa.
Alisisitiza
kuwa agizo la Rais John Magufuli lilikuwa ni maeneo yaliyoachwa wazi
kuainishwa kwa ajili ya kupangiwa matumizi mengine na siyo kuruhusu watu
kuvamia bila taratibu.
Sadiki
alisema hakuna viwanja vilivyotengwa kwa ajili ya kuwagawia wananchi
waliokumbwa na bomoabomoa katika maeneo ya mabondeni.
Zaidi
ya nyumba 8,000 zilizojengwa kwenye Bonde la Mto Msimbazi, fukwe za
bahari na kando ya mito zimeanza kubomolewa kabla ya kusitishwa na
Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Sadiki alisema wananchi waliobomolewa nyumba
zao na ambao watakumbwa na operesheni hiyo wasitarajie kupatiwa viwanja
vya kujenga nyumba zao.
Bomoabomoa hiyo inaendeshwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ikiwalenga waliojenga kinyume cha sheria.
“Serikali
haina viwanja vinavyotosha kuzigawia familia zaidi ya 8,000
zitakazobomolewa, niwashauri tu wasiendelee kupoteza muda wao kwa
kuwasikiliza wanasiasa, watafute makazi mengine waende. Kama walivyovamia na kujenga ndivyo wanatakiwa kutafuta maeneo mengine wahamie,” alisema Sadick.
Alisema
viwanja 1,007 vya Mabwepande vilitolewa kwa wananchi waliokumbwa na
mafuriko mwaka 2011 ambao waliwekwa kwenye kambi baada ya kukosa
makazi,lakini cha kushangaza baadhi yao waliviuza viwanja hivyo kwa bei
ya chini na kurudi tena kwenye maeneo hatarishi.
Alisema
kaya zote zilizokosa makazi kutokana na mafuriko hayo zilipatiwa
maeneo. Waathirika 580 walitokea Ilala, Kinondoni 349 na Temeke 81.
“Kuna
upotoshaji unaendelea kwamba yapo maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya
kuwapatia wanaobomolewa sasa, jambo hili halina ukweli, ikumbukwe
tuligawa viwanja vya Mabwepande baada ya Rais (Jakaya Kikwete) kuagiza
tufanye hivyo ili kuwasaidia wale tu, waliokumbwa na mafuriko mwaka
2011,” alisema.
Credit; Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment