*Ni wa Kinyerezi II uliogharimu Mabilioni
Na Jonas Mushi, Dar es Salaam
HARUFU ya kuwapo jipu la ufisadi katika mradi mkubwa wa umeme wa
Kinyerezi II imebainika, huku Serikali ikitoa dhamana kwa kampuni
inayoujenga.
Mradi huo uliozinduliwa na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, umegharimu zaidi ya Sh trilioni 1.6.
Kutokana na namna ilivyoendeshwa tenda hadi kupatikana Kampuni ya
Sumitomo ya nchini Japan, baadhi ya wanasiasa walipiga kelele kuhusu
gharama kubwa kuliko mahitaji halisi ya mradi huo.
Fedha za ujenzi wa mradi wa Kinyerezi II zinatokana na ubia kati ya
Serikali ya Tanzania na Japan wakati ujenzi wa Kinyerezi III na IV
zitatokana na ubia kati ya Serikali na kampuni ya Kichina.
Taarifa za ndani kutoka ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),
zinaeleza kwamba asilimia 12 ya fedha hizo zinatoka serikalini, huku
nyingine zikiwa ni mkopo kutoka katika benki moja ya nchini Japan.
Mradi huo unatarajia kuzalisha umeme megawati 239.5, ambapo mitambo yake itatumia gesi asilia kutoka Mtwara.
Taarifa zinaeleza kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa mitambo ya
kusafishia gesi asilia katika mikoa ya Mtwara na Lindi na pia ujenzi wa
bomba kuu la kusafirisha gesi asilia la inchi 36 kutoka Mtwara.
GHARAMA YA MRADI
Kwa mujibu wa mkataba ulioingiwa kati ya Tanesco na Kampuni ya
Sumitomo iliyopewa tenda hiyo kwa njia ya kawaida bila kutangazwa,
gharama za mradi ni kubwa na bei ya uuzaji wa umeme ukishazalishwa ni ya
juu kulinganisha na kampuni nyingine.
Kampuni ya Tallawara Power Station ya nchini Australia ilionyesha nia
ya kujenga mradi huo kwa gharama ya dola milioni 350 na kuiuzia Tanesco
umeme kwa dola 875 kila kilowati moja wakati Sumitomo ikiuza kwa dola
1,488.
Serikali ya Tanzania ilisaini mkataba huo wa ujenzi wa mradi huo
mwishoni mwa mwaka jana na hata kutoa dhamana kwa kampuni hiyo ambayo
tayari imeshapata fedha za mkopo, huku mradi ukiwa bado unasuasua kuanza
kujengwa.
MASWALI TATA
Pamoja na Serikali kuonyesha nia njema ya ujenzi wa mtambo wa
Kinyerezi II, lakini bado kumekuwa na maswali ambayo yanakosa majibu
ikiwamo kwanini mradi huo umetolewa kwa kampuni hiyo kwa mfumo wa
kawaida bila kufuata sheria za manunuzi.
Mkopo uliokopwa na Sumitomo kwa dhamana ya Serikali huku wao wakiwa
hawana kitu, nani ataulipa pamoja na riba yake kwa kila mwezi?
Kampuni ya Sumitomo itaendesha mradi huo kwa ubia ambapo yenyewe
itakuwa na hisa asilimia 60 na Serikali asilimia 40 je, kwanini hakuna
uwazi katika hili?
Ingawa hivi sasa Serikali ipo katika vita dhidi ya ufisadi je,
viongozi wake wanajua kuwa kuna hatari ya kupoteza zaidi ya Sh bilioni
360 katika mradi huu huku mwekezaji aliyepewa dhamana akinufaika yeye?
KAULI YA TANESCO
MTANZANI ilipomtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika Tanesco,
Mhandisi Felchesmi Mramba, alisema taarifa hizo si sahihi na hakuna
sheria iliyokiukwa.
“Takwimu unazonipa hazina ukweli wowote na kama unataka taarifa
kuhusu mradi wa Kinyerezi II njoo nikupeleke kwa wasimamizi wa mradi
waweze kukupa taarifa sahihi za mradi huo,” alisema Mhandisi Mramba.
Chanzo Mtanzania.
Thursday, 14 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment