Kivuko cha Mv Kilombero 11 mkoani Morogoro kikiwa kimezama kwenye mto Kilombero jana.
WATU kadhaa wanahofiwa kufa maji baada ya kivuko cha Mv Kilombero 11
kinachovusha watu na magari katika mto Kilombero mkoani Morogoro,
kupinduka na kuzama. Ajali hiyo ilitokea wakati kikitokea wilaya ya
Ulanga kwenda upande wa Ifakara wilaya ya Kilombero.
Kivuko hicho ambacho idadi ya abiria waliokuwemo hakijafahamika mara
moja, kilibeba pia pikipiki, bajaji, baiskeli na magari kadhaa likiwemo
la Benki ya CRDB Tawi la Ifakara, ambalo dereva wake anahofiwa kuzama.
Hata hivyo, akitoa taarifa ya serikali bungeni jana, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu,
Jenista Mhagama alisema kivuko hicho kilikuwa na abiria 31, magari
matatu na bajaji mbili.
Mhagama alisema abiria 30 walifanikiwa kuokolewa na maiti mmoja
amepatikana. Aidha, Mkuu wa kivuko hicho, Fadhir Haroub alisema kilikuwa
katika safari ya mwisho siku hiyo na kwamba kilipofika katikati ya mto,
ulitokea upepo mkali na kukisukuma na nahodha alijitahidi kukiokoa,
lakini ikashindikana na hatimaye kugonga nguzo za daraja la muda, kisha
kusimama na kuzama.
Pamoja na hayo, alisema kilikuwa na magari matatu likiwemo lori aina
ya Fuso lililobeba mchele na Land Cruiser mbili, moja ni ya benki ya
CRDB na lingine la Kampuni ya Mitiki -KVTC na aina nyingine ya usafiri
zikiwemo bajaj, bodaboda na baiskeli na vyote vimezama na kutojulikana
kwa idadi ya watu waliofariki.
Katika ajali hiyo, watu wapatao 31 walijiokoa baada ya kuvaa ‘live
jacket’ zinazohifadhiwa kama tahadhari ndani ya kivuko hicho, akiwemo
Meneja wa CRDB Tawi la Ifakara, Joel Mwageni na wenzake wawili.
Hiyo ni ajali ya pili ya kuzama kwa kivuko katika mto Kilombero, ya
kwanza ikiwa ni ya Mv Kiu kilichokuwa na kamba na kusukumwa na boti,
kilichopinduka na kuzama majini mwaka 2002 na watu kupoteza maisha.
Baada ya hicho kuzama, serikali ilinunua kivuko kingine cha Mv
Kilombero I ambacho kilizinduliwa Oktoba 12, 2002 kikiwa na uwezo wa
kubeba tani 50 abiria na mizigo. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa
Mkoa, Leonard Paulo, tukio la kupinduka na kuzama kwa kivuko hicho,
lilitokea saa 1:15 juzi usiku kilipokuwa kinafanya safari kutokea upande
wa Ulanga kuelekea upande wa Ifakara.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa
akiwa katika eneo la tukio, aliahidi kushirikiana na wananchi wa wilaya
za Ulanga, Kilombero na Malinyi katika uokozi kwa kutuma vikosi vya
ulinzi na usalama kwa ajili ya kutafuta miili ya watu waliofariki dunia
kwa ajali ya kuzama kivuko hicho.
Alisema serikali imeweka mkakati wa kuharakisha ujenzi wa daraja la
mto Kilombero na tayari mkandarasi, Kampuni ya M/S China Railway 15
Group Corporation amepatiwa Sh milioni 885 kukamilisha ujenzi huo.
Mkuu wa Mkoa, Dk Rajab Rutengwe, alikuwepo mjini Ifakara kwa ajili ya
kupata taarifa sahihi na hatua za kuchukuliwa, zikiwemo za kibinadamu
na urejeshaji wa huduma za usafiri kati ya Kilombero na Ulanga.
Chanzo Gazeti la habariLeo.
Thursday, 28 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment